Nani anayeweza kuchukua nafasi ya Biden ndani ya chama cha Democratic?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ana Faguy
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Baada ya kukataa wito wa wiki kadhaa wa kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais wa 2024, Rais Joe Biden Jumapili alitangaza kuwa atamaliza kampeni yake ya kuchaguliwa tena, ambayo ilionekana kutokamilika baada ya matokeo yake ya kuotoridhisha katika mjadala dhidi ya mpinzani wa Republican Donald Trump.
Muda mfupi tu baada ya kushiriki uamuzi wake wa kujiuzulu, Bw Biden alitangaza mgombea ambaye aliamini anafaa kuchukua nafasi yake: Makamu wa Rais Kamala Harris.
"Nataka kutoa usaidizi wangu kamili na kumuunga mkono Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu," aliandika kwenye X, zamani Twitter. "Wanademokrasia - ni wakati wa kuungana na kumshinda Trump."
Uamuzi wa Bw Biden wa kujiuzulu ulikuja baada ya takriban wabunge 30 katika Baraza la Wawakilishi, maseneta watano wa Marekani na baadhi ya wafadhili wakuu - akiwemo mwigizaji George Clooney - kumsihi Bw Biden aache kinyang'anyiro hicho na "kupitisha mwenge" wa uongozi.
Kuongeza shinikizo zaidi, msururu wa kura za maoni tangu mjadala ulipopendekeza Trump alikuwa akisonga mbele katika majimbo muhimu.
Baada ya tangazo la kushangaza la Bw Biden Jumapili, umakini ulielekezwa kwenye mchakato wa kuchukua nafasi yake katika kinyang'anyiro cha 2024 dhidi ya Trump.
Je, nafasi ya Biden itajazwa vipi?
Bwana Biden angeweza kulazimishwa kujiondoa na chama chake, lakini badala yake, alichagua kufanya hivyo peke yake.
Mchakato wa kujaza nafasi yake unakuwa wazi zaidi kwa sababu hiyo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bw Biden alikuwa amepata uungwaji mkono wa takriban wajumbe wote wa chama cha Democratic ambao watapiga kura ya kumfanya kuwa mteule. Sasa, wajumbe wake wataachiliwa ili kumpigia kura mgombea mwingine. Yeyote anayeweza kushinda idadi kubwa ya wajumbe kwenye kongamano ndiye atakuwa mteule mpya.
Wanademokrasia walikuwa wamepanga kupiga kura ya kutaka kumchagua rasmi Biden kama mteule wa chama kabla ya kongamano lao, ambalo litaanza tarehe 19 Agosti. Hatima ya wito huu haijulikani sasa baada ya tangazo la Bw Biden.
Bwana Biden hapo awali alisema Bi Harris anafaa kuwa mteule wa chama, ingawa wagombea wengine kadhaa walikuwa wakijadiliwa.
Bado kuna nafasi mtu wa nje anaweza kupigania uteuzi huo - Spika wa zamani wa Bunge Nancy Pelosi ametaka chama kiwe na ushindani na sio tu kumtia mafuta Harris kama mteule wao.
Swali lingine linalokuja ni nani atakuwa makamu wa rais mteule, na ikiwa jukumu hilo litaenda kwa mmoja wa watu wanaozingatiwa kuchukua nafasi ya Bw Biden.
Hawa ndio watu wa kufuatilia.
Makamu wa Rais, Kamala Harris

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu wa Rais Kamala Harris, tayari yuko kwenye mbio za urais na Biden, ni chaguo la wazi kuchukua nafasi yake.
Akiwa makamu wa rais, amekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kulinda haki za uzazi baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha haki ya kuavya mimba.
Bi Harris amethibitisha kuwa mshirika mwaminifu kwa rais na alitetea vikali uzungumzaji wake katika mdahalo. Baada ya hafla hiyo, alikiri kuwa rais alikuwa na "mwanzo wa polepole" lakini aliendelea kutoa majibu muhimu zaidi kuliko Trump.
"Watu wanaweza kujadiliana kuhusu mtindo wa uzungumzaji, lakini nani atakuwa rais wa Marekani katika uchaguzi huu, lazima hilo litokane na mambo ya maana," Harris aliiambia CNN siku ya Alhamisi.
Harris ana sifa na jina kubwa linalotokana na kazi ya makamu wa rais, lakini amekuwa na viwango vya chini vya kukubalika katika kipindi chote cha uongozi wake.
Asilimia 49 ya Wamarekani hawamuungi mkono Bi Harris, huku 39% wakimuunga mkono, kulingana na kura zilizofuatiliwa na FiveThirtyEight.
Lakini Bi Harris atakuwa na wakati mzuri kujitangaza, atakapokabiliana na mgombea mweza wa Trump, katika mdahalo utakao endeshwa na CBS, wa makamu wa ma-rais kabla ya Kongamano la Kitaifa la Democratic mwezi Agosti.
Gavana wa Michigan, Gretchen Whitmer

Chanzo cha picha, Getty Images
Gretchen Whitmer, gavana wa mihula miwili huko Michigan, anazidi kuwa maarufu na wadadisi wengi wanaamini atagombea urais 2028.
Amemfanyia kampeni Biden hapo awali. Aliliambia gazeti la New York Times, anataka kumuona rais wa Kizazi cha X mwaka 2028, lakini hakusema kuwa atagombea.
Mwaka 2022, aliongoza kampeni iliyokipatia chama cha Democratic, udhibiti wa bunge la jimbo la Michigan.
Udhibiti huo wa kisiasa ulimruhusu kutunga sera kadhaa, ikiwa ni pamoja na kulinda haki ya uavyaji mimba kwa watu wa Michigan na kupitisha kanuni salama za umiliki wa bunduki.
Gavana wa California, Gavin Newsom

Chanzo cha picha, Getty Images
Gavana wa California, Gavin Newsom ni mmoja wa waungaji mkono maarufu wa Utawala wa Biden. Huonekana mara kwa mara kwenye runinga akimsifu Biden.
Lakini Newsom ana malengo yake ya kisiasa.
Mara nyingi ameorodheshwa kama mgombea wa 2028, lakini wachambuzi wengi wa siasa wanaamini, anaweza kuwa bora kuchukua nafasi ya Biden sasa.
Newsom ameinua hadhi yake ya kitaifa katika miaka ya hivi karibuni kwa kuwa mzungumzaji mkuu wa chama kwenye vyombo vya habari vya kihafidhina, na kupitia mjadala dhidi ya Gavana wa Florida Ron DeSantis mwaka jana.
Waziri wa Uchukuzi, Pete Buttigieg

Chanzo cha picha, Getty Images
Sio siri kuwa Waziri wa Uchukuzi, Pete Buttigieg ana matarajio ya kuwa rais. Aligombea urais 2020 na mara nyingi huelezwa kama mmoja wa washirika bora wa Utawala wa Biden.
Buttigieg amesimamia mizozo kadhaa ya umma akiwa Waziri wa Uchukuzi.
Alisaidia kusimamia juhudi za serikali baada ya ajali ya treni katika kijiji cha East Palestina katika jimbo la Ohio, kuporomoka kwa Daraja la Baltimore na mzozo wa ratiba wa Shirika la Ndege la Southwest 2022.
Gavana wa Pennsylvania, Josh Shapiro

Chanzo cha picha, Getty Images
Gavana huyo, ambaye hapo awali aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, amefanya kazi katika nyadhifa mbalimbali za chama wakati wa uongozi wake.
Aligonga vichwa vya habari mwaka jana baada ya kujenga upya daraja lililoporomoka kwenye barabara kuu ya Philadelphia - ushindi mkubwa wa kisiasa kwa gavana wa awamu ya kwanza.
Ukarabati huo wa haraka ulisifiwa na wengi kama njia bora ya mazungumzo ya kisiasa katika miundombinu kwa mgombeaji wa urais 2028.
Gavana wa Illinois, JB Pritzker

Chanzo cha picha, Getty Images
JB Pritzker, gavana wa Illinois, ameinua hadhi yake katika miaka ya hivi karibuni kwa kumshambulia Trump na kumtetea Biden.
Mfanyabiashara bilionea - mrithi wa hoteli za Hyatt - ni mwepesi wa kuchapisha ukosoaji kwa Trump kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya mdahalo alimuita Trump "mwongo" na kusema yeye ni "mtuhumiwa wa makosa 34 ambaye anajijali yeye pekee."
Kama Whitmer, Pritzker ana rekodi ya kuweka kanuni za kulinda masuala ya haki za uavyaji mimba na udhibiti wa bunduki.
Wagombea wengine ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Gavana wa Kentucky, Andy Beshear, gavana wa mihula miwili katika jimbo la kihafidhina, amepata uungwaji mkono kitaifa tangu kuchaguliwa tena mwaka jana.
Gavana wa Maryland, Wes Moore amejikuta kwenye macho ya wengi katika miezi ya hivi karibuni kufuatia kuporomoka kwa Daraja kubwa la Francis Scott huko Baltimore.
Maseneta Amy Klobuchar na Cory Booker hutajwa mara kwa mara, kwani waliwahi kuwania urais siku za nyuma na wana kubalika miongoni mwa wana-Democratic.
Seneta wa Georgia Raphael Warnock, alishinda kinyang'anyiro cha useneta uliokuwa na ushindani mkubwa, pia ametajwa kuchukua nafasi ya Biden.
Kura ya maoni ya Reuters IPSOS iliyotolewa Jumanne inaeleza kuwa mtu pekee anaeweza kumshinda Trump Novemba ni Michelle Obama. Ingawa mke wa rais wa zamani amesema mara kwa mara hana matarajio ya kugombea urais.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












