Jasusi wa zamani wa Saudia amtaka Trump kuharibu kinu cha nyuklia cha Israel kama alivyofanya na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyekuwa mkuu wa ujasusi nchini Saudia Turki al-Faisal alizua hisia kwenye mitandao ya kijamii kwa makala iliyowashutumu viongozi wa nchi za Magharibi kwa "viwango viwili" katika misimamo yao dhidi ya Iran, Israel na tishio la silaha za nyuklia.
Katika makala yake kwenye tovuti ya The National news, Al-Faisal anasema: "Ikiwa tungeishi katika ulimwengu ambamo haki inaenea, tungeona ndege za kivita za Marekani aina ya B-2 zikinyesha mvua ya mawe ya mabomu kwenye kinu cha Dimona na maeneo mengine ya nyuklia ya Israel."
Anaongeza, "Israel inamiliki mabomu ya nyuklia, na hivyo kukiuka Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia. Haijawahi kutia saini mkataba huo ili kuepuka uangalizi wa IAEA. Hakuna anayekagua vituo vyake vya nyuklia."
Anasema wale wanaohalalisha "shambulio la upande mmoja la Israel" dhidi ya Iran kwa kutaja wito wa viongozi wa Iran "kuiangamiza Israel" wanapuuza kauli za Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, tangu alipoingia madarakani mwaka 1996, na wito wake wa mara kwa mara wa "kuiangamiza serikali ya Iran."
Al-Faisal anasema kwamba "unafiki wa nchi za Magharibi na uungaji mkono wao kwa Israel katika shambulio lake dhidi ya Iran ulitarajiwa. Pia 'wanailinda Israel katika mashambulizi yake yanayoendelea Palestina,'" hata kama baadhi yao wameondoa uungaji mkono huo.
Katika makala yake, mkuu huyo wa zamani wa kijasusi wa Saudia anatoa wito wa kulinganishwa kwa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi kwa Russia kutokana na uvamizi wake katika ardhi ya Ukraine na jibu lao kwa hatua za Israel. Anaona hili kama "mkanganyiko wa wazi wa kanuni na sheria zinazohubiriwa na Magharibi

Chanzo cha picha, Getty Images
Al-Faisal alikosoa mashambulizi ya anga ya Marekani kwenye maeneo matatu ya nyuklia ya Iran na kumshutumu Rais wa Marekani Donald Trump kwa "kuburutwa ili kupamba" mashambulizi haramu ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu dhidi ya Tehran.
Rais Trump alijionyesha wakati wa kampeni yake kama "mleta amani" ulimwenguni. Sehemu kubwa ya Wamarekani, ambao hawajaridhika na vita vinavyoendelea nchini mwao, walimchagua kwa msingi huu. Katika hotuba yake ya kuapishwa, aliahidi "kumaliza vita vyote na kueneza roho ya umoja kati ya mataifa na watu."
Lakini vita hiyo ambayo aliahidi kumalizika ndani ya saa 24 bado haijaisha. Vita vinaendelea kupamba moto huko Gaza pia. Kwa hakika, Marekani imejiingiza katika makabiliano mapya ambayo yameanza kati ya Israel na Iran. Ajabu, Washington ndiyo inayopatanisha makubaliano ya kusitisha mapigano na Tehran.
Mkuu huyo wa zamani wa kijasusi wa Saudia alibainisha kuwa Trump "alipinga kwa ujasiri" viongozi wa nchi yake katika uvamizi wao nchini Iraq zaidi ya miongo miwili iliyopita. Leo, lazima "ajue kwamba vita vya Iraq na Afghanistan vilikuwa na matokeo, na kwamba vita vya Iran vina madhara pia."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alisema haelewi undumilakuwili wa Trump anapoahidi kuleta amani Mashariki ya Kati na kisha kuipigania Iran. Pia alisema anaipongeza Tehran kwa kuitikia wito wa kusitisha mapigano huku akimsifu Netanyahu.
Kujibu msimamo huu, Turki al-Faisal alitangaza kwamba hatazuru Marekani hadi Donald Trump atakapoondoka Ikulu ya White House.
Alisema atafanya hivyo kwa kufuata nyayo ya baba yake, Mfalme Faisal, ambaye alikataa kuzuru Marekani wakati wa uongozi wa Harry Truman, akimshutumu kwa kuvunja ahadi ya mtangulizi wake, Rais Franklin Roosevelt, aliposaidia kuanzisha Israel.
Ahadi ya Rais wa Marekani Franklin Roosevelt kwa Mfalme Abdulaziz bin Saud ilianzia kwenye mkataba wa makubaliano uliotiwa saini kati yao wakati wa mkutano wa Februari 14, 1945, ndani ya USS Quincy.
Mfalme Abdulaziz alizungumza na Rais Roosevelt suala la "Waarabu wa Palestina na haki zao halali kwa ardhi yao." Alitoa angalizo la rais wa Marekani kuhusu "tishio la kuwepo kwa Waarabu na mgogoro uliosababishwa na kuendelea kuhama kwa Wayahudi na ununuzi wao wa ardhi."
Mfalme alisema katika mada yake kwamba "matumaini ya Waarabu yameegemezwa juu ya ahadi ya heshima waliyopewa na Washirika, na juu ya kupenda haki inayojulikana na Marekani, na kwamba Waarabu wanatarajia Marekani kuwaunga mkono."
Rais wa Marekani alijibu kwa kusema kwamba alitaka kumhakikishia mfalme kwamba "hatafanya chochote kuwaunga mkono Wayahudi dhidi ya Waarabu. Na kwamba hatafanya chochote cha uadui kwa Waarabu."
Lakini chini ya mrithi wake, Rais Harry Truman, Marekani ilibadili msimamo wake kuhusu mgogoro wa Palestina. Tarehe 26 Oktoba 1947, Mfalme Abdulaziz bin Saud alituma barua kwa rais mpya wa Marekani, akieleza wasiwasi wa Riyadh kuhusu kuhama kwa Washington.
"Uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuunga mkono matakwa ya Wazayuni huko Palestina ni kitendo cha chuki dhidi ya Waarabu. Wakati huo huo, ni kinyume na ahadi tuliyopewa na hayati Rais Roosevelt. Uamuzi huo pia hauendani na maslahi ya Marekani katika nchi za Kiarabu."
Mahusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia yalizidi kuwa magumu wakati wa uongozi wa Rais Truman kutokana na msimamo wa Marekani kuhusu suala la Palestina.
Inaaminika kuwa Mfalme Faisal, ambaye alikuwa mwanamfalme wakati huo, aliamua kutotembelea Amerika hadi Truman alipoondoka Ikulu ya White House.
Hivi ndivyo mwanawe Turki Al-Faisal alivyoonyesha katika makala yake: "Nitafuata mfano wa baba yangu, Mfalme Faisal, wakati Rais Harry Truman alipovunja ahadi ya mtangulizi wake, Franklin Roosevelt."
Idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ilitangamana na makala ya Turki Al-Faisal. Maoni yalitofautiana kati ya wale waliounga mkono pendekezo hilo, ambalo wengi walilitaja kuwa "jasiri na lenye busara," na wale ambao walisita kulisifu.
Amash Al-Harbi aliandika kwenye Twitter: "Makala ya Mwanamfalme Turki Al-Faisal kuhusu kiituo cha nyuklia cha Dimona cha Kizayuni inaniwakilisha mimi na kila mtu huru anayetaka haki na uhuru.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Abdullah bin Mufrih Al Shaya alisema, "Trump angeweza kweli kufanya amani ikiwa angenyima silaha za nyuklia kwa Iran na Israel, na kusimamisha vita vya Gaza na mauaji yanayoendelea ya watu wasio na hatia. Haki haigawanyiki, na amani haiwezi kujengwa kwa viwango viwili.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Maha alipinga kile alichokiona kama utetezi wa Iran katika makala ya Turki al-Faisal: "Anachosema ni kweli, lakini Iran ni adui mkubwa wa eneo."
Kwa mtazamo tofauti Barq al-Khalidi, katika kile kilichoonekana kuwa ni ulinzi wa Israel na umiliki wake wa silaha za nyuklia amesema: "Kuna tofauti kati ya serikali ya kidemokrasia, iliyoanzishwa kitaasisi inayomiliki silaha za maangamizi makubwa, na kundi la madhehebu lenye chuki na wagonjwa ambalo kaulimbiu zake ni kifo na uharibifu."
Uhusiano wa Saudia na Iran hivi karibuni umeanza kuimarika baada ya mataifa hayo mawili kutofautiana kwa muda mrefu kutokana na mgogoro wa Yemen. Tehran inawaunga mkono Wahouthi, huku Riyadh ikiunga mkono serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












