Hospitali ya Gaza 'yatandazwa' huku kisasi cha Israel kikiwaua na kuwajeruhi mamia
Na Rushdi Abu Alouf
BBC News, Gaza

Chanzo cha picha, EPA
Siku ya Jumamosi asubuhi, watu wa Gaza walisherehekea baada ya Hamas kurusha maelfu ya maroketi hadi Israel na kuanzisha mashambulizi makali ya kuvuka mpaka.
Siku moja baadaye, picha ilikuwa tofauti sana.
Baada ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel, watu walikuwa wakikaa ndani ya nyumba. Milipuko iliendelea Jumapili nzima.
Sauti hiyo ilikuwa ya kutisha. Mawingu ya moshi mweusi yalitanda majengo katika Ukanda wa Gaza.
Jeshi la Israel linasema kuwa limepiga shabaha zaidi ya 1,000 huko Gaza. Hizi ni pamoja na ngome za kijeshi, nyumba za viongozi wa Hamas, pamoja na benki zinazoendeshwa na kundi hilo la wanamgambo.
Moja ya mashambulio muhimu zaidi ya Israeli Jumapili asubuhi yalilenga Mnara wa Watan, ambao unatumika kama kitovu cha watoa huduma za mtandao huko Gaza.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maafisa wa afya wa Palestina wanasema zaidi ya watu 400 wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya anga ya Israel huko Gaza.
Maeneo mengi hayana umeme kwani Israel imeacha kusambaza umeme Gaza. Msambazaji mwenyewe wa Gaza anaweza tu kutoa 20% ya umeme unaohitajika.
Usambazaji wa chakula na maji pia umekatwa.
Nikiendesha gari katikati ya jiji la Gaza Jumapili asubuhi, niliona vifusi vikiwa vimeziba barabara. Maduka yalifungwa, isipokuwa viwanda vichache vya mikate ambapo foleni ndefu zilikuwa zimeundwa.
Kuongezeka huko kumeifanya hali mbaya ya kibinadamu ya Gaza kuwa mbaya zaidi.
Hospitali zake zisizo na vifaa - ambazo kwa nyakati bora zinatatizika kutoa huduma ya afya kwa wakazi zaidi ya milioni mbili - zimezindua wito wa kukata tamaa kwa wafadhili wa damu.
Mahmoud Shalabi, mkurugenzi wa Gaza wa shirika la misaada la Medical Aid kwa Wapalestina, alielezea hospitali kuu ya mji huo kama "machinjio".
Watu wengi walikuwa wamelala chini katika idara ya dharura, alisema. "Kulikuwa na maiti nyingi katika chumba cha kuhifadhia maiti na wafanyikazi wengi wa matibabu hawakuweza kukabiliana na wimbi kubwa la majeruhi waliokuwa wakipokea," Bw Shalabi aliongeza.
Baadaye siku ya Jumapili, wakaazi katika sehemu moja ya Jiji la Gaza walipokea jumbe za SMS kutoka kwa jeshi la Israel likiwashauri kwenda kujihifadhi kabla ya mashambulizi.
Zaidi ya watu 20,000 walifika maeneo ya Umoja wa Mataifa katika eneo hilo, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa aliambia BBC.
Hamas, ambayo imeidhibiti Gaza kwa muda wa miaka 17 iliyopita, inajua madhara ya kuishambulia Israel - hivyo lazima ilikuwa ikitarajia mashambulizi hayo makubwa ya kulipiza kisasi.
Kundi linaloungwa mkono na Iran limeweka wazi kuwa liko tayari kwa vita na Israel. Hamas imesema imekuwa ikisafirisha silaha kinyume cha sheria licha ya mzingiro wa Israel na Misri na kutengeneza silaha zake.
Kundi hilo limeapa kuendeleza kile linachokiita "mashambulizi ya kulipiza kisasi". Baada ya kukomeshwa siku ya Jumamosi usiku, ilisema ilikuwa imerusha makombora 100 katika mji wa Sderot kusini mwa Israel.
Wananchi wa kawaida wa Gaza wametoa hisia tofauti kuhusu mzozo huu ambao haujawahi kutokea. Ingawa wengine waliona mashambulizi ya roketi ya Hamas kama sababu ya kusherehekea, wengi wana wasiwasi kwamba ghasia hizo zitaendelea kwa muda mrefu sana.













