Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afya: Kwanini watoto wengi wana unene wa kupindukia?
India imekuwa ikiongoza kwa muda mrefu katika orodha ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watoto wenye utapiamlo duniani.
Sasa inazidi pia kuripoti viwango vya kutisha vya kunenepa kwa watoto ambavyo, wataalam wanasema, vinaweza kuwa janga ikiwa suala hilo halitashughulikiwa kwa haraka.
Wakati Mihir Jain mwenye umri wa miaka 14 alipoingia kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Max ya Delhi mwaka 2017 kwenye kiti chake cha magurudumu ili kushauriana na Dk Pradeep Chowbey, daktari wa upasuaji alisema " sikuamini macho yangu".
"Mihir alikuwa na unene uliopitiliza, hakuweza kusimama ipasavyo na hakuweza kufungua macho yake kwani uso wake ulikuwa mnene sana. Alikuwa na uzito wa 237kg .
Baada ya wiki za matibabu na upasuaji wa njia ya utumbo katika msimu wa joto wa 2018, uzito wa Mihir ulipungua hadi kilo 165.
Wakati huo, Mihir alielezewa kama "kijana mzito zaidi duniani", ambapo India inakadiriwa kuwa na watoto milioni 18 wenye unene uliopitiliza huku idadi yao ikiongezeka kila uchao.
Utafiti wa hivi karibuni wa Kitaifa wa Afya ya Familia (NFHS-5, uliofanyika mwaka wa 2019-21), ukifanya uchunguzi wa kina kwa kaya mbalimbali wa viashiria vya afya na kijamii uliofanywa na serikali, uligundua kuwa 3.4% ya watoto chini ya miaka mitano sasa wana uzito mkubwa ikilinganishwa na 2.1% mwaka 2015- 16.
Kwa mtazamo wake, idadi inaonekana ndogo, lakini Dk Arjan de Wagt, mkuu wa lishe katika shirika la Unicef nchini India, anasema kwamba "hata asilimia ndogo sana inaweza kumaanisha idadi kubwa sana" kwa sababu ya wingi wa wakazi wa India.
Kwa mujibu wa takwimu za Unicef ya World Obesity Atlas ya 2022, India inatabiriwa kuwa na zaidi ya watoto milioni 27 wanene, ikiwakilisha mtoto mmoja kati ya 10 duniani, ifikapo mwaka 2030. Inashika nafasi ya 99 katika orodha ya nchi 183 kwa kuzingatia utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa kunenepa sana. Athari za kiuchumi za unene uliopitiliza na unene unatarajiwa kuongezeka kutoka $23bn mwaka 2019 hadi $479bn ifikapo 2060.
"Tunaangalia tatizo kubwa la kunenepa kwa watoto nchini India," anasema Dk de Wagt. "Na kwa sababu tabia ambayo huanza kunenepa kwa ujumla huanzia utotoni, watoto wanene hukua na kuwa watu wazima wanene."
Watoto wa chini ya miaka mitano wenye uzito wa kupindukia
Na huo ndio wasiwasi mkubwa kwa wataalam wa afya. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO, mafuta mengi mwilini huongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni pamoja na aina 13 za saratani, kisukari cha aina ya pili, matatizo ya moyo na mapafu, hivyo kusababisha vifo vya mapema.
Mwaka jana, ugonjwa wa unene uliopitiliza ulisababisha vifo milioni 2.8 ulimwenguni kote.
India tayari imeingia katika nchi tano za juu kwa suala la unene wa watu wazima katika miaka michache iliyopita.
Takwimu za mwaka 2016 ziliwaweka Wahindi milioni 135 katika kundi la watu wanene zaidi huku idadi yao ikiongezeka.
Dkt. de Wagt anasema kwamba nchini India - ambapo 36% ya watoto chini ya miaka mitano bado wamedumaa - mafanikio ambayo tumekuwa tukiyapata katika kupambana na utapiamlo yanakabiliwa na lishe kupita kiasi.
"Watu wana lishe duni na lishe zaidi kwa wakati mmoja. Uzito kupita kiasi na unene ni matokeo ya lishe iliyozidi, lakini hiyo haimaanishi kwamba mtu anapata lishe yote anayohitaji."
Tatizo kubwa, anasema, "ni kutojua na ufahamu wa kutosha kuhusu lishe".
"Ikiwa watoto watapewa milo yenye usawa ambayo ni pamoja na wanga, protini, vitamini, matunda na mboga mboga, basi itazuia utapiamlo na kunenepa kupita kiasi.
Lakini watu hawajui ni chakula gani kizuri, wanakula kujaza matumbo yao kwa wanga zaidi, chakula cha urahisi zaidi."
Dk de Wagt anasema takwimu zinaonyesha kuwa ingawa unene wa kupindukia wa utotoni ni tatizo miongoni mwa tabaka zote za kijamii, hutokea zaidi katika familia tajiri za mijini ambapo watoto wanalishwa mlo wa vyakula na vinywaji vyenye mafuta mengi, sukari na chumvi nyingi.
Uchunguzi wa mwaka 2019 wa Max Healthcare huko Delhi na vitongoji vyake ulifichua ya kwamba takriban 40% ya watoto (miaka 5-9), vijana (wenye umri wa miaka 10-14) na vijana (wenye umri wa miaka 15-17) walikuwa na uzito wa kupindukia.
"Vijana hulala wakiwa wamechelewa na mara nyingi hukimbilia kula usiku wa manane, haswa kwa vitafunwa visivyofaa," anasema Dk Chowbey.
"Hawachomi kalori yoyote baada ya kula usiku sana kwani wanalala baada ya hapo na wakati wa mchana, wana uchovu, jambo ambalo linamaanisha kuwa wanachoma kalori chache sana.
Isitoshe, watoto wanatumia wakati mwingi kwenye kompyuta na simu badala ya kukimbia ama kucheza." "Unene kupita kiasi," anaonya pia, "athari si za kimatibabu tu, bali kila nyanja ya maisha, ikiwa ni pamoja na kisaikolojia na kijamii.
Watoto wanene mara nyingi wanakabiliwa na chuki na kutengwa na jamii.
Dk Ravindran Kumeran, daktari wa upasuaji katika mji wa kusini wa Chennai (Madras) na mwanzilishi wa Taasisi ya Obesity ya India, anasema tusipoingilia kati watoto sasa, hatutaweza kukabiliana na tatizo la unene nchini.
"Ukitazama TV sasa kwa muda wa nusu saa, utaona matangazo mengi kuhusu vyakula vya hovyo na vile vinavyotukuza vinywaji baridi. Ujumbe huu wa uongo wa mara kwa mara kuhusu faida za vyakula visivyo na afya lazima ukomeshwe, na inaweza kufanywa na serikali pekee."
Pia, anasema, tunahitaji kupata watoto wengi zaidi wakicheza nje. "Kama nchi hatuwekezi katika utimamu wa mwili. Miji yetu haina njia za miguu, hakuna njia salama za baisikeli, na kuna viwanja vichache vya michezo ambapo watoto wanaweza kucheza."
Hivyo ndivyo shirika la Sportz Village, ambalo ni shirika la michezo ya vijana, linavyojaribu kubadilisha, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji Saumil Majumdar aliambia BBC.
“Katika nchi yetu shule ndiyo sehemu pekee inayotoa sehemu salama kwa watoto kucheza, hivyo shule lazima zitoe mchango wake katika kupambana na unene,” anasema.
Uchunguzi wao wa watoto zaidi ya Watoto 254,000 ulionesha kuwa mtoto mmoja kati ya wawili hakuwa na afya inayoridhisha; idadi kubwa ya watoto walikosa kunyumbulika, walikuwa na nguvu duni.
Sio shida ya sera. Shule zote zina madarasa ya elimu ya viungo, lakini kwa ujumla ni watoto walio vizuri tu ndio hupata uangalizi wa kutosha.
Kwa hivyo si jambo la kufurahisha kwa watoto ambao hawafurahii kucheza," Bw Majumdar anasema. "Tunaamini kuwa shuleni kama vile watoto wanapaswa kujifunza kiwango cha msingi cha somo lolote, kwa namna hiyo hiyo lazima wafundishwe viwango vya msingi vya usawa."
Kwa miaka mingi, anasema, shule ambazo wamefanya nazo kazi zimeonesha maboresho kadhaa.
"Katika baadhi ya matukio tumeona viwango vya usawa huku baadhi ya vigezo vikiwa vimeboreshwa kutoka 5% hadi 17% na pia tumeweza kupata wasichana wengi zaidi wa kucheza. Nadhani kucheza kunaweza kutatua matatizo yote ya dunia," anaongeza.