Ndege iliyokuwa na timu ya Brazil iliishiwa na mafuta

Chanzo cha picha, AP
Utawala nchini Colombia unasema kuwa kuna ushahidi kuwa ndege iliyokuwa imewabeba wachezaji ya klabu ya Brazil ilianguka baada ya kuishiwa mafuta ilipojaribu kutua.
Ndege hiyo haikuwa na mafuta ilipokuwa ikitua, afisa mmoja alisema, akinukuu sauti ya rubani aliyekuwa akiomba ruhusa ya kutua kutokana na kuishiwa mafuta na hitilafu ya mitambo ya umeme.

Chanzo cha picha, EPA
Mji wa Bogota ulitajwa wakati wa ratiba ya safari kama mahala ambapo ndege ingeongeza mafuta lakini ndege hiyo haikutua mjini humo.
Ndege giyo iliangua eneo lenye milima siku ya Jumatatu. Ni watu 6 kati ya 77 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walionusurika.
Ndege hiyo ilikuwa na timu ya Chapecoense ya Brazil ambayo ilitarajiwa kucheza fainali dhidi ya klabu ya Atletico Nacional mjini Medellin siku ya Jumatano.

Chanzo cha picha, Reuters
Timu hiyo ilisafiri kutoka mjini Sao Paulo hadi Santa Cruz ikitumia ndege ya kawaida ya abiria, kabla ya kubadilisha na kusafiri kwa ndege ya kukodishwa.
Rubani alikuwa na uamuzi wa kuongeza mafuta mjini Bogota, lakini akaamua kuelekea Medellin.
Alipokaribia Medellin, rubani aliomba ruhusa ya kutua kutokana na matatizo ya mafuta, lakini ndege nyingine kutoka shirika la ndege la VivaColombia ilikuwa ikisubiri kutua kutoka na kuvuja kwa mafuta.

Chanzo cha picha, Reuters
Rubani wa ndege iliyoanguka anasikika akiomba kwa dharura kuelekezwa kwa uwanja wa ndege kabla ya sauti hiyo kuzima.
Maafisa wanasema kuwa vifaa vya kurekodi sauti vitapelekwa nchini Uingereza kufunguliwa kwa uchunguzi.












