Ebrahim Raisi: Kiongozi wa kidini mwenye msimamo mkali aliyekuwa rais wa Iran

g

Chanzo cha picha, EPA

Ebrahim Raisi ni kiongozi wa kidini mwenye msimamo mkali aliye karibu na Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, ambaye kuchaguliwa kwake kama rais mwaka 2021 kuliimarisha udhibiti wa wahafidhina katika kila sehemu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi huyo wa zamani wa mahakama mwenye umri wa miaka 63 alimrithi Hassan Rouhani baada ya ushindi wa kishindo katika kura iliyoshuhudia wagombea wengi mashuhuri wenye msimamo wa wastani na wanamageuzi wakizuiwa kugombea na wapiga kura wengi kujiondoa kwenye upigaji kura.

Alichukua mamlaka wakati Iran ikikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na matatizo makubwa ya kiuchumi, kuongezeka kwa mvutano wa kikanda, na kukwama kwa mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia na mataifa yenye nguvu duniani.

Hata hivyo, muda wake madarakani umetawaliwa na maandamano dhidi ya serikali yaliyoikumba Iran mwaka 2022, pamoja na vita vya sasa vya Gaza kati ya Israel na kundi la Palestina linaloungwa mkono na Iran, Hamas, ambapo vita vya kichinichini kati ya Iran na Israel vilizuka wazi.

Pia amekabiliwa na wito unaoendelea kutoka kwa Wairani na wanaharakati wengi wa haki za binadamu wa kutaka uchunguzi ufanyike dhidi yake kuhusu jukumu lake katika mauaji makubwa ya wafungwa wa kisiasa katika miaka ya 1980.

Ebrahim Raisi alizaliwa mwaka wa 1960 huko Mashhad, jiji la pili kwa ukubwa nchini Iran na eneo takatifu zaidi ya Waislamu wa Shia nchini humo. Baba yake, ambaye alikuwa mhubiri wa kiislamu, aliaga dunia Raisi akiwa na umri wa miaka mitano.

Bw Raisi, ambaye huvaa kilemba cheusi kinachomtambulisha katika mila za Shia kuwa uzao wa Mtume Muhammad, alifuata nyayo za baba yake na kuanza kuhudhuria shule ya mafunzo ya dini ya Kiislamu katika mji mtakatifu wa Qom akiwa na umri wa miaka 15.

Akiwa mwanafunzi alishiriki katika maandamano dhidi ya Shah anayeungwa mkono na nchi za Magharibi, ambaye hatimaye alipinduliwa mwaka 1979 katika Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Ayatollah Ruhollah Khomeini.

Baada ya mapinduzi hayo alijiunga na idara ya mahakama na kuhudumu kama mwendesha mashtaka katika miji kadhaa huku akifunzwa na Ayatollah Khamenei, ambaye alikua rais wa Iran mwaka 1981.

Uhusiano na 'kamati ya kifo' ya Iran

Bw Raisi alikua naibu mwendesha mashtaka mjini Tehran akiwa na umri wa miaka 25 pekee.

Akiwa katika nafasi hiyo aliwahi kuwa mmoja wa majaji wanne waliokaa kwenye mahakama za siri zilizoanzishwa mwaka 1988 zilizokuja kujulikana kwa jina la “Kamati ya Kifo”.

Mahakama hizo "ziliendesha upya kesi " za maelfu ya wafungwa ambao tayari wanatumikia vifungo kwa shughuli zao za kisiasa. Wengi wao walikuwa wanachama wa kundi la upinzani la mrengo wa kushoto Mujahedin-e Khalq (MEK), ambalo pia linajulikana kama People's Mujahedin Organization of Iran (PMOI).

g

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanaharakati wa upinzani wa Iran waliadhimisha kumbukumbu ya waathiriwa walionyongwa Paris mnamo 2019
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Idadi kamili ya waliohukumiwa kifo na mahakama hiyo haijajulikana, lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema takriban wanaume na wanawake 5,000 waliuawa na kuzikwa katika makaburi ya halaiki ambayo hayakujulikana katika kile kilichokuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu hawakanushi kwamba mauaji hayo yalitokea, lakini hawajadili maelezo na uhalali wa kesi za kila mtu binafsi aliyenyongwa.

Bw Raisi amekanusha mara kwa mara jukumu lake katika hukumu za kifo. Lakini pia amesema walihalalishwa kwa sababu ya fatwa, au uamuzi wa kidini, wa Ayatollah Khomeini.

Mnamo 2016, kanda ya sauti ya mkutano wa 1988 kati ya Bw Raisi, wanachama wengine kadhaa wa mahakama na kisha Naibu Kiongozi Mkuu Ayatollah Hossein Ali Montazeri (1922-2009) iligundulika kimakosa.

Katika kanda hiyo, Montazeri anasikika akielezea mauaji hayo kama "uhalifu mkubwa zaidi katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu". Mwaka mmoja baadaye Montazeri alipoteza nafasi yake kama mrithi aliyeteuliwa wa Khomeini na Ayatollah Khamenei akawa Kiongozi Mkuu baada ya kifo cha Khomeini.

Alipoulizwa mnamo 2021 kuhusu jukumu lake katika mauaji ya halaiki, Bw Raisi aliwaambia waandishi wa habari: "Ikiwa hakimu, mwendesha mashtaka, ametetea usalama wa watu, anapaswa kusifiwa ... Ninajivunia kutetea haki za binadamu katika kila nafasi niliyoshikilia hadi sasa."

Matarajio yasiyowezekana ya urais

Mnamo 2017, Bw Raisi aliwashangaza waangalizi kwa kugombea urais.

Kiongozi mwenzake, Bw Rouhani, alishinda muhula wa pili kwa kishindo katika duru ya kwanza ya uchaguzi, akipata asilimia 57 ya kura. Bw Raisi, ambaye alijidhihirisha kama mpiganaji wa kupambana na ufisadi lakini akashtumiwa na rais kwa kutofanya juhudi za kutosha kukabiliana na ufisadi kama naibu mkuu wa mahakama, aliibuka wa pili kwa 38%.

Hasara hiyo haikuharibu sifa ya Bw Raisi na mwaka wa 2019 Ayatollah Khamenei alimteua katika wadhifa mkubwa wa mkuu wa idara ya mahakama.

Wiki iliyofuata, alichaguliwa pia kama naibu mwenyekiti wa Bunge la Wataalamu, baraza la viongozi wa dini ya Kiislamu lenye wanachama 88 lililowajibika kumchagua Kiongozi Mkuu ajaye.

Akiwa mkuu wa idara ya mahakama, Bw Raisi alitekeleza mageuzi yaliyosababisha kupunguzwa kwa idadi ya watu waliohukumiwa kifo na kunyongwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya nchini humo. Hata hivyo, Iran iliendelea kuwaua watu wengi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote duniani isipokuwa China.

Idara ya mahakama pia iliendelea kufanya kazi na vyombo vya usalama ili kukabiliana na wapinzani na kuwafungulia mashtaka Wairani wengi wenye uraia wa nchi mbili au ukaaji wa kudumu wa mataifa ya kigeni kwa tuhuma za ujasusi.

Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alimwekea vikwazo Bw Raisi kwa sababu ya rekodi yake ya haki za binadamu mwaka wa 2019.

Alishtakiwa kwa kuwa kiongozi aliyesimamia mauaji ya watu waliokuwa vijana waliodaiwa kuwa wahalifu, na kuhusika katika kamata kamata ya watu iliyogubikwa na ghasia. juu ya dhidi ya watu waliofanya maandamano ya chama cha upinzani cha Green Movement baada ya uchaguzi wa rais uliokumbwa na utata mwaka 2009.

h

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Bw Raisi alijidhihirisha kama mpiganaji dhidi ya ufisadi katika mikutano ya kampeni kabla ya uchaguzi wa urais wa 2021.

Bw Raisi alipotangaza kuwania urais katika uchaguzi wa 2021, alitangaza kwamba "alikuja kama mtu huru jukwaani kufanya mabadiliko katika usimamizi mkuu wa nchi na kupambana na umaskini, ufisadi, udhalilishaji na ubaguzi".

Uchaguzi uliingia dosari baadaye wakati Baraza la Walinzi lenye misimamo mikali lilipowaondoa wagombeaji kadhaa mashuhuri wenye msimamo wa wastani na wapenda mabadiliko. Wapinzani na baadhi ya wafuasi wa mageuzi waliwataka wapiga kura kususia uchaguzi huo, wakilalamika kuwa mchakato huo umebuniwa ili kuhakikisha Bw Raisi hakabiliwi na ushindani wowote.

Alipata ushindi mnono, akishinda 62% ya kura katika duru ya kwanza. Lakini, waliojitokeza walikuwa chini ya 49% - ikiwa ni rekodi ya chini kwa uchaguzi wa rais tangu mapinduzi ya 1979.

Alipoanza muhula wake wa miaka minne mwezi huo wa Agosti, Bw Raisi aliahidi "kuboresha uchumi ili kutatua matatizo ya taifa" na "kuunga mkono mpango wowote wa kidiplomasia" ambao ulisababisha kuondolewa kwa vikwazo.

Alikuwa akirejelea mazungumzo ambayo yamekwama kwa muda mrefu jkuhusu kufufuliwa kwa makubaliano ya 2015 yanayozuia shughuli za nyuklia za Iran, ambayo yamekaribia kuporomoka tangu serikali ya Trump ilipoachana nayo na kurudisha vikwazo vya kiuchumi vya Marekani mnamo 2018. Tangu wakati huo Iran imelipiza kisasi kwa kuzidi kukiuka vikwazo.

Bw Raisi pia aliahidi kuboresha uhusiano na majirani wa Iran wakati huo huo akitetea shughuli zake za kikanda, akizitaja kuwa "nguvu ya kuleta utulivu".

Makubaliano na Marekani kuhusu kufufua mapatano ya nyuklia yaliripotiwa kukaribia kufikiwa Agosti 2022, licha ya msimamo mkali wa Bw Raisi katika mazungumzo hayo. Hata hivyo, juhudi hizo zilipitwa na wakati kutokana na matukio nchini Iran.

Kutikiswa na maandamano dhidi ya serikali

Mwezi huo wa Septemba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitikiswa na maandamano makubwa ya kudai kukomeshwa kwa utawala wa viongozi wa kidini.

Vuguvugu la "Mwanamke, Maisha, Uhuru" ( "Woman, Life, Freedom") lilisababisha kifo cha Mahsa Amini, msichana ambaye alikuwa amezuiliwa na polisi wa maadili mjini Tehran kwa madai ya kuvaa hijabu "isivyofaa".

Mamlaka zilikanusha kuwa alidhulumiwa, lakini ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa uligundua kuwa "alifanyiwa ukatili wa kimwili ambao ulisababisha kifo chake".

g

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Zaidi ya mwaka mmoja tu baada ya Bw Raisi kuwa rais, Iran ilitikiswa na maandamano yaliyoongozwa na wanawake dhidi ya utawala wa viongozi wa kidini

Bw Raisi aliapa "kushughulikia kwa uthabiti" machafuko hayo na mamlaka zinazowakadamiza kwa nguvu. Hawajatoa idadi rasmi ya vifo, lakini ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulisema takwimu za kuaminika zilionyesha kuwa waandamanaji 551 waliuawa na vikosi vya usalama, wengi wao kwa risasi. Serikali inasema maafisa wa usalama 75 waliuawa.

Zaidi ya waandamanaji wengine 20,000 waliripotiwa kuzuiliwa na vijana tisa waandamanaji waliuawa baada ya kile ujumbe wa Umoja wa Mataifa uligundua kuwa ni kesi za pamoja ambazo washtakiwa walilazimishwa kukiri makosa baada ya kuteswa.

Ingawa maandamano hatimaye yalipungua, kuliendelea kuwa na kutoridhika kwa watu wengi na utawala wa viongozi wa kidini na sheria za hijabu. Wanawake na wasichana wengi kwa dharau waliacha kufunika nywele zao hadharani - kitendo ambacho bunge la Iran na Bw Raisi walitaka kukabiliana nacho kwa sheria mpya na kuwakamata upya wahusika.

Kuongezeka kwa mvutano wa kikanda

Mnamo Machi 2023, serikali yake ilikubali maelewano ya kushangaza na mpinzani mkali wa Iran, mamlaka ya kieneo ya Sunni Saudi Arabia, miaka saba baada ya kuvunja uhusiano wa kidiplomasia.

Lakini mvutano wa kikanda uliongezeka mnamo Oktoba wakati Hamas ilipofanya shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kushuhudiwa katika eneo la kusini mwa Israel,na Israel ikajibu kwa kuanzisha kampeni kubwa ya kijeshi huko Gaza.

Wakati huo huo, mtandao wa Iran wa makundi washirika yenye silaha na washirika wanaofanya kazi katika Mashariki ya Kati - ikiwa ni pamoja na Hezbollah nchini Lebanon, Wahouthi nchini Yemen, na wanamgambo mbalimbali nchini Iraq na Syria - walizidisha kwa kiasi kikubwa mashambulizi yao dhidi ya Israeli katika kile walichosema kuwa maandamano ya mshikamano na Wapalestina.

Hofu ya kwamba ongezeko hilo la vita hilo lingezua vita vya eneo hilo iliongezeka mwezi Aprili, baada ya Iran kufanya shambulio la kwanza la kijeshi la moja kwa moja dhidi ya Israel.

Raisi aliunga mkono uamuzi wa kurusha zaidi ya ndege 300 zisizo na rubani na makombora dhidi ya Israel kulipiza kisasi shambulio baya dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria. Takriban wote walipigwa risasi na Israel, washirika wa Magharibi na washirika wa Kiarabu na kambi ya anga kusini mwa Israel ilipata uharibifu mdogo tu ilipopigwa.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Bw Raisi alisema shambulizi la moja kwa moja la Iran la kombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel mwezi wa Aprili lilionyesha "azma yake ya ajabu"

Israel ilijibu kwa kurusha kombora lililopiga kambi ya anga ya Iran kufuatia wito wa Magharibi wa kuzitaka pande husika kujizuia.

Bw Raisi alipuuzilia mbali umuhimu wa shambulio hilo na kusema shambulio la kombora la Iran na ndege zisizo na rubani "lilionyesha dhamira ya dhati ya taifa letu".

Siku ya Jumapili, saa chache kabla ya helikopta yake kuanguka kaskazini-magharibi mwa Iran, Bw Raisi alisisitiza uungaji mkono wa Iran kwa Wapalestina, akitangaza kwamba "Palestina ni suala la kwanza la ulimwengu wa Kiislamu".

Ni machache yanayojulikana kuhusu maisha ya kibinafsi ya Bw Raisi isipokuwa kwamba mkewe, Jamileh, anafundisha katika Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti huko Tehran, na kwamba wana binti wawili watu wazima. Baba mkwe wake ni Ayatollah Ahmad Alamolho, ni Imam katika Mashhad.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi