Kenya: Mpango wa Ruto wa kusafiri bila viza wageuka kuwa magumu kwa baadhi ya watu

v

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Priya Sippy
    • Nafasi, BBC

Rais wa Kenya William Ruto alipongezwa mwaka jana alipotangaza kuwa nchi yake itaruhusu kuingia bila viza kwa wageni kutoka Afrika, lakini wengi wameshangazwa na masharti mapya ambayo yameleta gharama mpya.

Adio, raia wa Zimbabwe anayeishi Ujerumani, hakuwa akitarajia matatizo yoyote katika uwanja wa ndege wa Bremen alipowasili kwa ndege kuelekea Kenya mapema mwezi huu.

Lakini kwenye dawati la ukaguzi aliombwa aonyeshe hati inayosema ana kibali cha kuingia Kenya.

"Kulitokea mabishano mafupi kwenye kaunta. Nilisisitiza, silazima niwe nacho," alisema kijana huyo wa miaka 33 ambaye anafanya kazi katika sekta ya teknolojia.

Raia wa Zimbabwe, pamoja na wa nchi nyingine zaidi ya 40 zikiwemo kadhaa kutoka Afrika, huko zamani waliweza kufika Kenya, kupata muhuri wa paspoti yao na kuingia bila kulipa.

Kuingia bila viza

bv

Chanzo cha picha, XINHUA/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Rais wa Rwanda Paul Kagame alizindua pasipoti ya Afrika mwaka 2016 lakini bado haitumiki

Kenya ilipotangaza haitotaka viza kuanzia tarehe 1 Januari 2024, Adio alifikiri sheria zile zile zitatumika.

"Mara nilipoperuzi simu yangu ili kupata maelezo mapya kuhusu kuingia Kenya, ndipo nikagundua kuingia bila viza haimaanishi ni kuingia bila viza moja kwa moja," aliambia BBC.

Kama wengine, Adio alikuwa na fikra kwamba sera mpya ya Kenya ya kutokuwa na visa ingerahisisha usafiri.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini chini ya sheria mpya, wasafiri lazima wapate Idhini ya Usafiri wa Kielektroniki (ETA) kila mara wanapoingia Kenya.

ETA ni ya kuingia mara moja na ni halali kwa siku 90. Inagharimu dola za kimarekani 30 na inachukua hadi siku tatu kutolewa.

Ni raia tu kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao hawahitaji kuwa na ETA kwa sasa.

Hati zinazohitajika ili kupata ETA zinajumuisha maelezo ya safari ya ndege na uthibitisho wa hoteli unayokwenda.

"Kwa watu kama mimi, ni usumbufu. Hapo awali, tungeweza kuja Kenya bila kuhitaji chochote," alisema Adio.

Wakili wa uhamiaji wa Kenya Davis Nyagah anaamini ETA kimsingi ni "viza chini ya jina lingine."

"Kwa mtazamo wa kisheria, hakuna tofauti kati ya ETA na viza. Tofauti pekee ni kwamba Kenya haitaweka tena kikaratasi cha viza kwenye paspoti yako," aliambia BBC.

Pia inaonekana ni njia ya kuongeza mapato kwani wageni wote lazima walipe dola za kimarekani 30 kila wanapoingia. Hapo awali wasafiri walilipa dola 50 kwa viza ya kuingia mara nyingi ambayo inaweza kuwa halali kwa miaka kadhaa.

Mfumo huu wa ETA sio mpya, unatumiwa na Marekani, Canada na Australia, na Umoja wa Ulaya utautumia hivi karibuni.

Lakini nchi nyingine zisizo na viza barani Afrika, kama vile Rwanda, hazihitaji idhini yoyote kabla ya kuwasili na hakuna gharama ya kuingia kwa wasafiri.

Rwanda ilisema imepata ongezeko la 14% ya wageni wa Afrika kwa mwaka baada ya kuondoa viza 2018. Ilikuwa inagharimu dola 30, lakini sasa watu wanaweza kwenda na kukaa hadi siku 30 bila kulipa.

Bado kuna Changamoto

nb

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mamlaka ya Kenya inasema mfumo wa ETA unapaswa kurahisisha mambo kwa wasafi

Salim Swaleh, katibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Kenya, aliambia BBC kuwa ETA ni muhimu kwa ajili ya kuwachunguza wasafiri.

"Ugaidi ni moja ya kitisho cha kimataifa kwa sasa, kwa hivyo tunahitaji mbinu za kuhakikisha kila mtu anayekuja Kenya [sio hatari] kwa nchi," alisema.

Kenya imekuwa ikilengwa na wanamgambo wa kijihadi wa al-Shabab kutoka nchi jirani ya Somalia.

Wanauchumi wanasema kupunguza vikwazo vya usafiri ni muhimu kwa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, ambalo linalenga kuunda soko moja barani Afrika. Pia kumekuwa na maono ya kuunda pasipoti moja ya Afrika.

"Urahisi wa kusafiri ni muhimu sana kuvutia watalii na biashara," alisema Anthony Mveyange, mwanauchumi na mtaalamu wa sera za umma anayeishi Kenya.

"Nadhani ETA inaweza kuathiri uchumi wa Kenya katika muda mfupi hadi wa kati kwa njia tofauti."

Msemaji wa serikali ya Kenya, Isaac Maigua Mwaura, alikiri kwa BBC kwamba ETA, kwa hatua za awali imeleta matatizo lakini anasema yataondoka kadiri muda unavyosonga.

‘Zaidi ya maombi 60,000 yameshughulikiwa hadi sasa na huduma hiyo kwa sasa inaweza kushughulikia maombi 5,000 kwa siku,’’ aliongeza.

Mambo si mabaya

gfv

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Rais wa Kenya, William Ruto

Kufikia mwisho wa 2022, ni robo tu ya safari kati ya nchi za bara la Afrika na Waafrika zinafanywa bila viza, kwa mujibu wa Africa Visa Openness Index.

Hata hivyo, watafiti wanasema mambo yanaelekea vizuri kwenye uhuru wa kutembea.

Nchi kadhaa zikiwemo Ghana na Afrika Kusini, Botswana na Zimbabwe, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda zilianzisha mikataba baina ya nchi mbili za kuondoa viza.

Angola ilianzisha kuingia bila viza kwa nchi 98, yakiwemo mataifa 14 ya Afrika.

Nchi nne - Benin, Rwanda, Shelisheli na Gambia – zimeondoa viza kwa raia wa Afrika.

Nchi 30 bado zinahitaji raia wa zaidi ya nusu ya nchi za bara la Afruja kupata viza kabla ya kusafiri.

Libya, Sudan, Equatorial Guinea, Eritrea, Sudan Kusini na Misri ni baadhi ya mataifa yenye masharti magumu zaidi ya viza.

"Barani Afrika, haijalishi nchi ni ndogo kiasi gani, bado kuna mchakato mrefu wa kupitia," anasema Adio.

Kwa mtazamo wake, kuna mengi zaidi yanahitajika kufanywa.