Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uhaba wa vyoo huua kuliko risasi
Takribani nusu ya idadi ya watu duniani wako katika hatari ya kuaga dunia kutokana na magonjwa yatokanayo na mazingira machafu - Umoja wa Mataifa unasema.
Mifumo duni ya maji taka na maji machafu yanaweza kusababisha magonjwa ya kuendesha (kuhara) na magonjwa mengine hatari kwa maisha - maji hayo yanapochanganyika na maji yanayotumika kwa kunywa.
Tarehe 19 Novemba ni Siku ya Usafi Duniani, iliyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2013. Kulingana na ripoti ya 2023 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), karibu watoto 400,000 walio chini ya umri wa miaka 5 hunywa maji yasiyo salama.
Na hilo hupelekea vifo vya takribani watoto 1,000 kila siku. Ripoti hiyo pia inasema vifo vya kila mwaka vitaendelea kutokea kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji taka na maji machafu.
''Si jambo zuri hata kidogo. Ili kuboresha hali hiyo, inabidi tubadili mtazamo wa watu kuhusu mifumo ya maji taka. Tunapaswa kutambua mahitaji ya kimsingi ya afya ya kila siku,'' mtaalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anayehusika na usafi wa mazingira na udhibiti wa taka, Kate Madicock, aliambia BBC.
Eeneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, mataifa ya visiwa vya Asia Kusini na Pasifiki yanakabiliwa na changamoto kubwa katika suala la mifumo ya maji taka kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Nchini Nigeria
Idadi ya watu ambao hujisaidia nje ulimwenguni kote imepungua kwa theluthi mbili katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Lakini karibu watu milioni 4,200 duniani bado wanajisaidia nje, kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Nchini Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, watu milioni 46, asilimia 23 ya watu wote, bado wanajisaidia haja kubwa nje, na ndio kiwango cha juu zaidi duniani.
"Idadi ya wanaojisaidia nje bado ni kubwa kiasi kwamba kuacha kujisaidia nje limekuwa suala la heshima ya taifa," mkuu wa programu za misaada katika shirika la WaterAid Nigeria, Kolawole Banwo, aliiambia BBC.
Takriban Wanigeria milioni 95 hawana huduma za msingi za maji taka. Katika jimbo la kaskazini mashariki mwa Nigeri, Bono - mlipuko wa kipindupindu wa Januari 2023 uliua karibu watu 400.
Nigeria inapambana ili kumaliza tatizo la kujisaidia nje ifikapo 2025. UNICEF inasema ili kufikia lengo hilo kwa wakati, karibu vyoo milioni 4 vinahitajika.
Mabadiliko nchini India
Ripoti za mashirika ya kimataifa zinaeleza kuwa idadi ya vyoo imeongezeka tangu 2000.
Nigeria kwa sasa ina idadi kubwa zaidi ya watu wanaojisaidia nje. Lakini muongo mmoja uliopita, India ilikuwa na idadi kubwa zaidi, lakini serikali ya India iliweza kubadilisha hali ya mambo.
Mwaka 2014, idadi ya watu wanaojisaidia haja kubwa nje nchini India ilikuwa nusu ya watu milioni 1200 ambao hujisaidia nje duniani kote, na Asia Kusini ilichangia asilimia 90.
Wakati huo, kila shule moja kati ya tano kote nchini India hazikuwa na vyoo vya wasichana. Kampeni kubwa ya kujenga vyoo ilianza. Katika muda wa miezi 60 tu, karibu vyoo 110 vilijengwa kwa ajili ya watu milioni 600.
Serikali ya India ilitangaza 2019 kwamba "imekomesha tatizo vijijini la kujisaidia haja kubwa nje," lakini UNICEF inasema bado tatizo hilo linahitaji kukomeshwa zaidi.
Nchini Bangladesh
''Linapokuja suala la kusimamia mifumo ya maji taka bado tuko nyuma,'' Mkurugenzi wa WaterAid nchini Bangladesh, Hasan Jahan aliiambia BBC.
Chini ya Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa, Bangladesh imedhamiria kuwa na huduma ya vyoo safi vya kutosha ifikapo mwaka 2030.
Lakini juhudi hizi ni lazima ziende sambamba na kutokomeza umaskini. Katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, 25% ya wakaazi wa mji huo wenye watu milioni 4.4, wanaishi katika makazi duni.
''Bado kuna familia zinazotumia vyoo ambavyo haviwezi kuchukuliwa kuwa salama. Haiwezekani kujenga vyoo kwa sababu ya ufinyu wa nafasi,'' Gajahan analezea.
Suluhisho
''Changamoto ya wa mifumo ya maji taka na maji machafu ni kubwa, lakini suluhisho linaonekana kuwa rahisi. Kujenga vyoo vya kutosha na kuongeza mifumo ya maji machafu kunaweza kupunguza tatizo hili,'' Ann Thomas wa UNICEF anaeleza.
Pia kuna sababu nyingine zinazochangia tatizo hili kama vile upanuzi wa maeneo ya miji, athari za mabadiliko ya tabia nchi, ukame na mafuriko.
''Ikiwa tunataka kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, lazima tudhamirie duniani kote kuyafanya maji tunayotumia yasiwe machafu.''
Suluhisho jingine ni pamoja na kuwa na vyoo ambavyo havijaunganishwa na mifumo ya maji taka au vyoo vinavyotumia nishati ya jua.
Mtoto mmoja kati ya watatu duniani kote anaishi katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji. Mabadiliko ya hali ya hewa yanatishia kuzidisha hali hii, kulingana na utafiti wa UNICEF.
Vyoo visivyo tumia maji ni suluhisho kwa maeneo yanayokumbwa na uhaba wa maji.
Lakini wataalamu wanasema jinsi hali ya hewa inavyozidi kuwa mbaya, mabadiliko ya hali ya hewa yataathiri nchi maskini na tajiri - hivyo kuzingatia suluhisho zitokanazo na teknolojia ni jambo bora zaidi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah