Nani atamrithi Ayatollah Khamenei baada ya kifo cha Raisi?

RGFV

Chanzo cha picha, EPA

Kabla ya kifo chake kutokana na ajali ya helikopta, kulikuwa na imani kwamba hayati Rais wa Iran Ebrahim Raisi ndiye atakuwa mrithi wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Khamenei, ambaye ana umri wa miaka 85.

Raisi hajawahi kukanusha uvumi huu. Kabla ya urais wake, alishika nyadhifa kadhaa katika mahakama, na pia nafasi ya Makamu wa Rais wa Baraza la Wataalamu.

Licha ya kushindwa katika uchaguzi wa urais wa 2017, Kiongozi Mkuu alimteua kuwa mkuu wa idara ya mahakama. 2021, Raisi alishinda urais wa Iran na kuwa rais wa nane wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Je, Kiongozi Mkuu anachaguliwa vipi?

GFV

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Baraza la Wataalamu linamteua Kiongozi Mkuu na linaweza kumwondoa

Kiongozi Mkuu, Ayatullah Khamenei ni wa pili tu tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya 1979, amechaguliwa na baraza la maulamaa 88 linalojulikana kama Baraza la Wataalamu.

Wajumbe wa Baraza la Wataalamu huchaguliwa na Wairani kila baada ya miaka minane, lakini wagombea wa baraza hili lazima waidhinishwe na Baraza la Walinzi.

Wajumbe wa Baraza la Walinzi wanachaguliwa, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, na Kiongozi Mkuu. Kwa hivyo, Kiongozi Mkuu ana ushawishi mkubwa katika vyombo vyote viwili.

Baada ya kuchaguliwa, Kiongozi Mkuu anaweza kubaki katika nafasi hii maisha yake yote. Kwa mujibu wa katiba ya Iran, kiongozi mkuu lazima awe na cheo cha Ayatollah, ikiwa na maana awe kiongozi maarufu wa kidini wa madhehebu ya kishia.

Lakini Ali Khamenei alipochaguliwa hakuwa Ayatollah, hivyo sheria zilibadilishwa ili kumwezesha kuchukua nafasi hiyo. Kwa hivyo, sheria zinaweza kubadilika tena kulingana na hali ya kisiasa utakapo fika wakati wa kuchagua kiongozi mwingine.

TH

Kwa nini nafasi hii ni muhimu?

FG

Chanzo cha picha, ANADOLU AGENCY

Maelezo ya picha, Kiongozi Muadhamu ndiye mkuu wa muundo wa kisiasa wa Iran
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kiongozi Mkuu ana mamlaka makubwa nchini Iran. Ana usemi wa mwisho kuhusu masuala muhimu, na anaweka sera na mwelekeo wa nchi kuelekea ulimwengu wa nje.

Iran ndiyo nchi ya Kishia yenye nguvu zaidi duniani, na chini ya uongozi wa Ali Khamenei, imejaribu kuimarisha ushawishi wake katika Mashariki ya Kati.

Uadui kati ya Iran, Marekani na Israel, kwa mfano, ambao ulichochewa kwa kiasi kikubwa na chuki binafsi za Ayatollah Khamenei kwa nchi hizo, umesababisha mvutano wa miaka mingi na ukosefu wa utulivu katika eneo.

Utaratibu wa kuchagua mrithi umezoeleka kwamba kiongozi ajaye atakuwa na mielekeo sawa na Khamenei.

Khamenei alijenga ushawishi wake kupitia mtandao binafsi wa watiifu wake, ambao idadi kubwa ni wanachama wa chombo muhimu zaidi cha nchi, Walinzi wa Mapinduzi.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi huenda linaweza kujaribu kuzuia mgombea yeyote lionae hafai kuchukua ofisi hiyo. Ingawa kuna uvumi kuhusu orodha ya siri ya wagombea, hakuna anayejua ni nani na hakuna aliyedai kuifahamu.

Ripoti za ndani zinasema kuwa mgombea anayependekezwa na Ali Khamenei huenda ni mwanawe Mojtaba au marehemu Rais Ebrahim Raisi.

Mrithi wa Raisi kama mkuu wa Baraza la Mahakama, Sadiq Larijani, na Rais wa zamani Hassan Rouhani pia wana nafasi ya kuchukua nafasi hiyo.

Mojtaba Khamenei ni nani?

DC

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Walinzi wa Mapinduzi wakiongozwa na Meja Jenerali Hossein Salami ni jeshi kubwa la kisiasa na kiuchumi nchini Iran.

Ni mtoto wa kiume wa Kiongozi Mkuu Khamenei mwenye umri wa miaka 51 , alizaliwa katika mji wa kidini wa Mashhad. Yeye ni mhubiri kama baba yake.

Alingia kwenye vichwa vya habari, baada ya msako mkali dhidi ya waandamanaji kufuatia uchaguzi wa urais uliokuwa na utata wa mwaka 2009. Anaaminika alihusika na ukandamizaji huo.

GHBV

Chanzo cha picha, DPA/ALAMY LIVE NEWS

Maelezo ya picha, Mojtaba Khamenei

Ingawa Ali Khamenei si mfalme na hawezi tu kuhamisha madaraka kwa mwanawe, Mojtaba ana nguvu kubwa wakati huu wa uongozi wa baba yake, ikiwemo kusimamia ofisi inayosimamia vyombo vya kikatiba.

Iwapo atapata uungwaji mkono wa Walinzi wa Mapinduzi, inaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika mchakato wa kumpendekeza yeye.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah