Kwa nini Israel ina wasiwasi kuhusu Saudia kununua ndege za kivita za F-35 kutoka Marekani?

Chanzo cha picha, Win McNamee/Getty Images
Katika uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia, masuala kadhaa muhimu, kama vile mikataba ya usalama na kuanzisha uhusiano na Israel, yamekuwa yakijadiliwa mara kwa mara.
Huku Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman akitarajiwa kuzuru Marekani hivi karibuni, suala la Saudi Arabia kununua ndege za kivita za F-35 kutoka Marekani limeibuka tena.
Sehemu mbili za habari zimeibuka kuhusu hili. Kwanza, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeidhinisha mkataba huo wa mabilioni ya dola. Pili, imetangazwa kuwa Saudi Arabia itanunua ndege 48 kutoka Marekani chini ya mkataba huu.
Shirika la habari la Reuters liliripoti habari hii, likiwanukuu maafisa wanaofahamu mpango huo wa F-35.
F-35, bunge la Congress na Saudi Arabia
Hata hivyo, njia ya kufikia makubaliano haya haiko wazi kwa wakati huu, na makubaliano hayo yanahitaji idhini ya pande zote tatu: serikali ya Marekani, Rais wa Marekani, na Congress kukamilishwa.
Mwandishi wa Saudia Mubarak Al-Attiyah alisema kuwa Saudi Arabia inaelewa kuwa mikataba hiyo inahitaji, kwa mujibu wa sheria, sio tu kuidhinishwa na serikali ya Marekani bali pia na bunge.
Akizungumza na BBC Urdu, alisema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump anaweza tu kusonga mbele na mpango huo ikiwa bunge la Marekani litamuunga mkono.
Mubarak al-Attiyah anasema kwamba Wanademokrasia na wanachama wa Congress watashinikiza kuhalalisha uhusiano wa Saudi-Israel kuhusiana na makubaliano haya.
Trump amechukua hatua za kisheria kuidhinisha mpango huo kwa sababu anaichukulia Saudi Arabia kuwa mshirika wa kimkakati na kwa hivyo anaamini kuwa kukidhi mahitaji yake ya usalama ni muhimu chini ya sera ya kigeni ya Marekani.
Mubarak al-Attiyah anasema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameeleza wasiwasi wake mara kadhaa kwamba Saudi Arabia inaweza kununua zana hizo kwa maadui wa Marekani kama vile China na Urusi iwapo Marekani itakataa kutimiza matakwa ya usalama ya Saudi Arabia.
Al-Attiyah alieleza kuwa Saudi Arabia imezungumza mara kwa mara kuhusu ununuzi wa aina nyingine za zana za kijeshi na usalama, pamoja na ndege za kivita.

Chanzo cha picha, SAUL LOEB/AFP via Getty Images
Wasiwasi wa Israeli kuhusu makubaliano haya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iwapo makubaliano haya yatatimizwa, yataashiria mabadiliko makubwa katika sera ya mambo ya nje ya Marekani, na uwezekano wa kutoa changamoto kwa nguvu za kijeshi za Israel katika Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, makubaliano haya na Saudi Arabia yanaweza kujumuisha masharti na vikwazo vitakavyohakikisha utawala wa kijeshi wa Israel katika eneo hilo.
Trump anataka kukamilisha mpango huo kwa sababu anaelewa nia ya uongozi wa Saudia. Mubarak al-Attiyah anasema Trump anaamini lengo la Saudi Arabia linakwenda zaidi ya kulinda mipaka yake.
Al-Attiyah anasema Rais Trump pia anajua kwamba Saudi Arabia, tofauti na baadhi ya majirani zake katika eneo hilo, haina malengo ya kujitanua.
Wataalamu wanasema Israel haitaki Marekani kuiuzia Saudi Arabia ndege za kivita za F-35.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel, makubaliano hayo yanaweza kuwa tishio kubwa kwa usalama wa Israel katika siku zijazo iwapo uhusiano wake na nchi nyingine za Mashariki ya Kati hautarejea katika hali yake ya kawaida.
Lakini, kuhusu Saudi Arabia, Mubarak Al-Attiyah pia anaamini kwamba haitaki kubadilisha sera na wajibu wake katika masuala ya nchi za Kiarabu hivi sasa.
Suala muhimu ni Palestina, na Saudi Arabia inaamini kuwa taifa huru la Palestina linapaswa kuundwa kwa kuzingatia mipaka ya 1967.
Hili ni sharti la msingi kwa mazungumzo yoyote juu ya mustakabali wa Mashariki ya Kati.
Al-Attiyah anasema Israel inahofia kwamba Saudi Arabia inaweza kushiriki teknolojia ya ndege ya kivita ya F-35 na Urusi, China au Iran. Hilo likitokea, litaipa Iran hatua karibu na usalama na kupunguza utawala wa Israel juu yake.
Wasiwasi kama huo uliibuliwa mapema mwaka wa 2020, wakati Marekani ilipopangiwa kuuza ndege za F-35 kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) chini ya Makubaliano ya Abraham. Hatahivyo, mpango huo haukuweza kupiga hatua.
Miongoni mwa masharti ya makubaliano hayo, Marekani iliweka vikwazo kadhaa kwa uendeshaji wa ndege hiyo, ikiwa ni pamoja na masharti ya kutumia ndege hiyo.
Marekani ilikuwa na wasiwasi kwamba uhamisho wa teknolojia ungetokea kutokana na uhusiano wa kina wa UAE na China.
Je, mwelekeo wa uhusiano wa Saudia na Marekani utabadilika?
Trump alifungua milango ya mikataba ya silaha kwa Saudi Arabia katika muhula wake wa pili.
Mwezi Mei mwaka huu, Marekani na Saudi Arabia zilitia saini makubaliano makubwa ya ulinzi, yanayoelezwa kuwa makubaliano makubwa zaidi ya ushirikiano wa kiulinzi katika historia ya Marekani.
Mkataba huo ulitiwa saini wakati wa safari ya Trump nchini Saudi Arabia, Qatar, na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ikulu ya Marekani, Marekani imetia saini mkataba wa kina na Saudi Arabia wenye thamani ya dola bilioni 600. Mkataba wa ulinzi wenye thamani ya dola bilioni 142 ni sehemu ya makubaliano haya ya kina. Chini ya makubaliano hayo Saudia itanunua ndege za kivita za F-35 kutoka kwa Marekani.
Hata hivyo, jaribio la kweli la mpango wa ndege ya kivita ya F-35 litafanyika katika kumbi za Bunge la Marekani.
Mubarak al-Attiyah anasema kuwa moja ya sifa maalumu za uhusiano wa Saudia na Marekani chini ya mwana mfalme wa Saudia na utawala wa Trump ni kwamba mafaili yote yanajadiliwa na pande zote mbili, na tofauti za kimtazamo haziruhusiwi kuwa vikwazo katika uhusiano huo.
Anasema pia lengo la ziara ya mwana mfalme wa Saudia nchini Marekani sio kukamilisha makubaliano ya silaha, bali ni kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Ni wazi kuwa mikataba ya usalama itajadiliwa katika kipindi hiki.
Kuhusu Saudi Arabia, Mubarak al-Attiyah alisema kuwa inapitisha sera ya usalama kulingana na chaguzi nyingine, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita za F-35.
Anasema mjadala wa F-35 ulikuwa muhimu katika safari ya mwana mfalme wa Saudi Marekani, lakini haikuwa sababu kuu iliyoamua mahusiano.
Ndege ya kivita au dhamana ya usalama?

Chanzo cha picha, Win McNamee/Getty Images
Hakuna shaka kuwa Saudi Arabia imejitolea kununua ndege za kivita za F-35 kutoka Marekani.
Lakini lengo lake ni kuhitimisha makubaliano ya kina ya usalama na Marekani ili kuilinda Saudi Arabia endapo itatokea shambulio lolote.
Hivi majuzi, Marekani ilitangaza makubaliano ya usalama ya Marekani na Qatar, ambapo mashambulizi yoyote dhidi ya Qatar yatazingatiwa kuwa tishio kwa "amani na usalama" wa Marekani.
Makubaliano hayo yalitolewa kama 'amri ya utendaji' ya rais, ikimaanisha kuwa yanaweza kurekebishwa au kufutwa ikiwa rais wa Marekani atabadilika.
Makubaliano hayo na Qatar si makubaliano ya kiusalama yanayotekelezeka kisheria, na hayahitaji idhini ya Bunge la Marekani.
Changamoto kubwa inayoikabili Saudi Arabia hivi sasa ni hii: Je, itakubali makubaliano ambayo yanafungamana na mabadiliko katika utawala wa Marekani, kama Qatar, ili kuhakikisha usalama wake?
Au itashinikiza kuwe na makubaliano madhubuti ya usalama wa kisheria na Marekani, ili dhamana yake ya usalama isiathirike hata rais akibadilika Marekani?















