Ni nani anaongoza Iran?

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amefariki katika ajali ya helikopta, na hivyo kufungua njia kwa uchaguzi mpya wa urais nchini humo.
Lakini kifo cha ghafla cha mhubiri huyo mwenye msimamo mkali hakitarajiwi kuathiri pakubwa siasa katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu, hasa pale mamlaka yanapokuwa na kiongozi mkuu wa nchi.
Ni nini kitafanyika Iran sasa?
Katiba ya Iran iko wazi linapokuja suala la rais kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya ugonjwa, kifo, au kushtakiwa na kuondolewa na bunge.
Kufuatia kifo cha Bw Raisi, Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei alimteua Makamu wa Kwanza wa Rais Mohammad Mokhber kusimamia masuala ya nchi.
Bw Mokhber ataandaa uchaguzi mpya wa urais - akishirikiana na wakuu wa bunge na mahakama - utakaofanyika ndani ya siku 50.
Katika uchaguzi uliopita, wote waliompinga rais walizuiwa kugombea, hivyo kumsafishia Raisi njia ya kuingia ofisini akiwa na idadi ndogo zaidi ya wapiga kura.
Walio wengi walisusia walichokiona kuwa uchaguzi uliopangwa.

Je, mamlaka ya kiongozi mkuu ni yapi?
Mtu mwenye mamlaka zaidi nchini Iran ni Ayatollah Khamenei, ambaye amekuwa kiongozi mkuu tangu 1989.
Ni mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu.
Pia ana mamlaka dhidi ya polisi wa kitaifa na polisi wa maadili.
Ayatullah Khamenei anadhibiti Jeshi la Ulinzi la Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambalo linasimamia usalama wa ndani, na mrengo wake wa kujitolea wa Basij Resistance Force - kutumika kuzima upinzani nchini Iran.
Rais ana mamlaka gani?
Rais ndiye afisa mkuu aliyechaguliwa na wa pili kwa cheo nyuma ya kiongozi mkuu.
Anasimamia uendeshaji wa kila siku wa serikali na ana ushawishi mkubwa juu ya sera za ndani na mambo ya nje.
Hata hivyo, uwezo wake ni mdogo – hasa katika masuala ya usalama.
Wizara ya mambo ya ndani ya rais inaendesha jeshi la polisi la taifa. Hata hivyo, kamanda wake anateuliwa na kiongozi mkuu na anawajibika moja kwa moja kwake.
Ndivyo ilivyo kwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Basiji.
Madaraka ya rais pia yanaweza kuthibitiwa na bunge, ambalo linabuni sheria mpya.
Kwa upande wake, Baraza la Walinzi - ambalo lina washirika wa karibu wa kiongozi mkuu - lina kazi ya kuidhinisha sheria mpya na inaweza kuzipinga.
Je, mamlaka ya serikali yamepingwa vipi nchini Iran?
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitikiswa na wimbi kubwa la maandamano mwaka 2022 kufuatia kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22, ambaye alizuiliwa na polisi wa maadili kwa madai ya kukiuka kanuni kali za mavazi za Iran.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema mamia waliuawa katika ukandamizaji huo na maelfu kutiwa mbaroni.
Maandamano hayo yaliongezeka kwa muda kutoka kwa kutoridhika na kanuni ya mavazi hadi hasira dhidi ya serikali kwa ujumla.

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi wa maadili ni nini?
Polisi wa maadili ni sehemu ya polisi wa kitaifa.
Kikosi hicho kilianzishwa mnamo 2005 ili kudumisha maadili na sheria za Kiislamu kuhusu mavazi "sahihi" ambayo yalianzishwa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.
Maafisa wake wanaokadiriwa kufikia 7,000 wanaume na wanawake wana uwezo wa kutoa onyo, kutoza faini au kuwakamata washukiwa.
Wiki kadhaa kabla ya machafuko katika majira ya joto ya 2022, Rais Raisi alikuwa ameamuru kuimarishwa kwa "sheria ya hijabu na usafi wa kimwili" ya Iran ambayo inawawajibisha wanawake kuzingatia vazi la hijab kulingana na muongozo wa kanuni za sheria.
Kamera za uchunguzi ziliwekwa mitaani ili kusaidia kuwakamata wanawake waliofichuliwa na hukumu ya lazima gerezani ilianzishwa kwa watu wanaopinga sheria za hijab kwenye mitandao ya kijamii.
Walinzi wa Mapinduzi ni akina nani?

Chanzo cha picha, Anadolu Agency
IRGC ni shirika kuu la Iran lililobuniwa kwa ajili ya kudumisha usalama wa ndani, na sasa ni jeshi kuu la kitaifa, kisiasa na kiuchumi nchini, na lina zaidi ya wafanyakazi 150,000.
Vikosi vyake vya ardhini, jeshi la wanamaji na anga, vinasimamia silaha za kimkakati za Iran.
Ina kitengo cha ng'ambo kinachofahamika kama Kikosi cha Quds ambacho hutoa kwa siri pesa, silaha, teknolojia na mafunzo kwa washirika wa Iran kote Mashariki ya Kati.
Pia inadhibiti Kikosi cha Basij.
Basij ni nini?
Kikosi cha Upinzani cha Basij, kilichotambuliwa rasmi kama Shirika la Uhamasishaji wa Wanyonge, kiliundwa mnamo 1979 kama shirika la kujitolea la kijeshi.
Ina matawi katika kila mkoa na jiji nchini Irani, na ndani ya taasisi nyingi rasmi za nchi.
Wanachama wake wanaume na wanawake, wanaojulikana kama "Basijis", ni watiifu kwa mapinduzi na chini ya maagizo ya IRGC.
Takriban maafisa 100,000 wanaaminika kutekeleza majukumu ya usalama wa ndani.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












