Super League: Je, mashindano mapya yanaweza kuboresha michezo ya klabu barani Afrika?

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ligi ya Mabingwa Afrika, iliyoshinda timu ya Wydad Casablanca msimu uliopita, klabu hiyo inaweza kutengwa na Ligi mpya ya Afrika.

Huenda Morocco imevunja vizuizi vya soka la Afrika kutokana na historia ya nchi hiyo kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia, lakini mchezo wa klabu barani Africa bado uko nyuma ya viwango vya Ulaya.

Kwa hivyo, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Patrice Motsepe anatumai kuzinduliwa kwa Ligi Kuu ya Afrika mwaka ujao kutabadilisha hilo.

Raia huyo wa Afrika Kusini alitaja mashindano hayo mapya kama "moja ya matukio ya kusisimua zaidi katika historia ya soka ya Afrika" alipozindua mipango ya hivi punde nchini Tanzania mwezi Agosti.

Akizungukwa rais wa shirikisho la soka duniani, rais wa Fifa Gianni Infantino, Motsepe alisisitiza kuwa yote ni kuhusu kuingiza pesa zaidi katika soka la vilabu barani Afrika, huku $100m zikiwepo kama pesa za zawadi na washindi wakipata $11.5m.

Mashindano hayo yalikuwa yamepangwa kuanza Agosti 2023, huku kukiwa na mipango ya kushirikisha vilabu 24 kutoka nchi 16, ingawa ripoti za hivi punde zinaonyesha kuwa huenda yakawa na timu nane pekee .

Hata hivyo nyingi ziko katika muundo ambao huenda ukafuata Ligi ya Mabingwa Ulaya, mpango ni kufikia kilele kwa fainali ya 'Super Bowl-kama' Mei 2024.

Nia ni kuwa Ligi Kuu ya Afrika itaendeshwa sambamba na Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopo, ambayo inashirikisha timu 16 katika hatua ya makundi lakini imekuwa ikitawaliwa na timu za Afrika Kaskazini katika muongo mmoja uliopita.

Caf inaahidi uwekezaji mkubwa wa dola milioni 200 kwa jumla - sio tu kwa vilabu vinavyoshiriki, lakini pia kwa maendeleo ya mchezo wa wanawake na shule za mafunzo ya vijana katika nchi zake 54 wanachama.

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Caf, Patrice Motsepe (kushoto) alizindua Ligi ya Mabingwa mwezi Agosti pamoja na rais wa Fifa Gianni Infantino.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uchaguzi wa vilabu usio wazi

"Hatujashauriwa hata mara moja," anasema John Comitis, mwenyekiti na mmiliki wa Cape Town City FC, ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Soka ya Afrika Kusini (PSL).

Mshambulizi huyo wa zamani amekuwa akijihusisha na soka la Afrika kwa takriban miaka 40 na hajafurahishwa na kile anachokiita "mchakato wa kuchagua usio wazi" wa vilabu kwa ajili ya League mpya.

Comitis anasema alipokea orodha kadhaa za vilabu ambavyo vingejumuishwa, na anaamini kwamba vilivyochaguliwa ni "vilabu vilivyowekwa kisiasa, vinavyomilikiwa na watu fulani matajiri au serikali".

Umiliki wa vilabu vya soka na serikali bado ni jambo la kawaida kote barani Afrika, ingawa sivyo ilivyo nchini Afrika Kusini kwenyewe.

Wasiwasi mkubwa wa Comitis ni athari ambayo shindano jipya la bara linaweza kuwa nayo kwa PSL, ambayo anaielezea kuwa "yenye ufanisi na weledi" katika masuala ya ufadhili na haki za utangazaji.

"Hali mbaya ya miundombinu barani Afrika ni mbaya," anasema, akiangazia jinsi timu yake ilivyosafiri hadi DR Congo kwa mchezo na haikuweza kufika huko na kurudi kwa chini ya siku tano na kuelezea gharama za safari kama "kubwa sana."

Katika muktadha huu, Comitis anaamini kuwa itakuwa vigumu sana kusawazisha michezo ya Super League katika ratiba iliyopo na kwamba bila shaka ligi za kitaifa zitakumbwa na matatizo, na uwezekano wa kupoteza pesa za matangazo ikiwa vilabu vikuu vitapanga timu zingine katika michezo ya nyumbani.

"Mwisho wa siku, tunalinda biashara zetu na soka la Afrika Kusini," anasema.

Wengine wanaweza kuziita zabibu chungu, kwani Comitis amedokeza wazi kwamba timu yake haikuwa miongoni mwa 24 zilizochaguliwa kwenye League hiyo.

Bado haijulikani ni wapi zawadi ya $200m itatoka, hasa baada ya Caf kuripoti hasara ya zaidi ya $40m katika hesabu zake zilizokaguliwa hivi majuzi., hata kama Motsepe anaendelea kuzungumzia maslahi makubwa kutoka kwa sekta ya biashara.

Msemaji wa Caf alisema Motsepe, aliyechaguliwa kama raisi wa Caf Machi 2021, "ana masilahi bora ya kandanda ya Afrika moyoni mwake".

Wakati huo huo, hakuna shaka kwamba bilionea wa madini Motsepe amewekeza pesa nyingi katika mchezo huo akiwa mmiliki wa mabingwa watetezi wa Afrika Kusini Mamelodi Sundowns.

q

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mamelodi Sundowns, inayomilikiwa na Motsepe, ilikuwa klabu ya mwisho kutoka nje ya Afrika Kaskazini kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoifunga Zamalek ya Misri mwaka wa 2016.

Kufanya mchezo wa Kiafrika uwe wa ushindani zaidi

Iwapo yatatokea, hela zitakazohusika zitafanya Ligi huyo (Super League) kuwa ya thamani zaidi kuliko Kombe la Mataifa ya Afrika, ambalo mara zote limekuwa likivutia kimataifa na kufikia hatua ya fainali iliyowakutanisha wachezaji-wenza wa Liverpool wakati huo na nyota wa kimataifa Sadio Mane na Mohamed Salah dhidi ya kila mmoja wakati Senegal ilishinda Misri mnamo Februari.

Osasu Obayiuwana, mwandishi wa habari wa kandanda nchini Nigeria, anaamini dhana ya mashindano mapya ya vilabu haikuundwa barani Afrika, lakini kwa hakika, ilikuwa ni chimbuko la Infantino.

"Kuna imani nje ya Afrika kwamba Waafrika wanahitaji kuongozwa kama watoto wachanga. Naona hili aibu kubwa," Obayiuwana alisema.

Kama vile Comitis, Obayiuwana ana wasiwasi kwamba kalenda ya soka itakuwa na msongamano mkubwa sana.

Iwapo timu 24 zitashiriki, Ligi Kuu ya Afrika itakuwa na siku 24 za mechi kwa msimu mmoja - nyingi za kutosheleza pamoja na kampeni za nyumbani zilizoenea karibu wiki 38 na ahadi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ongeza kwa hilo utaratibu wa usafiri katika bara zima, ambayo inatoa changamoto yenyewe, na ukubwa wa kazi ni wazi.

"Unaweza kufikiria kiasi cha shinikizo ambacho kitakuwa kwa wachezaji," Obayiuwana aliongeza.

Msaada nyumbani

Caf inasema maelezo ya Ligi Kuu ya Afrika bado yanatatuliwa lakini, huku kukiwa na ukosoaji mwingi na maswali yasiyo na majibu, shindano hilo jipya lina wafuasi wake wenye majina makubwa.

Mfungaji bora wa Afrika Kusini Benni McCarthy alicheza barani Afrika na Ulaya, akishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Porto ya Jose Mourinho mwaka wa 2004, na sasa ni kocha wa kikosi cha kwanza Manchester United baada ya kufunza nchini mwake huko Cape Town City na AmaZulu.

Anadhani Ligi mpya ya Super League itatoa uwezo zaidi wa mapato kwa vilabu na jukwaa bora kwa wachezaji ambalo linaweza kuleta mabadiliko.

"Ningependa kuona mchezaji wa Kiafrika akishindana dhidi ya wachezaji bora zaidi duniani kwa sababu ni muda mrefu sana tangu tupate Mwafrika kushinda Ballon d'Or," mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 45 alisema, akirejea ushindi wa Mliberia George Weah mwaka 1995. .

“Soka la Afrika lina kipaji lakini haliko katika kiwango sawa na soka la Ulaya, kasi na upande wa kiufundi ni tofauti na wachezaji walivyozoea Afrika.

"Nadhani Super League hii itaondoa kizuizi hicho kwa kufanya soka la Afrika kuwa la ushindani zaidi."

q

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa Wydad Casablanca walijaa kwenye Uwanja wa Stade Mohammed V kwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly mwezi Mei, lakini mashindano hayo yanatatizika kuonyeshwa kwenye TV kote Afrika.

Hayo ndiyo matumaini, lakini, kiuhalisia, ikiwa Ligi mpya ya Afrika Super League itapata nafasi ya kupambana na kufanikiwa itahitajika kuvutia pesa za TV, ambazo ni tegemeo la soka barani Ulaya na zilizochangia kuifanya Ligi Kuu ya Uingereza kuwa yenye mafanikio makubwa kifedha duniani.

Lakini, kama Obayiuwana anavyoonyesha, wapeperusha matangazo wa Kiafrika wanatumia pesa nyingi katika mchezo wa Ulaya kuliko kandanda ya Afrika - huku hoja yao ikiwa ni kwamba bidhaa hiyo haistahili kuwekeza.

Kwa hiyo, unatatuaje hali hii? Bila fedha za TV na udhamini, itakuwa vigumu kukuza ubora wa soka.

Obayiuwana anaamini Caf inapaswa kujenga ligi za ndani kwanza, kuzikuza barani na kuzifanya kuwa maarufu.

Kisha, kama ilivyo kwa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, mashabiki "watapata kujua wachezaji na vilabu na watawekeza kwao, jambo ambalo sivyo ilivyo barani Afrika".

Huanza na watu kuweza kutazama mechi katika bara zima, jambo ambalo katika nchi nyingi ni tatizo.

"Ni rahisi kwangu kutazama Ligi ya Ulaya huko Lagos kuliko kutazama mechi kati ya Esperance na Raja Casablanca katika Ligi ya Mabingwa Afrika," Mnigeria huyo alisema.

Licha ya maendeleo ya timu za Afrika kwenye Kombe la Dunia, kuboresha mchezo wa vilabu kunaweza kuwa changamoto kubwa kwa Motsepe.