Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afya: Kwanini baadhi ya watu hawapungui uzito hata kwa mazoezi na lishe?
Watu ambao ni wanene au wazito wanalalamika kwamba hawawezi kupunguza uzito licha ya lishe na mazoezi, au hawawezi kudhibiti uzito wao. Sababu ya hilo ni nini?
Mtu anaposikia neno 'mafuta, ongezeko la uzito, au kunenepa,’ jambo linalokuja akilini - ni ulaji usiofaa, kula kupindukia na maisha ya anasa.
Hakika hizi ni sababu kuu za kuongezeka uzito. Lakini wale ambao hawawezi kupunguza uzito licha ya mazoezi ya kawaida au lishe, kuna sababu nyingine nyuma ya uzito huo.
Kemikali za Obesogens (osojeni.) Hizi zinaathiri mfumo wa usagaji chakula na wakati mwingine huathiri homoni pia.
Kiwango cha juu cha kemikali za osojeni katika mwili huongeza idadi na ukubwa wa seli zinazohusika na uhifadhi wa mafuta. Na bakteria ambao hufyonza mafuta, hupunguza kufanya hivyo. Na kupelekea kuongezeka unene wa safu ya mafuta chini ya ngozi.
Unene na kisukari cha aina ya pili - vinanaweza kusababisha shinikizo la damu, magonjwa ya moyo au matatizo ya moyo, kukosa usingizi na hata saratani.
Pia, kutokana na mkusanyiko wa glukozi na asidi ya mafuta katika viungo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ini, mabadiliko katika shughuli za homoni hutokea na matatizo ya usagaji chakula pia hutokea.
Hata hivyo, kemikali hizi hufanya uharibifu mkubwa zaidi ikiwa ziko tumboni au umezipata wakati wa utoto. Zinaweza kubadilisha muundo wa 'DNA,’ shughuli za seli na pia zinaweza kuathiri vizazi vijavyo.
Kwa maneno rahisi, kutokana na kemikali za osojeni – mmenge’nyo wa chakula, uzazi na ukuaji wa binadamu huathirika zaidi.
Kemikali hizi zinatoka wapi?
Bidhaa nyingi tunazotumia siku hizi zina kemikali hizi za osojeni. Kwa mfano; sabuni au bidhaa yoyote ya usafi, vipodozi, vyakula vya kwenye mapaketi, vyombo vya plastiki, vyombo vya kupikia, nguo, vifaa vya kuchezea, vifaa vya matibabu n.k.
Bidhaa hizi tunazitumia sana katika maisha yetu kiasi cha kwamba hatuwezi kuziepuka. Kutokana na matumizi ya mara kwa mara ya bidhaa hizo - hupelekea chakula, maji na hewa kuchafuka na watu kuwa katika hatari ya kunenepa kupita kiasi na magonjwa mengine.
Kuna aina 50 za kemikali za osojeni katika mwili wa binadamu, kemikali yoyote kati ya hizo inapoongezeka mwilini na uzito huanza kuongezeka. Kati ya kemikali hizo tano ni hatari zaidi; BPA, Phthalate, Atrazine, Organotins na PFOA.
BPA
Vyombo vya chakula, makopo ya chakula na vinywaji na vifaa vya plastiki vyote vina BPA. Hii inaathiri utengenezaji wa homoni ya ngono kwa wanawake, sukari ya mwili na uundaji wa mafuta.
Inaweza kusababisha unene, kisukari na shinikizo la damu. Watu huathiriwa na BPA kupitia chakula ikiwa mtu atapasha moto au kuhifadhi chakula cha moto kwenye vyombo vya plastiki vyenye BPA.
BPA huathiri watu wa rika zote, hata watoto wachanga. Damu, mkojo, maziwa ya mama na mafuta hupimwa ili kugundua BPA.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani-FDA, kiasi cha BPA kilichomo kwenye pakiti za chakula ni kidogo sana na haileti hatari kwa mwili wa binadamu.
Phthalates
Kemikali hutumiwa kuifanya plastiki kudumu na kunyumbuika. Hupatikana katika vifaa vya kuchezea, vifaa vya matibabu, vifungashio vya chakula, sabuni, kemikali za usafi, shampoo, rangi ya kucha, losheni na manukato.
Kemikali hii huathiri homoni ya kiume ya androjeni, na kusababisha matatizo katika usagaji chakula. Na kusababisha hatari ya kuongezeka uzito na kupata kisukari cha aina ya 2.
Kemikali hii inaweza kuingia katika mwili wa binadamu kwa kula chakula kutoka katika vyombo na vifungashio vyenye phthalates au kutumia bidhaa zenye kemikali hizi.
Hata hivyo, Kituo cha Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), kinasema kiasi cha phthalates kinachopatikana katika pakiti za chakula au vipodozi si hatari kwa afya.
Atrazine
Atrazine ni kemikali inayotumika kuongeza uzalishaji wa mazao. Kutokana na hilo, kemikali hii hupatikana kwenye udongo na maji.
Inaathiri homoni za ngono kwa wanaume na wanawake. Pia, huongeza hatari ya kunenepa kupita kiasi, kisukari, kasoro za kuzaliwa na hata saratani.
Organotins
Kemikali hii hupatikana katika bidhaa kama vile mabomba, rangi na dawa zinazotumiwa kwenye boti au meli.
Ndiyo maana kemikali hii inapatikana kwenye konokono wa baharini na katika maji. Pia, kemikali hii hupatikana katika plastiki za kuchezea, vifaa vya kuandikia na nguo.
Ina athari kwenye homoni za ngono na huongeza mafuta mwilini.
PFOA
PFOA hupatikana katika kitambaa chochote kisichopitisha maji kama vile; makoti ya mvua, mwavuli, hema, vyombo vya kupikia, vipodozi, bidhaa za usafi, dawa za kuzuia madoa na katika vyakula vilivyowekwa kwenye microwave.
Kemikali hii husababisha unene wa kupindukia, kisukari na kuongezeka uzito.
Je, kemikali hizi zinaweza kuepukwa?
Kuna mambo machache ya kuzingatia ili kuepuka kemikali hizi:
- Kwanza kabisa, unapaswa kuacha sigara.
- Kupunguza ulaji wa vyakula na vinywaji vilivyowekwa katika vifurushi na makopo/chupa.
- Tumia chuma, gilasi au udongo badala ya vyombo vya plastiki.
- Ikiwa vyombo vya plastiki vitatumika, hakikisha havina kemikali hizi.
- Usipashe moto chakula au kuweka chakula moto kwenye plastiki yoyote.
- Punguza matumizi ya vyakula vilivyotiwa dawa.
- Tutumia vipodozi ambavyo havina kemikali hatari.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi