Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afya: Kukosa kupiga mbweu inaweza kuwa dalili ya tatizo la kiafya
- Author, Aurelia Foster
- Nafasi, BBC
Watu ambao hawawezi kupiga mbweu hupata wasiwasi na msongo wa mawazo kwa sababu ya hali hiyo, pamoja na maumivu ya mwili, watafiti wanasema.
Kutoweza kupiga mbweu kunasababisha uvimbe wa tumbo, kelele za ajabu kifuani na shingoni na gesi tumboni.
Utafiti huo ulifanywa na kikundi cha wasomi kutoka chuo kikuu huko Texas.
Umechunguza ukubwa wa tatizo katika maisha ya kila siku ya watu, pamoja na athari zake za kiakili na kijamii, kwa sababu ni tatizo linaloweza kuathiri maisha ya mtu.
Kutokwenda mbweu hutokea wakati misuli ya koo inaposhindwa kukunjuka ili kuruhusu gesi kupanda.
Daktari wa koo, pua na masikio katika Hospitali ya Guy's and St Thomas huko London, Uingereza, Yakubu Karagama, anaeleza “hali hiyo imekuwa ikiwasumbua watu kwa muda mrefu."
“Unapokula au kunywa kitu unasikia maumivu, wagonjwa wengine wanalazimika kulala chini ili gesi itoke, wengine huweka kidole mdomoni kulazimisha kutapika na gesi ndio inatoka."
Karagama ansema amekuwa akiwatibu watu wenye tatizo hilo kwa sindano za Botox tangu 2016, ambazo hulegeza misuli ya koo. Anasema, “matibabu hayo yamedilisha maisha kwa karibu kila mgonjwa aliyemtibu.”
“Hata hivyo, matibabu hayo kwa sasa yanapatikana katika hospitali chache nchini Uingereza kwa sababu kuna uelewa mdogo kuhusu ugonjwa huu miongoni mwa wataalamu wa afya,” anaeleza Karagama.
"Watu wengi hucheka unaposema 'siwezi kupiga mbweu.' Watu hawaelewi kuhusu kupiga mbweu."
Kwa mujibu wa Karagama, haijulikani ni watu wangapi wana ugonjwa huo, lakini anaamini ni wengi.
"Watu wengi hata hawajui dalili wanazopata ni matokeo ya tatizo hili. Wagonjwa wengi wamekuja kwenye kliniki yangu wanasema wana shida hiyo katika maisha yao yote."
Msemaji wa Huduma ya Afya Ya Taifa (NHS) anasema: "Wafanyakazi wa NHS hupata ushauri wa kimatibabu kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Afya. Na huduma zinazofaa kwa wagonjwa walio na shida hiyo hutolewa.”
Utafiti huo kwa watu 199 ambao hawawezi kupiga mbweu, ulihitimisha kuwa kuna na uelewa mdogo sana kuhusu hali hiyo miongoni mwa wataalamu wa afya.
Watafiti wanasema uelewa mzuri wa ugonjwa huo unaweza kuongeza viwango vya utambuzi na matibabu. Na kupelekea hali bora ya maisha kwa wagonjwa.
Watafiti waligundua nusu ya watu wasio piga mbweu nchini Uingereza walijadili dalili zao na madaktari, lakini 90% wanasema hawakupokea msaada wa kutosha.
Ugonjwa huo ulipokea jina rasmi la DCF-R mwka 2019, wakati daktari Mmarekani, Robert W. Bastian, kutoka Chicago, alipogundua misuli ya koo kuwa ndio chanzo cha tatizo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah