Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mpatakuva: Majani yanayotumika kama mbadala wa karatasi za chooni Afrika na Marekani
- Author, Soo Min Kim
- Nafasi, BBC
Je, majani ya mpatakuva ama Plectranthus barbatus (boldo) kwa lugha ya kiengereza, ni mbadala endelevu kwa karatasi za gharama kubwa za chooni katika bara la Afrika?
Martin Odhiambo, mtaalamu wa mitishamba katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Kenya, anasema majani hayo yanaweza kuwa karatasi ya chooni ya siku zijazo."
Kama ilivyo kwa bidhaa nyingine nyingi, bei ya karatasi za chooni imeongezeka kote barani Afrika. Ingawa zinatengenezwa barani, lakini karatasi zinazotumika katika utengenezaji wake mara nyingi huagizwa kutoka nje.
Martin, mtaalamu wa mimea, anaamini jibu la kupanda kwa gharama ya karatasi za chooni huenda tayari lipo katika bara hili.
"Majani ya mpatakuva ni karatasi ya chooni ya Kiafrika. Vijana wengi leo hawafahamu mmea huu, lakini una uwezo wa kuwa mbadala wa rafiki kwa karatasi za chooni," anasema.
‘Majani yake ni laini,’’ anasema Martin, na harufu yake ni kama majani ya mnanaa (mint).
Mmea huo hulimwa kote barani Afrika na unatumika katika maeneo ya vijijini, hivyo basi kupatikana kwake ni kwa urahisi.
Majani hayo yana ukubwa sawa na mraba wa karatasi ya chooni inayotengenezwa viwandani, na yanaweza kutumika katika vyoo vya kisasa.
Benjamin, ambaye amekuwa akitumia mpatakuva kwa zaidi ya miaka 25, analima mmea huo kwenye ua wake, karibu na nyumba yake huko Meru, Kenya.
Anasema: "nilijifunza kuhusu mmea huo kutoka kwa babu yangu mwaka 1985 na nimekuwa nikiutumia tangu wakati huo. Ni laini na una harufu nzuri."
Unaweza kutumiwa na kila mtu?
Bado hakuna ulimaji mwingi wa mme huo. Lakini uwezo wake kwa sasa unachunguzwa katika nchi nyingine nje ya Afrika.
Robin Greenfield, mwanaharakati wa mazingira nchini Marekani, anasema amekuwa akitumia majani ya mpatakuva kwa miaka mitano sasa.
Robin amepanda zaidi ya miti mia moja ya mpatakuva kwenye kitalu chake huko Florida. Amegawa miche kupitia mpango unaohimiza watu kupanda miti hiyo kwa matumizi ya chooni.
“Kuna watu wengi wanahusisha matumizi ya mmea huu chooni na umaskini, lakini niwakumbushe wanapotumia karatasi za chooni bado wanatumia mimea, tofauti ni kwamba zimepitia tu viwandani,” anasema.
Robin anasema amepokea maoni chanya kutoka kwa watu ambao wametumia mmea huo. Anasema ni watu wanaothamini kukuza mmea huu kwa matumizi ya chooni.
"Kwa mtu yeyote ambaye anasitasita kujaribu mpatakuva kama karatasi ya chooni, niseme achana na wasiwasi kuhusu watu watasema nini kuhusu wewe.’’
Anaongeza kuwa, “nitabaki peke yangu. Nikimaanisha nitaendelea kujifuta kwa majani laini ambayo mimi mwenyewe hupanda."
End of Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla