Kwa nini Israel ilichukua muda mrefu kukabiliana na mashambulizi ya Hamas?

xc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiganaji wa Hamas waliweza kuuzidi nguvu ulinzi wa Israel katika shambulio la kushtukiza

Vikosi vya Ulinzi vya Israeli vilikuwa wapi wakati wapiganaji wa Hamas wakizurara karibu na vijiji vya mpakani na Gaza, watu wanauliza.

"Jeshi lilishindwa kabisa kujibu mapigo kwa haraka," Muisraeli mmoja alisema, akionyesha jinsi baadhi ya jamii zilizoshambuliwa zilivyolazimika kutegemea vikosi vyao vya ulinzi wa kiraia wakati wakisubiri wanajeshi kufika.

Jibu kamili la kwa nini Jeshi la Israel lilichukua muda kujitokeza, litapatikana siku za usoni. Lakini inaonekana kana kwamba shambulio la ghafla, kubwa na la kasi - liliuzidi nguvu ulinzi ambao ulikuwa dhaifu na haukuwa umejitayarisha.

Ujasusi wa Israeli ulishindwa kutambua mipango ya ndani ya Hamas ya shambulio hilo. Kundi hilo linaonekana limefanya mpango wa muda mrefu wa udanganyifu ili kutoa hisia kuwa lilikuwa halina uwezo au halitaki kuanzisha shambulio.

sdxc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maelfu ya makombora kutoka Gaza yamepiga maeneo mbalimbali ya Israel, likiwemo jiji la Tel Aviv

Maelfu ya roketi zilirushwa ili kuwalinda wavamizi. Lakini pia kulikuwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye vituo vya ufuatiliaji ambavyo Israel huvitumia kwenye uzio wa mpaka kuangalia kinachoendelea. Vilipuzi vizito na magari kisha yakavunja uzio wa usalama katika maeneo 80.

Ndege za kutengeneza na pikipiki pia vilihusika. Kati ya watu 800 na 1,000 wenye silaha walifurika kutoka Gaza kushambulia maeneo ya Israel.

Mbinu hizi zinaonekana kufaulu kuuzidi nguvu ulinzi wa Israeli - angalau kwa muda. Ilikuwa ni siku tulivu ya Jumamosi asubuhi ambayo pia ilikuwa sikukuu ya kidini.

Baadhi ya wapiganaji wa Hamas waliwalenga raia wa kawaida na wengine wakilenga vituo vya kijeshi. Kumekuwa na mshtuko kwamba vituo hivi vya kijeshi havikuwa na ulinzi mkali na ikawa rahisi kuzidiwa, huku picha zikionesha vifaru vya Israeli vikiwa mikononi mwa Hamas.

Na maeneo yaliyovunjwa kwenye mpaka yalibaki wazi kwa muda wa kutosha kuruhusu mateka kupelekwa Gaza kabla ya vifaru hatimaye kutumika kuziba.

sdx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Israel sasa inapeleka vifaru na wanajeshi katika mpaka na Gaza

Ulinzi unaonekana kuwa dhaifu - vikosi vya ulinzi vya Israeli katika miezi ya hivi karibuni vimekuwa vikilenga zaidi Ukingo wa Magharibi badala ya Gaza. Na Hamas huenda walitegemea mgawanyiko katika jamii ya Israel juu ya sera za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ili kuvuruga zaidi usalama.

Uwezo wa kijeshi na kijasusi wa Israeli kwa muda mrefu unaelezwa kuwa bora zaidi Mashariki ya Kati na ulimwenguni. Lakini pia wanaweza kuwa walidharau uwezo wa wapinzani wao.

Mashambulizi hayo yamelinganishwa na yale ya 9/11 nchini Marekani, wakati hakuna mtu aliyetabiri kwamba ndege zinaweza kutumika kama silaha. Haikudhaniwa.

Kutodhaniwa huko kutakuwa sehemu ya maswali ya muda mrefu kwa Israel, wakati lengo litakuwa kutafuta nini cha kufanya badala ya kuangalia nyuma.