Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Namna haja ndogo ilivyo 'lulu' Marekani
- Author, Becca Warner
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Mkojo ulitumika kama mbolea katika Roma ya kale na China. Na sasa wakulima huko Vermont, Marekani wanarudisha mbolea hii ili kuongeza mavuno na kukuza mazao kwa njia endelevu zaidi.
Wakati Betsy Williams anapokwenda chooni, anajua kwamba mkojo wake hautopotea. Kwa miaka 12 iliyopita, yeye na majirani zake katika kijiji cha Vermont, wamekuwa wakikusanya mkojo wao na kuutoa kwa wakulima kwa ajili ya matumizi ya mbolea ya mimea yao.
Betsy anashiriki Mpango wa Urejeshaji Virutubisho vya Mkojo (UNRP), unaoendeshwa na Taasisi ya Rich Earth (REI), shirika lisilo la kiserekali lenye makao yake makuu Vermont.
Yeye na majirani zake 250 katika Kaunti ya Windham huchangia jumla ya galoni 12,000 (lita 45,400) za mkojo kila mwaka.
Mbolea hutengenezwaje?
Mkojo huo hukusanywa na lori na kupelekwa hadi kwenye tanki kubwa ambapo hupashwa moto hadi nyuzijoto 80C (176F) kwa sekunde 90. Kisha huhifadhiwa kwenye tanki lenye joto, tayari kunyunyiziwa kwenye shamba wakati ufaao kurutubisha mazao.
Wanasayansi wa zama hizi wamegundua kuwa mkojo unaweza kuongeza mara mbili mavuno ya mazao kama vile kabichi na mchicha ikilinganishwa na kutoweka mbolea, na mkojo huboresha mavuno hata katika udongo wenye rutuba kidogo.
Nguvu ya mkojo kama mbolea inatokana na nitrojeni na fosforasi iliyomo - virutubisho ambavyo huongezwa katika mbolea ya viwandani inayotumiwa kwenye mashamba mengi. Lakini mbolea hizi za viwandani huharibu mazingira.
Nancy Love, profesa wa uhifadhi wa mazingira katika Chuo Kikuu cha Michigan ambaye yuko katika timu ya REI zaidi ya miaka kumi, amegundua kuwa kutumia mkojo badala ya mbolea ya kawaida ya kiwandani, hupunguza uzalishaji wa gesi chafu, na inatumia maji kidogo.
Kwa hakika, tangu mwaka 2012, UNRP inakadiria kuwa imehifadhi zaidi ya galoni milioni 2.7 (lita milioni 10.2) za mikojo.
Wasiwasi wa kiafya
Awali Betsy alikuwa akikusanya mikojo kwa kutumia chupa kubwa alizokuwa akitembea nazo kwenye buti ya gari lake na kisha kuzipeleka kwenye tanki kubwa la kukusanya mikojo, akifanya hivyo mara moja kwa mwezi.
Mara baada ya kuwa na mazoea ya kukusanya mkojo, Betsy hakupenda kuuacha mkojo upotee. "Sikupenda hata kwenda popote ambapo ningelazimika kukojoa na kushindwa kuhifadhi mkojo kwenye chupa. Ilikuwa ni sehemu ya utaratibu wangu, kama vile kufunga mkanda kwenye gari," anasema.
Kwa sasa Betsy anatumia mfumo wa choo ambao hutenganisha choo kikubwa na kidogo nyumbani kwake. Mkojo huo husafirishwa hadi kwenye tangi lililo ndani ya handaki chini ya ghorofa yake, na mkojo huo hufyonzwa mara kadhaa kila mwaka na lori ambalo humtembelea Betsy na wengine katika eneo lake wanaoshiriki katika mradi huo.
Mkojo unawasha na unanuka. Lakini Betsy, anasema "ni mfumo mzuri ambao unakuruhusu kutohangaika na mikojo. Ni kazi rahisi."
Hata hivyo, watu wengi wana wasiwasi kuhusu mbolea ya mkojo. REI imefanya utafiti, ingawa matokeo ya mwisho bado hayajatolewa, lakini matokeo ya awali yanaonyesha hakuna madhara ya kiafya kwa watumiaji wa mbolea hiyo.
Wasiwasi kuhusu hatari za kiafya, Betsy anasema, "ni mtazamo wetu wa Kimagharibi ambao unahitaji kubadilika haraka."
"Sisi sio wakamilifu, lakini tunajaribu angalau kuwajibika kwa kile kinachotokea katika uchafu wetu wa mwili," anasema Betsy.