China 'yaipiga pabaya' Marekani yatumia madini adimu kama silaha

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Aisha Pereira
- Akiripoti kutoka, BBC Singapore
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Vita ya kibiashara kati ya China na Marekani inazidi kupamba moto, huku wachambuzi wakielekeza macho yao kwenye ushuru wa kisasi unaowekwa katika bidhaa zinzozuzwa kati ya nchi hizi mbili.
Lakini ushuru wa kisasi sio silaha pekee ambayo Beijing inaitumia katika vita hii. China pia imeweka vikwazo vya usafirishaji nje kwa idadi kubwa ya madini adimu na sumaku, jambo ambalo linaonekana na wengi kama pigo kubwa kwa Marekani.
Hatua hii imefichua kiwango cha utegemezi wa Marekani kwa madini haya, na Rais Donald Trump ameiagiza Wizara ya Biashara kutafuta njia za kusaidia uzalishaji wa madini haya nchini Marekani na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, kama sehemu ya juhudi za Washington kufufua sekta hii muhimu.
Lakini madini haya adimu ni nini? Na kwa nini yana athari kubwa katika vita hii ya kibiashara?
Madini adimu ni nini na yanatumika wapi?
Madini adimu ni kundi la madini 17 yenye mfanano wa kikemikali ambazo ni muhimu sana katika utengenezaji wa bidhaa nyingi za teknolojia ya hali ya juu.
Licha ya kupatikana kwa wingi kwenye maeneo kadhaa, hujulikana kama adimu kwa sababu mara chache hupatikana katika katika ubora wake, na mchakato wa kuyachimba ni hatari.
Watu wengi huenda wasiyafahamu kwa majina kama neodymium, yttrium, na europium, lakini wanazifahamu bidhaa zinazotengenezwa kutokana na madini hayo.
Kwa mfano, neodymium hutumika kutengeneza sumaku zinazotumika katika spika, diski za kompyuta, na injini za magari ya umeme na ndege za kivita ambapo huchangia katika kuwa na vifaa vidogo zaidi na vyenye ufanisi mkubwa.
Yttrium na europium hutumika katika kutengeneza skrini za televisheni na kompyuta, ambapo husaidia katika kuonyesha rangi.
"Madini adimu hutumika katika kutengeneza kila kifaa kinachoweza kuwashwa au kuzimwa," anasema Thomas Cromer, mkurugenzi wa Kikundi cha Ginger kinachojihusisha na Biashara na Uwekezaji wa Kimataifa.
Madini haya pia ni sehemu muhimu ya teknolojia ya tiba, kama upasuaji kwa kutumia leza na vipimo vya MRI, pamoja na teknolojia muhimu za kijeshi.
China inadhibiti nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
China ina ukiritimba katika uchimbaji wa madini adimu, pamoja na kuyasafisha na kuyatenganisha na madini mengine.
China huchimba takriban asilimia 61 ya madini yote adimu duniani na huchakata asilimia 92 ya madini hayo, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA).
Hii inamaanisha kuwa China inadhibiti mnyororo mzima wa usambazaji wa madini haya, na inaweza kuamua ni kampuni zipi zitapokea madini hayo kutoka China.
Michakato ya uchimbaji na usafishaji ni ya gharama kubwa na pia husababisha uchafuzi wa mazingira. Madini haya huambatana na mionzi, jambo lililowafanya baadhi ya mataifa kama vile Umoja wa Ulaya kusita kuyachimba.
"Uzalishaji wa madini haya huacha taka zenye mionzi, na taka hizo zinahitaji kutupwa kwa njia salama na ya kudumu," anasema Thomas Krömer. "Lakini miundombinu ya kutupa taka hizo katika Umoja wa Ulaya bado ni ya muda tu."
China haikupata udhibiti huu wa mnyororo wa madini adimu kwa bahati, bali ni matokeo ya sera za kimkakati zilizoendelezwa kwa miongo kadhaa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 1992, aliyekuwa Rais wa China, Deng Xiaoping, alipotembelea Mongolia ya Ndani alisema: "Kama Mashariki ya Kati ina mafuta, basi China ina madini adimu."
Kwa mujibu wa Gavin Harper, mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, China ilianza kuwekeza katika sekta hii mwishoni mwa karne ya 20, na ikaitanguliza kwa uzalishaji wa gharama nafuu na viwango vya chini vya kimazingira na mishahara.
"China iliweza kuwashinda wapinzani wake duniani na kuwasukuma nje ya soko, hadi ikawa nchi yenye kuongoza na kudhibiti mnyororo mzima wa madini haya," Harper alisema.
China ilizuiaje usafirishaji wa madini haya?
Ili kukabiliana na kujibu ushuru wa Marekani, China mapema mwezi huu ilianza kuweka vikwazo vya usafirishaji kwa madini saba adimu ambayo mengi ni ya kundi la "madini mazito" ambayo ni muhimu sana katika sekta ya ulinzi.
Madini haya mazito ni adimu zaidi na ni magumu zaidi kuchakatwa kuliko madini mepesi, hivyo huwa ya gharama zaidi.
Tangu Aprili 4, kampuni zote zinahitajika kupata leseni maalum ya usafirishaji kabla ya kusafirisha madini au sumaku zake nje ya China.
China ina haki ya kuweka vikwazo kwa bidhaa zenye matumizi ya kiraia na kijeshi chini ya Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), ambao China imeridhia.
Kwa kuwa hakuna nchi nyingine yenye uwezo wa kuzalisha madini mazito kwa kiwango cha China, Marekani inajikuta katika hali ngumu, kwa mujibu wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa.
Hii inaweza kuiathiri vipi Marekani?
Ripoti ya Jiolojia ya Marekani ilisema kuwa Marekani iliagiza asilimia 70 ya madini adimu kutoka China kati ya 2020 na 2023, hivyo vikwazo vipya vitakuwa pigo kubwa.
Madini haya yanatumika sana katika viwanda vya kijeshi, kama vile utengenezaji wa makombora, rada, na sumaku za kudumu.
Ripoti ya Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati ilieleza kuwa teknolojia nyingi za ulinzi wa Marekani zinategemea madini haya, zikiwemo ndege za kivita aina ya F-35, makombora ya Tomahawk, na droni za kijeshi.
Hii inatokea wakati ambapo "China inaongeza uzalishaji wa silaha na kuendeleza mifumo ya kisasa ya kijeshi kwa kasi mara tano hadi sita zaidi ya Marekani," kwa mujibu wa ripoti hiyo.
"Sekta ya ulinzi ya Marekani itaathirika kwa kiwango kikubwa," anasema Thomas Cromer.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa ujumla, viwanda vya Marekani vitakumbwa na upungufu wa vifaa na ucheleweshwaji wa uzalishaji kutokana na usafirishaji kusimama na uhaba wa hifadhi ya madini haya.
Gavin Harper anatarajia bei ya bidhaa zinazotumia madini haya kuanzia simu janja hadi vifaa vya kijeshi kuongezeka sana.
Kampuni za Marekani zinazotengeneza bidhaa hizo pia zitakumbwa na kupungua kwa uzalishaji.
Iwapo vikwazo vya China vitaendelea, Marekani huenda ikalazimika kupanua vyanzo vya usambazaji na kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa ndani, lakini hili litahitaji uwekezaji mkubwa na wa muda mrefu, teknolojia mpya, na gharama kubwa zaidi.
Jumatatu iliyopita, Rais Trump aliamuru uchunguzi kuhusu hatari za kiusalama zinazotokana na utegemezi wa madini haya kutoka nje.
Agizo hilo la kiutendaji linasema: "Rais Trump anatambua hatari ya utegemezi mkubwa kwa madini haya na bidhaa zake kwa ajili ya uwezo wa ulinzi wa Marekani, maendeleo ya miundombinu, na ubunifu wa kiteknolojia. Madini haya ni muhimu kwa usalama wa taifa na uimara wa uchumi."
Je, Marekani haiwezi kuzalisha yenyewe madini haya?
Marekani ina mgodi mmoja pekee unaoweza kuzalisha madini haya, lakini hauna uwezo wa kuchakata madini mazito, hivyo huyatuma China kwa usafishaji.
Hadi miaka ya 1980, kulikuwa na kampuni za Marekani zilizozalisha sumaku za madini adimu, na Marekani ilikuwa mzalishaji mkubwa duniani.
Lakini kampuni hizi zilijiondoa sokoni, na China ikachukua nafasi hiyo kutokana na gharama zake za chini.
Wachambuzi wanaamini kuwa hii ndiyo sababu kubwa ya shauku ya Rais Trump kusaini makubaliano ya madini na Ukraine kupunguza utegemezi kwa China.
Trump pia ameonesha nia ya kuichukua Greenland ambayo ina hifadhi ya nane kwa ukubwa duniani ya madini haya.
Trump amewahi kusema wazi kuwa yuko tayari kutumia nguvu za kijeshi au kiuchumi kuiweka Greenland chini ya udhibiti wa Marekani.
Ukraine na Greenland huenda zikawa chanzo cha madini haya kwa Marekani, lakini matamshi ya chuki kutoka kwa Trump dhidi yao yanaifanya kazi hiyo kuwa ngumu.
"Marekani inakabiliwa na changamoto mbili," anasema Harper. "Kwa upande mmoja, imejiweka mbali na China, inayodhibiti madini haya, na kwa upande mwingine, imechukua msimamo wa uhasama dhidi ya mataifa ambayo hapo awali yalikuwa marafiki."
"Je, mataifa haya yataamua kubaki na urafiki wa Marekani kuwa kipaumbele? Hilo litaamuliwa na siku zijazo, kutokana na mazingira ya kisiasa yenye misukosuko ya utawala huu mpya," Harper aliongeza.
Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi












