Je, Biden anaweza kubadilishwa kama mgombea? Si kwa urahisi hivyo

Rais Joe Biden

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Christal Hayes, Holly Honderich & Rachel Looker
    • Nafasi, BBC News

Joe Biden amekuwa akikabiliwa na kibarua kigumu baada ya utendakazi wake duni katika mdahalo wa kwanza wa urais 2024 dhidi ya Donald Trump.

Huku uchaguzi wa Novemba ukikaribia, idadi ya wafuasi wa chama cha Democratic wanaomnamtaka rais ajiondoe kwenye kinyang'anyiro hicho kutokana na wasiwasi kuhusu afya yake inaongezeka.

Makumi ya Wademocrats wametoa wito hadharani kumtaka Bw. Biden kutogombea urais na kumpisha mtu mwinye umri mdogo kwenye chama chake.

Bw. Biden ameapa kugombea muhula wa pili, amesisitiza hilo katika mikutano ya hadhara na mahojiano katika vituo vya habari vya ABC News na MSNBC.

Endapo hataitikia wito wa baadhi ya wafuati wake mambo huenda yakawa mabaya.

Tunaangazia nadharia ambazo zinaweza kujitokeza.

Je, Joe Biden anaweza kujiondoa?

Ndio, ikilazimu kufanya hivyo - lakini ikiwa- Bw Biden ataamua kujiuzulu kama mgombea urais wa Chama cha Democratic, itakuwa rahisi kupata mgombea mwingine.

Atakayepeperusha bendera ya chama atachaguliwa rasmi katika Kongamano la Kitaifa la wajumbe wa chama cha Democratic (DNC) mjini Chicago kati ya tarehe 19-22 Agosti.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wademocrats wanaripotiwa kupanga kumteua Bw Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris kabla ya mkutano huo.

Katika kongamano hilo, mgombea lazima apate uungwaji mkono kutoka kwa wengi wa "wajumbe" - maafisa wa chama wanaomchagua rasmi mteule. Wajumbe hutumwa kwa wagombea sawia kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa kila jimbo.

Mwaka huu, Bw Biden alipata uungwaji mkono wa karibu 99% ya wajumbe 4,000.

Kulingana na sheria za DNC, wajumbe hao "wameahidi" kumuunga mkono rais aliye madarakani.

Biden akiamua kujiondoa kwa hiari, ulingo utakuwa wazi kwa yeyote aliye na azma ya kuiwakilisha kuwasilisha ombi la uteuzi.

Democrats watasalia na kongamano la wazi ambapo watapendekeza watu wanaotarajiwa kuteuliwa na kuendelea kupiga kura hadi mgombea atakayepata kura nyingi za wajumbe atakapopewa idhini ya kukiwakilisha chama katika uchaguzu wa urais.

Hilo linaweza kuibua mchuano mkali kati ya Wademocrats wanaowania uteuzi.

Bw Biden hadi sasa hajatoa dalili yoyote kwamba atafikiria kujiuzulu.

Lakini ikiwa ataamua kufanya hivyo, "hilo litafungua chupa tofauti kabisa ya minyoo", mwanahistoria wa kisiasa Leah Wright Rigueur aliambia BBC News.

"Nadhani kama angebadilishwa, sehemu ya mazungumzo ya kuachia ngazi itakuwa kwamba atapata uamuzi wa mwisho wa nani atakayechukua nafasi yake," alisema.

What next graphic

Je, anaweza kulazimishwa kujiondoa?

Akikataa wito wa kujiondoa kwa hiari, hapo ndipo mchakato unakuwa mgumu sana.

Katika enzi ya siasa za kisasa, chama kikuu cha kitaifa hakijawahi kuchukua uamuzi wa wa kumshurutisha mgombea kujiondoa.

Lakini, kanuni za DNC zina mianya ambayo inaweza, kwa nadharia, kumuondoa Bw. Biden kwa nguvu.

Sheria hizo zinawaruhusu wajumbe "kwa nia njema kuakisi hisia za wale waliowachagua", kumaanisha kwamba wanaweza kumteua mtu mwingine.

"Inaweza kuwa hali mbaya sana," Bi Wright Rigueur alisema.

Wataalamu waliambia BBC kwamba wanatilia shaka uwezekano wa ugovui kuibuka kati ya wajumbe wa chama.

Lakini DNC inaweza kubadilisha sheria za chama wakati wowote.

Bi Wright Rigueur aliashiria 1968, wakati Rais Lyndon B Johnson alipoamua kutogombea tena urais.

Chama kilihama kutoka kwa mchakato wa kongamano la wazi, ambapo wajumbe wangeweza kupiga kura kwa yeyote waliyemchagua, hadi mchakato wa kawaida, ambapo mjumbe aliambatanishwa na mgombeaji kulingana na matokeo ya msingi.

Hata kama Bw Biden angejiondoa katika kinyang'anyiro hicho ghafla, makundi ya wahafidhina yameapa kuwasilisha kesi mahakamani kupinga uhalali wa mtu yeyote atakayechukua nafasi ya Democratic kustahiki kupigiwa kura.

BBC graphic

Maelezo zaidi kuhusu uchaguzi:

BBC graphic

Kamala Harris atachukua nafasi ya Biden?

Makamu wa Rais Kamala Harris angechukuwa nafasi ya Bw Biden moja kwa moja endapo angejiuzulu kama mgombea wa urais kwa muhula wake wa pili.

Lakini sheria hizo hizo hazitatumika ikiwa Bw Biden atajiondoa kama mgombeaji wa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa Novemba, na hakuna utaratibu unaoweza kumpa makamu wa rais tiketi ya moja kwa moja katika kinyang'anyiro cha wazi.

Badala yake, Bi Harris angelazimika kushinda idadi kubwa ya wajumbe, kama mgombeaji mwingine yeyote.

Huenda Bw Biden atamuunga mkono kuchukua nafasi yake ikiwa atajitenga.

Kwa kuwa tayari yuko kwenye tikiti ya chama cha Democratic, Bi Harris angeweza kupata pesa zote za kampeni zinazotolewa rais kwa sasa. Na ana wasifu wa kitaifa.

Lakini umaarufu wake wa kitaifa miongoni mwa Wamarekani unaweza kumnyima faida hiyo.

Je, Marekebisho ya 25 yanaweza kutekelezwa?

Marekebisho ya 25 ya Katiba yanaruhusu makamu wa rais wa Marekani na wengi wa baraza la mawaziri kutangaza kuwa rais hawezi kutekeleza majukumu yake.

Hilo likizingatiwa, mamlaka huhamishiwa kwa makamu wa rais kuhudumu kama kaimu rais.

Hii haijawahi kutokea.

Lakini kufuatia mjadala huo, wabunge wakuu wa chama cha Republican walitoa wito kwa baraza la mawaziri la Bw Biden kutathmini uwezekano wa kutumia kifungu hiki.

Baada ya ghasia za Bunge la Marekani mnamo 2021, Bunge linalodhibitiwa na chama cha Democratic liliidhinisha azimio la kumtaka Makamu wa Rais wa wakati huo Mike Pence aitishe Marekebisho ya 25 ya kumuondoa Trump, lakini hatua hiyo haikuenda popote.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah