Mwanafunzi wa miaka 84 alivyowachochea wengine wengi kupata elimu

Kimani Maruge

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kimani Maruge alijifunza jinsi ya kushika penseli akiwa na umri wa miaka 84.
    • Author, Vicky Farncombe
    • Nafasi, BBC Witness History
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mnamo 2004, Kimani Maruge alikua mwanamume mzee zaidi kuanza shule ya msingi alipojiunga na Shule ya Msingi ya Kapkenduiywo nchini Kenya.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 84 alikuwa mwanajeshi wa zamani ambaye alipigana dhidi ya utawala wa kikoloni katika harakati za Mau Mau kudai uhuru.

Hakusoma shule akiwa mtoto kwa hivyo serikali ya Kenya ilipofuta karo zote za elimu ya msingi ya umma, aliona fursa yake ya kujifunza kusoma na kuandika.

Aliyekuwa mwalimu wa Kimani Jane Obinchu anasimulia hadithi yake, ambayo iliwatia moyo watu kote ulimwenguni.

Sio mzee sana

Ni Oktoba 2003 na mwalimu mkuu Jane Obinchu kutoka Shule ya Msingi ya Kapkenduiywo huko Eldoret, kilomita 320 kutoka Nairobi alisikia mtu akibisha hodi alipokuwa akijiandaa kwa mwaka uliofuata wa shule.

Kimani Maruge

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kimani Maruge alichochewa na hamu yake ya kusoma biblia

Nje ya mlango alikuwa Kimani Maruge. Alimwambia kwamba alitaka kuchukua fursa ya sheria mpya nchini Kenya, inayotoa elimu ya bure katika shule za msingi za serikali.

Jane alichanganyikiwa na hakuwa na uhakika wa kumuongeza mzee huyo kwenye daftari lake.

"Tulimfpuuza. Tukamwambia: "Wewe ni mzee sana kujifunza." Kwa hivyo, ili kumuondoa, nilimwambia arudi Januari 2004," Jane aliiambia BBC.

Lakini Kimani hakukata tamaa.

"Nilishangaa sana, kumuona tena shule zilipofunguliwa mwaka 2004, alikuwa karibu na ofisi yangu na amevaa sare za shule na alikuwa na begi na vitabu vichache vya mazoezi na penseli kwenye begi," anakumbuka Jane.

Jane alimwomba tena arudi baada ya wiki moja. Kimani aliporudi tena, aliamua kuzungumza naye.

Kuhamasishwa na maono

Kimani alimwambia kwamba hakushawishika na kile alichosikia kutoka kwa mhubiri kanisani ni kweli. Alitoka nje ya kanisa kwa ukaidi. Akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake, alihisi kisunzi na kupata maono.

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kimani Maruge aliendelea na elimu hata alipokuwa akiishi kwenye hema.

“Aliambiwa aje shuleni kwetu ili aweze kusaidiwa kujifunza kusoma ili aweze kujisomea Biblia,” anasema Jane.

"Kisha akaelezea kile alichopata katika maono. Alikuwa ameambiwa kwamba kuna mwanamke ambaye angemsaidia kujua kusoma. Na akasema kwamba ni mimi ambaye aliniona katika maono yake."

Jane alimuandikisha. Siku ya kwanza ya muhula huo, Kimani alifika kwa wakati na akiwa nadhifu akiwa amevalia sare zake mpya. Utayari wake wa kupata elimu ya msingi ulizua wimbi la msisimko.

Alikuwa akienda kucheza na watoto huku akitembea na fimbo.

Miaka michache baadaye, Kimani alieleza azma yake.

"Sababu iliyonifanya kutaka kusoma ni kuwaonyesha watoto wa Kenya na dunia nzima kwamba elimu ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote, zaidi ya kuwa tajiri. Utajiri wa kweli unaelimishwa," Kimani alieleza alipokuwa akizungumza na Reuters mwaka wa 2006.

Changamoto

Baadhi ya wazazi hawakufurahi kumuona mzee pamoja na watoto wao darasani. Walifanya maandamano.

tt

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kimani Maruge alishiriki kikamilifu katika michezo na watoto wengine.

Jane aliogopa. Lakini wanafunzi wake mwenyewe walitoka darasani na kuwapinga wazazi wao.

Bila kukata tamaa baadhi ya wazazi waliwasilisha malalamishi kwa idara ya elimu na kumfanya Jane ahamishwe.

Jane alipigana na akarudishwa katika kazi yake ya zamani. Aliweza kupata ukaribu na Kimani na kumfundisha kusoma.

"Kumbukumbu zangu bora zaidi alipokuwa akijaribu kutamka silabi," Jane anaendelea.

"Ilikuwa ya kusisimua na wakati wa masomo ya kuimba, aliweza kuimba na kufanya masomo mengine ambayo wanafunzi wengine walikuwa wakifanya."

Kimani alianza kuonyesha matokeo. Siku moja Kimani alichukua Biblia na kusoma, Yohana 316.

"Huo ndio ulikuwa mstari wa kwanza aliousoma. Unaangazia kuhusu Mungu kumtuma Mwana wake wa pekee kufa kwa ajili ya dhambi zetu.."

"Tulifurahi aliposoma na tulitokwa na machozi."

Jane aliamini kwa mwendo huo maono ya Kimani yalitimia.

Utambuzi wa kimataifa

Msisimko zaidi ulifuatia hatua ya mzee Kimani Maruge kutafuta elimu licha ya umri wake mkubwa.

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alifurahia safari yake ya Marekani lakini Kimani Maruge hakuwa na uhakika kwa nini hakuna mtu aliyemwalika nyumbani kwake.

Mnamo 2005, Kimani na Jane walipata fursa ya kusafiri hadi New York Marekani kuwasilisha ujumbe kwa Umoja wa Mataifa. Safari hiyo ilipangwa na mashirika ya misaada ya kimataifa yanayokuza elimu.

Picha za Reuters za Kimani huko New York zikimuonyesha akiwa amepanda basi la shule ya Marekani la rangi ya njano la kupitia Times Square, akitembea na fimbo yake nje ya Jengo la Empire State na kuamkuana na afisa wa polisi aliyepanda.

Lakini, moyoni mwake, hakufurahishwa sana na ukaribisho huo.

"Hakupokelewa Marekani kama alivyotarajia. Aliendelea kuuliza kwa nini hatukualikwa kwa nyumba ya mtu, kama ilivyo Afrika."

Pia alikosa chakula chake cha Kenya.

Hata hivyo, alitoa ujumbe wazi kwa Umoja wa Mataifa.

"Ninatumai kwamba kila mtu duniani kote atapata ujumbe na kwamba wale ambao hawajaweza kwenda shule wataweza kwenda shule."

Urithi

Nyumbani nchini Kenya, Kimani aliteuliwa kuwa mkuu wa wanafunzi wa shule yake. Hadithi yake iliingia kwenye kitabu cha kumbukumbu cha Guinness.

Alifariki mwaka wa 2009 na mwaka uliofuata maisha yake yakageuzwa kuwa filamu iitwayo The First Grader.

Mwaka uliofuata, Priscilla Sitienei, mkunga Mkenya mwenye umri wa miaka 85, alianza shule ya msingi kujifunza kuandika, na alishiriki madarasa na wajukuu zake sita na watoto kadhaa ambao alikuwa amewasaidia mama zao kujifungua.

Priscilla Sitienei

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Priscilla Sitienei alikuwa shuleni hadi kifo chake

Ingawa alianza mwaka mmoja zaidi ya Maruge, aliweka rekodi yake mwenyewe: alipofariki mwaka 2022, alikuwa bado anasoma na, akiwa na umri wa miaka 99, anaaminika kuwa mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri mkubwa zaidi duniani.

“Kitu ninachojivunia ni kwamba wazee wengi walirejea shuleni, wakiwemo wafanyakazi wangu wengi walirejea madarasani ili kuendeleza masomo yao,” anahitimisha Jane Obinchu.

"Ilinifanya nihisi kama Mungu alikuwa na kusudi kwangu, na kusudi lilikuwa kumsaidia Kamani kujifunza kusoma na kuandika."