Ukweli usioujua kuhusu simu yako - na kwa nini unahitaji kuacha kuitumia chooni

Tunazibeba kila mahali, tunaenda nazo chumbani kulala nazo, chooni na kwa watu wengi huwa ndio kitu cha kwanza wanachoamka nacho asubuhi - zaidi ya asilimia 90% ya watu ulimwenguni wanamiliki au hutumia simu za mkononi (rununu) na wengi wetu hatuwezi kukaa bila simu.

Ingawa utumiaji wa simu huzingatia athari zake za kiafya na wakati kuendesha gari, athari za mawimbi ya redio, lakini hatari ya maambukizo ya vijidudu kwenye simu yako haitazamwi sana - lakini tatizo kubwa.

Utafiti wa mwaka 2019 uligundua kuwa watu wengi nchini Uingereza hutumia simu zao wakiwa chooni. Kwa hivyo haishangazi kuona tafiti zimegundua simu zetu za mkononi ama rununu kuwa chafu zaidi ya masinki ya vyoo.

Tunawapa simu zetu watoto wacheze nazo (ambazo hazijulikani vyema usafi wake). Pia tunakula huku tukitumia simu zetu na kuziweka kila mahali. Vyote hivi vinaweza kuhamisha vijidudu kwenye simu yako pamoja na akiba ya chakula kwa vijidudu hivyo kula.

Inakadiriwa kuwa watu hugusa simu zao kwa zaidi ya mamia au maelfu ya mara kwa siku. Na ingawa wengi wetu tunanawa mikono mara kwa mara baada ya mfano, kwenda chooni, kupika, kusafisha, au kutengeneza bustani, kuna uwezekano mdogo sana wa kufikiria kunawa mikono yetu baada ya kugusa simu zetu. Lakini kutokana na jinsi simu zinavyoweza kuathiriwa na vijidudu, pengine ni wakati wa kufikiria zaidi juu ya usafi wa simu yako ya mkononi.

Vidudu, bakteria, virusi

Mikono hubeba bakteria na virusi kila wakati na inatambulika kama njia moja wapo ya kupata maambukizi. Vivyo hivyo na simu tunazogusa pia. Tafiti kadhaa zilizofanywa kuhusu ukoloni wa kibayolojia wa simu za mkononi ama rununu zinaonyesha kuwa zinaweza kuambukizwa na aina nyingi tofauti za bakteria zinazoweza kusababisha magonjwa kwa binadamu.

Hizi ni pamoja na E. coli inayosababisha kuhara (ambayo, hutoka kwenye kinyesi cha binadamu) na Staphylococcus inayoathiri ngozi, Actinobacteria, ambayo inaweza kusababisha kifua kikuu na diphtheria na Citrobacter, ambayo inaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo.

Klebsiella, Micrococcus, Proteus, Pseudomonas na Streptococcus pia zimeonekana kwenye simu na zote zinaweza kuwa na athari mbaya kwa wanadamu.

Utafiti umegundua kuwa vimelea vingi vya magonjwa kwenye simu mara nyingi ni sugu kwa viua sumu au dawa, ikimaanisha kwamba haviwezi kudhibitiwa kwa dawa za kawaida. Hii inatia wasiwasi kwani bakteria hawa wanaweza kusababisha matatizo ya ngozi, tumbo na maambukizo ya mfumo wa upumuaji ambayo yanaweza kuhatarisha maisha.

Utafiti pia umegundua kuwa hata ukisafisha simu yako kwa vitambaa maalumu zenye dawa za kuua bakteria au wipes za antibacterial au pombe bado inaweza kuvamiwa tena na vijidudu, ikionyesha kuwa usafishaji lazima uwe mchakato wa kawaida.

Simu zina plastiki ambayo inaweza kubeba na kusambaza virusi ambavyo baadhi yake (virusi vya homa ya kawaida) vinaweza kuishi juu plastiki ngumu kwa hadi wiki moja.

Virusi vingine kama vile COVID-19, rotavirus (kidudu cha tumbo kinachoambukiza sana ambacho huwaathiri watoto wachanga na watoto wadogo), mafua na norovirus - ambayo inaweza kusababisha maambukizi makubwa ya kupumua na tumbo - inaweza kudumu kwa mfumo wa kuambukizwa kwa siku kadhaa tu.

Hakika, tangu mwanzo wa janga la COVID, Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani vimeanzisha miongozo ya kusafisha na kuua vijidudu katika simu za rununu pamoja na vitasa vya milango na mashine za kutolea pesa (ATM) ambazo huchukuliwa kma vitu vinavyo hifadhi vijidudu vya maambukizi.

Wasiwasi umeonyeshwa kuhusu jukumu la simu za mkononi katika kusambaza vijidudu vya maambukizi.

Safisha simu yako

Kwa hiyo ni wazi kwamba unahitaji kuanza kusafisha simu yako mara kwa mara. Tume ya Mawasiliano ya Shirikisho la Marekani inapendekeza usafi wa kila siku wa simu yako na vifaa vingine.

Tumia wipes zilizo na pombe au dawa. Unahitaji kuwa na angalau 70% ya pombe ili kuua vijidudu kwenye simu hasa kwenye ‘skrini’ za kugusa, na zoezi hili linahitaji kufanyika kila siku ikiwezekana.

Usinyunyize dawa za kuua vijidudu moja kwa moja kwenye simu. Epuka kabisa kutumia bleach. Na osha mikono yako vizuri baada ya kumaliza kusafisha.

Kufikiria jinsi unavyoshughulikia simu yako pia kutasaidia kuiepusha kuwa makazi ya vijidudu. Ukiwa haupo nyumbani, weka simu yako mfukoni, au kwenye kamfuko. Usitumie simu mara kwa mara kuperuzi, tumia kwa vitu vya msingi kupunguza maambukizi. Gusa simu yako kwa mikono safi - iliyooshwa kwa sabuni na maji au dawa ya kuua vijidudu.

Kuna mambo mengine unaweza kufanya ili kuepuka simu yako kuwa chanzo cha virusi. Usishiriki simu yako na wengine ikiwa una maambukizi yoyote, au hujanawa kwanza. Ikiwa watoto wanaruhusiwa kucheza na simu yako, isafishe haraka iwezekanavyo baada ya kuitumia.

Na uwe na mazoea ya kuweka simu yako mbali wakati haitumiki, kisha kusafisha au kunawa mikono yako. Unaweza pia kutaka kusafisha chaja ya simu yako mara kwa mara unaposafisha simu yako.