Fahamu sababu za kiafya zinazosababisha kinyesi chako kuelea na wakati mwingine kuzama

    • Author, Richard Gray
    • Nafasi, BBC

Wakati mwingine kinyesi cha binaadamu huelea juu ya maji badala ya kuzama. Hivi karibuni imethibitishwa kisayansi hilo linapotokea, linaashiria kuna mabadiliko katika mfumo wa usagaji chakula.

Mkurugenzi wa Maabara ya Seli na Biolojia ya Saratani katika kliniki ya Mayo, huko Rochester, Minnesota, Nagaraja Kannan anauliza: Je, kinyesi chako kinaelea au kinazama?"

Utafiti wa kinyesi cha binadamu

Dkt. Kannan ametumia muda wake mwingi kusoma mifumo ya seli na molekuli ambayo husababisha saratani ya matiti.

Wakati akiwa likizo ya kikazi, Kannan alijaribu kutafuta jibu la swali jingine. Kwa nini kinyesi wakati mwingine huelea?

Labda wengi wetu tumekumbana na jambo hili. Wakati mwingine kinyesi cha binadamu huelea juu ya maji bila kuzama. Lakini, wakati mwingine huzama kabisa.

Aaamini jibu la swali hili litatoa maelezo kuhusu kile kinachoendelea ndani ya miili yetu na afya na vijidudu vinavyoishi humo.

Mafuta mengi

Hapo awali ilifikiriwa viwango cha mafuta kwenye kinyesi ndicho kilisababisha kinyesi kuelea. Lakini mwanzoni mwa miaka ya 1970 wataalamu wawili wa mfumo wa usagaji chakula kutoka Chuo Kikuu cha Minnesota waliamua kufanya msururu wa tafiti.

Baada ya kufanya vipimo kadhaa kwenye vinyesi vya watu 39 waliojitolea na vinyesi vya baadhi ya wataalamu wenyewe, jibu lao likawa sio mafuta bali ni gesi.

Kiwango cha gesi iliyopo kwenye kinyesi, husababisha kinyesi kuelea juu ya maji au kuzama. Watafiti waligundua ikiwa kinyesi hakina gesi kitazama na kinyume chake.

Walihitimisha kuwa sababu ya tofauti hii ni kutokana na uzalishwaji wa gesi ya methane kupita kiasi. Kwa maneno mengine, kuwepo kwa gesi tumboni kupita kiasi.

Na hapa ndipo Kannan anapoingia kwenye mada hii ya kusisimuwa. Katika miaka ya sasa - sayansi imegundua jukumu la vijidudu katika nyanja nyingi za afya yetu, husababisha unene hadi ugonjwa wa moyo.

Kannan alishuku kuwa bakteria trilioni 100 na vijidudu vingine kwenye matumbo yetu vinaweza kuwa ndio sababu ya vinyesi vyetu kuelea au kuzama.

Utafiti wa panya

Ili kujaribu nadharia hii, yeye na wenzake katika Kliniki ya Mayo walichunguza kinyesi cha panya waliokuzwa kwenye maabara. Panya hawa wasio na vijidudu kwenye matumbo yao.

Katika vipimo vya kuelea kwa kinyesi, kinyesi cha panya hawa mara moja kilizama kwenye maji. Lakini, karibu 50% ya vinyesi cha panya walio na vijidudu tumboni vilielea.

Baadaye, kulifanyika upandikizaji kwenye baadhi ya panya wasio na vijidudu. Waliingizwa bakteria kwenye matumbo yao. Panya hao walianza kutoa kinyesi kinachoelea.

Hata panya walipolishwa bakteria kutoka kwa watu waliojitolea, kinyesi kilielea.

"Mara tu vijidudu hivyo vinapotua kwenye utumbo, kinyesi cha panya huinuka mara moja, bila kujali vimetokea wapi," Kannan anasema.

Yeye na wenzake walifanya uchunguzi wa kina wa spishi za bakteria katika kinyesi kinachoelea kilichopatikana kutoka kwa panya. Pia walipata aina 10 za bakteria zinazozalisha gesi kwa wingi.

Kuhusu binaadamu

Ingawa matokeo ya majaribio ya panya yanapaswa kutumiwa kwa tahadhari, bado hayajathibitishwa sababu ya kuelea na kuzama kinyesi kwa upande wa binadamu.

Kannan anaamini kuelea kwa kinyesi chetu kunaweza kuwa ishara ya mabadiliko yanayosababishwa na bakteria katika mfumo wetu wa usagaji chakula.

Mambo mengi yanaweza kubadilisha muundo wa bakteria kwenye utumbo wetu, ikiwa ni pamoja na chakula chetu, kuvuta sigara, msongo wa mawazo na dawa mbalimbali tunazotumia.

Kannan sasa ana nia ya kuchunguza ini husababisha bakteria wanaotengeneza gesi kustawi.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah