Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Magonjwa unayoweza kupata kwa kutumia simu yako chooni
- Author, Omkar Karambelkar
- Nafasi, Mwandishi BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Tunazibeba kila mahali, tunaenda nazo chumbani kulala nazo, chooni na kwa watu wengi huwa ndio kitu cha kwanza wanachoamka nacho asubuhi - zaidi ya asilimia 90% ya watu ulimwenguni wanamiliki au hutumia simu za mkononi (rununu) na wengi wetu hatuwezi kukaa bila simu.
Lakini kama unapendelea kutumia simu ukiwa chooni huku ukiendeleza haja zako, ni mtindo unaoibua wasiwasi.
Kwa watu wengi kufuatilia maudhui ya mitandaoni kupitia simu za mikononi kwa muda mrefu huwa hawamaizi madhara yake ya kiafya.
Hebu tuangazie maambukizi ambayo watu huyapata pindi wanapoenda msalani na kutumia simu zao.
Changamoto kuu ni ipi?
Wengi wetu haswa vijana hupendelea kutumia simu wakiwa chooni.
Watu ambao hutumia zaidi ya nusu saa wakiwa chooni hupata magonjwa mengi.
Watu kama hao hukaa mahali pamoja kwa muda mrefu kwa sababu wanakagua simu zao za rununu kila wakati.
Hii inaweka shinikizo la ziada kwenye misuli karibu na sehemu ya njia ya haja kubwa.
Misuli hii husaidia katika haja kubwa.
Kwenda haja kubwa kwa kujilazimisha huongeza hatari ya magonjwa kwa viungo vyote mwilini.
Hii ikiwemo ugonjwa wa bawasili, gesi tumboni, nasuri na pia dutu.
Pia ukikaa mahala pamoja kwa muda mrefu huvuruga usambazaji wa damu mwilini.
Kulazimisha kupata choo ukiwa umekaa sehemu moja husababisha kujaa gesi tumboni na pia kupata choo kigumu.
Kwa mfano, choo cha aina ya kukalia kinaongeza shinikizo kwenye njia ya haja kubwa na misuli yake, na kuikalia kwa muda mrefu kunaweza kuleta msongo wa mawazo.
Hili hutokea wakati unapochelewa kupata haja na una hamu yakutoa kilicho mwilini, watu hujipata wakijishinikiza zaidi na kuingia mashakani.
Pia unapokaa kwa muda mrefu chooni huku ukipekua simu yako husababisha shinikizo katika viungo vya mwili kama maumivu shingoni na pia ya mgongoni.
Hivyo basi, ni muhimu kukumbuka kuwa mtu anapaswa kumaliza haja yake kwa muda mfupi na kuepuka kutumia simu ya mkononi wakati anapofanya hivyo.
Pia unawezapata matatizo kama kufa ganzi katika mikono na nyayo, au inakuwa vigumu kutembea kwa muda mfupi kutokana na kuweka mikono katika sehemu moja.
Mtindo wa maisha wa kukaa kwa muda mrefu umeonekana kuwa na madhara makubwa katika miaka mitano ya hivi karibuni, hasa tangu janga la Corona.
Kuendelea kukaa muda mrefu, kufanya kazi ukiwa umekaa, kutokutoka nje, kukosa mazoezi au yoga, na kula vibanzi na vyakula vilivyosindikwa kumekuwa jambo la kawaida.
Isitoshe, kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu kunaweza kusababisha magonjwa ya moyo, kisukari, unene, maumivu ya mgongo na shingo, udhaifu wa misuli, na maumivu ya viungo.
Matatizo kama vile gesi kujaa tumboni, kuongezeka uzito wa mwili, na mfumo wa mwili wa kimetaboliki wa polepole pia yanaathiri afya ya akili.
Na sio hayo tu, mtindo wa maisha wa kukaa tu pia unaweza kusababisha matatizo kama wasiwasi, unyogovu, msongo wa mawazo, na matatizo ya kula.
Nini kinatokea unapokaa kila wakati?
Mtindo wa maisha wa kukaa kwa muda mrefu bila shughuli yoyote ya kimwili unaharibu ubora wa maisha na kuongeza hatari ya matatizo mengi ya kiafya.
Vile vile, kukaa kwa muda mrefu huzuia mwili kudhibiti viwango vya sukari ya damu na insulini, na kusababisha kisukari cha aina ya pili, wasiwasi, unyogovu, maumivu ya viungo na misuli, kuongezeka kwa shinikizo la damu na mafuta mwilini, na hatari kubwa ya kiharusi na magonjwa ya moyo.
Pia kukaa kwa muda mrefu pia huleta shinikizo kwa misuli ya mgongo na kusababisha matatizo ya uti wa mgongo.
Mtindo huu wa maisha unahusishwa na magonjwa kama maumivu ya mgongo na shingo, na uvimbe wa vena.
Jinsi ya kuacha tabia ya kutumia simu chooni?
Tulimuuliza Dkt. Narendra Nikam, Daktari Mkuu katika Hospitali ya Lilavati, Mumbai, kuhusu jinsi ya kukabiliana na tabia ya kutumia simu chooni.
Dkt. Nikam alisema, "Kukaa chooni kwa muda mrefu kunaleta udhaifu kwa misuli ya fupanyonga, yaani misuli kutoka kitovu hadi makalioni, na kusababisha matatizo katika kudhibiti mkojo na kinyesi.
Hivyo basi, mtu hapaswi kukaa chooni kwa zaidi ya dakika tano au kumi.
Hakuna haja ya kutoa shinikizo kubwa kwenye misuli.
Ili kuepuka matatizo, mtu anapaswa kunywa lita mbili hadi tatu za maji kila siku, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, na kuongeza ufumwele lishe."
Ni muhimu pia kuona daktari ikiwa dalili za maumivu ya tumbo au tumbo kujaa gesi itaendelea kwa zaidi ya siku mbili, alisema Dkt. Nikam.
Eneo lisilopaswa kuwa na simu
Dkt. Shahid Parvez, Daktari Mkuu katika Hospitali ya AIIMS, Dombivli, alisisitiza kwamba sababu ya ugonjwa wa bawasili na matatizo yanayohusiana nayo siyo tu ukosefu wa ufumwele katika lishe, bali pia kukaa chooni kwa muda mrefu na kutumia simu kila wakati.
Hii husababisha shinikizo kwenye mishipa ya damu karibu na njia ya haja kubwa, na kusababisha maumivu makali wakati damu inapotoka katika vidonda vya utupu wa wanawake.
Aidha, vijidudu vinavyoweza kuwa kwenye simu kisha uguse uso na mikono, vinaweza kukusababishia maambukizi kwenye tumbo.
Dkt. Parvez alishauri watu kuunda maeneo yasiyotumika simu nyumbani, ikiwa ni pamoja na chumba cha kulala, eneo la kula, na choo, ili kuepuka matatizo ya kiafya yanayohusiana na matumizi yasiyofaa ya simu za mkononi.
Uyabisi wa tumbo husababisha bawasili
Gesi kujaa tumboni au kizuizi cha mchakato mzima wa mmeng'enyo wa chakula tumboni kunaweza kusababisha shida nyingi.
Wakati mfumo wa kusaga chakula tumboni unapoharibika, shinikizo huwekwa kwenye rektamu.
Hii inaweza kusababisha matatizo kama vile bawasiri.
Tatizo hili ni la kawaida kwa watu zaidi ya umri wa miaka 45.
Wagonjwa kama hao wana uwezekano mkubwa wa kupata shida kama vile bawasili.
Katika hali mbaya, kujaa kwa gesi tumboni kunaweza kusababisha damu kuganda kutokana na shinikizo kubwa kwenye rektamu, ambayo huongeza hatari ya mashambulizi ya moyo na kiharusi.
Katika hali hiyo, ni muhimu kutibu kujaa gesi tumboni mara moja ili kuepuka matatizo ya baadaye.
Kushiba kupita kiasi kwa muda mrefu kunamaanisha kutopata choo kwa wiki moja au zaidi.
Dalili zake ni pamoja na kutokwa na damu, maumivu ya tumbo, kujilazimisha wakati wa kwenda haja kubwa, na matatizo ya kutokamilika kwa haja kubwa.
Tulipata habari zaidi kutoka kwa madaktari juu ya suala hili
Dkt. Lakin Veera, Daktari Mkuu katika Hospitali ya Apollo Spectra, Mumbai, alisema kuwa sababu za kuziba kwa njia ya haja kubwa ni pamoja na ukosefu wa nyuzi katika lishe, ukosefu wa mazoezi, matumizi ya vyakula vilivyosindikwa, na matatizo mengine ya kimwili kama kuzuiwa kwa utumbo wakati wa ujauzito au umri wa uzee.
Hali hii husababisha shinikizo kwenye mishipa ya damu ya mrija wa haja kubwa na kusababisha vidonda na michubuko.
Kujitahidi kwa muda mrefu kunaweza kusababisha michubuko ndani na nje ya tundu la haja kubwa.
Dkt. Veera aliongeza kusema kuwa asilimia 20 ya watu wa umri wa miaka 45 hadi 65 wanakutana na matatizo ya kujaa kwa gesi tumboni, na wengi wanahitaji matibabu ya haraka ili kuepuka matatizo kama vidonda vya bawasili na michubuko.
Dkt. Hemant Patel, daktari wa jumla katika Hospitali ya Zenova Shelby, Mumbai, alisema kuwa wagonjwa wengi wanaokuja kwa sasa wanakutana na matatizo ya kujaa gesi tumboni, maumivu ya tumbo, na kushiba kupita kiasi.
Alisisitiza umuhimu wa matibabu ya haraka, na kusema kwamba lishe yenye nyuzi nyingi, mazoezi ya mara kwa mara, na kunywa maji ya kutosha ni miongoni mwa hatua muhimu za kuboresha afya ya utumbo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi