Mfalme akamatwa kwa kuchochea ghasia Uganda

Ramani ya Uganda
Maelezo ya picha, Ramani ya Uganda

Polisi nchini Uganda wanasema watu 50 wameuawa, katika mapambano baina ya askari wa usalama na kundi jipya lenye silaha, linalopigana kutaka kujitenga, magharibi mwa nchi.

Polisi wamemkamata mfalme wa kabila la huko, Charles Wesley Mumbere, mfalme wa Rwenzururu, ambaye wanamshutumu kwa kuchochea fujo hizo.

Amekanusha kuwa amehusika.

Polisi pia wanasema wamewakamata wapiganaji kadha walipovamia kasri ya mfalme huyo mjini Kasese, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.

Eneo hilo dogo limekuwa na mvutano na serikali ya Uganda kwa muda mrefu, na linavutana piya na eneo la Mfalme wa Toro.