Je, ushindani wa silaha wa Saudia dhidi ya Iran unaingia katika awamu mpya?

Chanzo cha picha, Reuters
Marekani na Saudi Arabia zimetia saini mkataba wa kihistoria wa ushirikiano wa kiuchumi na kijeshi wenye thamani ya mamia ya mabilioni ya dola.
Kulingana na Ikulu ya Marekani, kifurushi hicho kina thamani ya zaidi ya dola bilioni 600 na kinajumuisha "mkataba mkubwa zaidi wa silaha katika historia."
Makubaliano hayo yaliyotangazwa wakati wa ziara ya Rais wa Marekani Donald Trump mjini Riyadh, yanajumuisha ahadi katika maeneo ya kimkakati kama vile ulinzi, nishati, miundombinu Ujasusi na akili mnemba yakiwa makubaliano ambayo ni zaidi ya mabadilishano ya kibiashara.
Mkataba wa karibu dola bilioni 142 wa kuupa ufalme wa Saudia teknolojia ya hali ya juu ya kijeshi umeambatana na uwekezaji wa mabilioni ya dola za Saudia katika vituo vya data, anga, huduma za afya na uchimbaji madini kwenye ardhi ya Marekani.

Chanzo cha picha, Reuters
Tangazo hilo lilitolewa mwanzoni mwa safari ya siku nne ya Trump huko Mashariki ya Kati, iliyoanzia Saudi Arabia na kuendelea nchini Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Pia, maadhimisho ya miaka 80 ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili yalimalizika huku eneo hilo likikumbwa na vita huko Gaza, mvutano na Iran, na mashambulizi ya vikosi vya Houthi nchini Yemen.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Marekani, kifurushi kilichotangazwa na Marekani na Saudi Arabia kinajumuisha ahadi nyingi za kiuchumi, kibiashara na kijeshi zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 600.
Sehemu kubwa zaidi ya makubaliano hayo ni mauzo ya silaha za Marekani yenye thamani ya karibu dola bilioni 142, ambayo Washington imeeleza kuwa "mkataba mkubwa zaidi wa ulinzi katika historia."Mkataba huo unahusisha maeneo makuu matano:
- Kuimarisha uwezo wa anga ya Saudi Arabia
- Mifumo ya ulinzi wa makombora
- Usalama wa baharini na pwani
- Uboreshaji wa Vikosi vya Ardhini na Walinzi wa Mipaka
- Kuboresha mifumo ya habari na mawasiliano

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mfuko huo pia unajumuisha programu za mafunzo na usaidizi wa kiufundi ili kuongeza uwezo wa uendeshaji wa jeshi la Saudi, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya vyuo vya matibabu vya kijeshi na huduma za afya.
"Sitasita kamwe kutumia mamlaka ya Marekani kutetea Marekani au kusaidia kutetea washirika wetu," Trump alisema katika hotuba yake kufuatia tangazo hilo.
Mchambuzi wa sera za kigeni Daniel DePetris aliiambia BBC Mundo kwamba makubaliano hayo ya mabilioni ya dola yataimarisha nafasi ya Saudi Arabia kama nguvu ya kijeshi ya kikanda, ingawa alisisitiza kuwa "vikosi vya kijeshi vya Saudi tayari vina uwezo wa kupata vifaa vya hali ya juu zaidi katika ghala la silaha la Marekani. Hiyo ndiyo imekuwa hali yao."
Mpango huo mkubwa ulitangazwa kwa hotuba za furaha, za kejeli na kuonyesha ukaribu wa kibinafsi kati ya Trump na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman.
Rais wa Marekani alikaribishwa kwa sherehe rasmi na alijumuika na viongozi wa biashara kama vile Elon Musk na watendaji kutoka BlackRock na Blackstone. Hotuba yake iliisha kwa kupeana mkono jukwaani na wimbo wa YMCA ukicheza.
Sherehe hiyo ilitofautiana na mapokezi ya baridi aliyopewa Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden na Saudi Arabia mwaka wa 2022. Alikuwa amesafiri hadi nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kuomba msaada wa kupunguza bei ya petroli na alikuwa amepeana tu mkono na mwana mfalme wa Saudia.
Safari hiyo ilikuja miaka miwili baada ya Joe Biden kuitaja Saudi Arabia "nchi yenye chuki" kufuatia mauaji ya 2018 ya mwanahabari mkosoaji Jamal Khashoggi.
Sasa inaonekana kwamba masuala haya yote yamekuwa historia

Chanzo cha picha, Reuters
Trump aliashiria "kasi nzuri" katika uhusiano wa nchi hizo mbili, akisema, "Tumepata maendeleo yasiyokuwa ya kawaida na ya kushangaza pamoja."
Alichokiita mwanzo wa "zama angavu kwa Mashariki ya Kati."
"Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka elfu moja, ulimwengu utatazama eneo hili sio kama mahali pa vita na kifo, lakini kama nchi ya matumaini na fursa," aliongeza.
Donald Trump aliendelea: "Tutafanya kazi pamoja, tutafanikiwa pamoja, tutashinda pamoja, na tutakuwa marafiki daima."
Mohammed bin Salman, kwa upande wake, alielezea makubaliano hayo kuwa yanaakisi "uhusiano wa kina wa kiuchumi" kati ya nchi hizo mbili.
Alihakikisha kwamba mapatano hayo yatapanuka katika miezi ijayo na kufikia thamani ya takriban dola trilioni moja, akisisitiza kwamba ushirikiano haukomei katika nyanja ya kiuchumi, bali pia unajumuisha usalama wa kikanda, utulivu na amani.
Zaidi ya sekta ya ulinzi, kifurushi hiki cha kina pia kinajumuisha sekta za kiuchumi na kiteknolojia.
Maeneo haya yanajumuisha uwekezaji wa Saudi Data Vault wa $20 bilioni katika vituo vya data na miundombinu ya nishati nchini Marekani.
Pia, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, ushirikiano wa pamoja umeanzishwa kati ya makampuni ya teknolojia kama vile Google, Oracle, Salesforce, AMD, na Uber ili kuwekeza dola bilioni 80 katika teknolojia za "mabadiliko" katika nchi zote mbili.
Usafirishaji wa mabomba ya gesi na mitambo yenye thamani ya dola bilioni 14.2 pia umetiwa saini, pamoja na uuzaji wa ndege za Boeing 737-8 kwa Saudi Avi Lease zenye thamani ya dola bilioni 4.8.

Chanzo cha picha, Reuters
Katika sekta ya huduma ya afya, Shamakh IV Solutions ilitangaza kwamba itawekeza dola bilioni 5.8 kujenga kiwanda chenye uwezo wa juu wa kutengeneza sindano huko Michigan.
Mfuko huo pia unajumuisha uundaji wa fedha katika sekta mbalimbali ili kuelekeza uwekezaji wa Saudia katika viwanda vya Marekani: moja kwa ajili ya nishati (dola bilioni 5), nyingine kwa ajili ya teknolojia ya anga na ulinzi (dola bilioni 5), na ya tatu kwa ajili ya michezo ya kimataifa ($ 4 bilioni).
Hati za maelewano pia zimetiwa saini kwa ajili ya ushirikiano katika nyanja za madini na rasilimali za madini, pamoja na nishati na anga.
Katika muongo mmoja uliopita, Saudi Arabia imewekeza mabilioni ya dola katika ununuzi wa silaha za hali ya juu ili kuimarisha nafasi yake kama nguvu ya kijeshi ya kikanda.
Mpango huo mkubwa uliotangazwa wiki hii na Marekani, na hasa mkataba wa mauzo ya silaha wa dola bilioni 142, wataalam wanasema, unaimarisha njia hii na kuimarisha uhusiano wa kimkakati unaozingatia ushirikiano wa ulinzi.
"Saudi Arabia imepiga hatua katika miaka ya hivi karibuni katika kukuza uwezo wake wa kijeshi, hasa katika maeneo ya ulinzi wa anga na angani," Grant Rumley, afisa wa zamani wa Pentagon na mwenzake mkuu katika Taasisi ya Washington, aliiambia BBC Mundo.
Ramli anahusisha sehemu ya maendeleo haya kutokana na uzoefu wa vita vya Riyadh katika mapambano dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, ambapo mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo imejaribiwa mfululizo.
Amebainisha kuwa makubaliano hayo mapya na Washington "yanalenga kuimarisha maendeleo haya, kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiulinzi kati ya nchi hizo mbili, na kutuma ujumbe wa vikwazo kwa wapinzani wa kikanda wa Saudi Arabia, hususan Iran."
Ushindani kati ya Riyadh na Tehran umetawala mazingira ya kijiografia ya Mashariki ya Kati kwa miaka mingi na umeingia kwenye migogoro mingi ya kikanda.
"Wakati Saudi Arabia imejikita katika ununuzi wa teknolojia ya hali ya juu ya kijeshi ya Magharibi, hasa kutoka Marekani, Iran imelazimika kuendeleza uwezo wake wa ndani kutokana na vikwazo ambavyo vimeifanya isiweze kupata silaha hizo," anabainisha mchambuzi Daniel DePetris.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Badala ya kushindana moja kwa moja katika ngazi ya kawaida, Iran imewekeza katika makombora ya bei nafuu lakini yenye ufanisi wa kiasili, ndege zisizo na rubani na mifumo," anafafanua.
"Saudi Arabia, kwa upande mwingine, haina sekta kubwa ya ulinzi wa ndani, lakini ina pesa za kutumia mabilioni ya dola kila mwaka kwa silaha za Magharibi," anasema DePetris.
Anasisitiza, hata hivyo, kwamba nguvu za kijeshi hazipimwi kutokana na ubora wa silaha pekee.
"Tatizo la Riyadh si ukosefu wa vifaa, lakini jinsi ambavyo vimetumika katika operesheni zilizopita," mchambuzi wa sera za kigeni Daniel DePetris aliambia BBC Mundo. "Ikiwa mkakati wao ni mbovu au wenye malengo makubwa, hata ndege bora za kivita au makombora hayawezi kufidia mapungufu haya."
Anamalizia kwa kusisitiza kwamba, makubaliano hayo mapya na Marekani sio tu kwamba yanajumuisha kuipatia Saudi Arabia vifaa vingi vya hali ya juu vya ulinzi, bali pia yanajumuisha kutoa uwezo wa kiutendaji na wa kimkakati unaoiwezesha Riyadh kutumia rasilimali hizo kwa ufanisi zaidi.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












