Afisa wa Trump: Wanahabari wamekuwa 'chama cha upinzani'

Chanzo cha picha, Reuters
Mkuu wa mikakati wa Donald Trump amesema vyombo vikuu vya habari nchini Marekani vimekuwa "chama cha upinzani" na kusema vinafaa "kufyata ulimi".
Stephen Bannon ameambia New York Times kwamba amshirika mengi ya habari yanajihisi "kuaibishwa" kutokana na kushindwa kutabiri ushindi wa Trump kwenye uchaguzi mkuu Novemba.
Mashirika ya habari yametofautiana na ikulu ya White House kuhusu idadi ya watu waliohudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Bw Trump.
Aidha, wametilia shaka madai kwamba kuna mamilioni ya watu ambao hawakufaa kupiga kura waliopiga kura katika uchaguzini.
Akihojiwa na gazeti hilo kwa njia ya simu, Bw Bannon amesema "vyombo vya habari vinafaa kuaibika na kuona haya na kufyata ndimi zao na kusikiza yanayojiri kwa muda tu."
"Mashirika ya habari hapa ndiyo chama cha upinzani," alisema kabla ya kuongeza muda mfupi baadaye "na si chama cha Democratic".
Bw Bannon alisema mashirika ya habari "hayaifahamu vyema nchi hii".
"Bado hayajaelewa ni kwa nini Donald Trump ndiye rais wa Marekani".
Wakati wa mahojiano hayo, alizungumzia sana kuhusu mashirika makuu ya habari, ingawa alitaja moja kwa moja The New York Times na The Washington Post.
Bw Bannon alikuwa msimamizi wa mtandao wa siasa za mrengo wa kulia wa Breitbart News hadi Agosti na baadaye akawa afisa mkuu wa kampeni za Donald Trump miezi ya mwisho ya kampeni kabla ya uchaguzi Novemba.












