Unayajua majukumu ya Mfalme na nafasi yake katika familia ya kifalme?

Charlses

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Jennifer Clarke
    • Nafasi, BBC News

Siku ya Jumamosi tarehe 6 Mei, 2023 Mfalme Charles III atakuwa rasmi mfalme wa 40 wa Uingereza kutawazwa huko Westminster Abbey.

Anachukua ufalme kufuatia kifo cha mama yake, Elizabeth II, mnamo Septemba 2022.

Nini majukumu ya Mfalme?

Mfalme ndiye kiongozi mkuu wa Uingereza. Hata hivyo, nguvu zake ni za kiishara na ni za sherehe, na haegemee upande wowote wa kisiasa.

Anapokea taarifa kila siku kutoka Serikalini kupitia sanduku nyekundu la ngozi, ikiwa ni pamoja na maelezo mafupi kabla ya mikutano muhimu, au nyaraka zinazohitaji saini yake.

Waziri mkuu kawaida hukutana na Mfalme siku ya Jumatano katika Jumba la Buckingham, ili kumjulisha juu ya maswala mbalimbali ya serikali.

Mikutano hii ni ya faragha kabisa na hakuna rekodi rasmi ya kile kinachozungumzwa.

King Charles shaking the hand of incoming Prime Minister Rishi Sunak

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mfalme Charles akiwa na Rishi Sunak, waziri mkuu wa pili tangu Charles amrithi mama yake

Mfalme ana majukumu mengine kadhaa na rasmi ya kibunge:

  • Kuteua serikali - kiongozi wa chama kinachoshinda uchaguzi mkuu kwa kawaida huitwa kwenye kasri la Mfalme la Buckingham, ambako wanaalikwa kwenda kuunda serikali. Mfalme pia anajukumu la kuvunja rasmi serikali kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.
  • Ufunguzi wa bunge na Hotuba ya Mfalme - Mfalme huanza mwaka wa bunge na sherehe ya Ufunguzi wa taifa, ambapo anaweka wazi mipango ya serikali, katika hotuba maalumu kutoka kwa kiti cha enzi.
  • Idhini ya Kifalme - wakati sheria au marekebisho yaake yanapitishwa kupitia Bunge, lazima kiidhinishwe rasmi na Mfalme ili kuwa sheria. Mara ya mwisho Uidhinishaji wa Kifalme ulikataliwa ilikuwa mnamo mwaka 1708.

Kwa kuongezea, mfalme anaongoza hafla ya kumbukumbu ya kila mwaka mnamo Novemba kwenye Cenotaph huko London.

Mfalme pia huwa anakutana na kukaribisha wakuu wa nchi wageni - amefanya hivyo hivi karibuni alipomkaribisha Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa - na mara kwa mara hukutana na mabalozi wa kigeni na makamishna wakuu walioko Uingereza.

Ziara yake ya kwanza ya kiserikali, Mfalme Charles alitembelea Ujerumani, ambapo akawa mfalme wa kwanza wa Uingereza kuhutubia bunge la Ujerumani.

Mfalme pia ni mkuu wa Jumuiya ya Madola, muungano wa nchi huru 56 zenye watu bilioni 2.5 - na mkuu wa nchi wa nchi 14 kati ya hizi, zinazojulikana kama ulimwengu wa Jumuiya ya Madola.

South Africa's President, Cyril Ramaphosa, King Charles and Camilla, Queen Consort

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mfalme na mkewe Camilla pamoja na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa

Camilla, mkewe ambaye ni Malkia mfariji, anamsaidia na kumuunga mkono Mfalme katika kutekeleza majukumu yake na anajishughulisha na umma kwa niaba ya mashirika 90 ya misaada anayounga mkono.

Mengi ya haya yanajielekeza kwenye kusaidia masuala ya afya na ustawi wa jamii na kufanya kazi na watu ambao wamepatwa na madhara kama ubakaji, kunyanyaswa au kushambuliwa kingono.

Nini kinafanyika wakati wa kutawazwa kwakwe kuwa Mfalme?

Wakati wa sherehe hizo huko Westminster Abbey, Mfalme atavikwa taji pamoja na mkewe, Camilla.

Kutawazwa ni ibada ya kidini ya Kianglikana, inayofanywa na Askofu Mkuu wa Canterbury. Mfalme anapakwa "mafuta matakatifu", na anapokea 'orb' na fimbo, ambavyo ni ishara za kifalme.

Katika kilele cha sherehe hiyo, Askofu Mkuu ataweka Taji la St Edward juu ya kichwa cha Charles - taji lenye thamani thabiti ya dhahabu, na la kitambo tangu mwaka 1661.

St Edward's Crown

Chanzo cha picha, Reuters

Hiki ndicho kitovu cha mataji ya vito ambayo huvaliwa na mfalme tu wakati wa kutawazwa kwakwe.

Tofauti na harusi za kifalme, kutawazwa ni tukio la serikali - serikali inalipia gharama, na pia huwa na maamuzi kuhusu orodha ya wageni watakaohudhuria.

Familia ya Kifalme inaundwa na kina nani wengine?

Members of the Royal Family on the Queen's official birthday

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Wana familia ya Familia ya Kifalme wakisherehekea siku ya kuzaliwa rasmi ya Malkia Elizabeth II katika Jumba la Buckingham, ilikuwa mwaka 2019 wakati wa uhai wake.
  • Mwanamfalme au Prince William ni mtoto mkubwa wa Mfalme Charles na mke wake wa kwanza, marehemu Princess Diana. Baada ya kifo cha Malkia, alikua Mkuu wa Wales na Duke wa Cornwall huku akiendelea kuwa Duke wa Cambridge. Amemuoa Catherine, Princess wa Wales na Duchess wa Cornwall na Cambridge. Wana watoto watatu: Prince George, Princess Charlotte na Prince Louis
  • Binti mfalme (Anne) alikuwa mtoto wa pili wa Malkia Elizabethi II na binti yake pekee. Ameolewa na Timothy Laurence. Ana watoto wawili aliozaa na mume wake wa kwanza, Kapteni Mark Phillips: Peter Phillips na Zara Tindall
  • Duke wa Edinburgh (Prince Edward) alikuwa mtoto wa mwisho wa Malkia. Amefunga ndoa na Duchess wa Edinburgh (Sophie Rhys-Jones). Wana watoto wawili: Lady Louise Windsor na Earl wa Wessex (James Mountbatten-Windsor)
  • Duke wa York (Prince Andrew) alikuwa mtoto wa pili wa Malkia. Ana binti wawili na mke wake wa zamani, Duchess wa York (Sarah Ferguson): Princess Beatrice na Princess Eugenie. Prince Andrew alijiuzulu "kazi za kifalme" mnamo 2019 baada ya mahojiano yenye utata ya BBC Newsnight kuhusu madai kwamba alikuwa amemnyanyasa kingono Virginia Giuffre. Mnamo Februari 2022, alilipa kiasi ambacho hakikujulikana ili kusaka suluhu ya kesi ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo Bi Guiffre alifungua dhidi yake nchini Marekani.
  • Duke wa Sussex (Prince Harry) ni mdogo wake William. Amemuoa Duchess wa Sussex (Meghan Markle). Wana watoto wawili: Prince Archie na Princess Lilibet. Mnamo 2020, walitangaza kuwa wanajiweka kando kama washiriki wa familia ya kifalme na kuhamia huko California

Urithi wa kimamlaka hufanyaje kazi?

Utaratibu wa urithi linaweka wazi ni mwanachama gani wa Familia ya Kifalme atachukua kama mfalme wakati aliyepo anakufa au kujiuzulu. Wa kwanza katika mstari - mrithi wa kiti cha enzi - ni mtoto mkubwa wa mfalme.

Sheria za urithi wa kifalme zilirekebishwa mwaka wa 2013 ili kuhakikisha kwamba wana hawatatanguliza tena dada zao wakubwa.

Mrithi wa Mfalme Charles ni mtoto wake mkubwa, Mkuu wa Wales.

Mtoto mkubwa wa William, Prince George, ni wa pili katika kiti cha enzi, na binti yake Princess Charlotte ni wa tatu. Prince Louis ni wa nne na Prince Harry wa tano.

h

Familia ya Kifalme ina umaarufu gani?

Ili kuangalia umma inavyotazama umaarufu wake kabla ya kutawazwa, kipindi cha BBC Panorama kiliendesha kura mpya ya maoni ya YouGov.

Matokeo yanaonyesha kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa kwa kudumisha utawala wa kifalme, huku 58% wakiunga mkono utawala wa kifalme kuliko mkuu wa nchi aliyechaguliwa - ambao uliungwa mkono na asilimia 26% tu.

B

Lakini, kwa takwimu zaidi, kura hiyo ya maoni imeonyesha mitazamo inavyotofautiana kutokana na umri. Kwa vijana utawala wa kifalme unaonekana kutowavutia.

Watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65s walionekana kuunga mkono ufalme kwa 78%, wenye umri wa miaka 18-24 walionekana hawauungi mkono kwa kiasi kikubwa.

Ni 32% tu waliounga mkono utawala wa kifalme. Kundi hili changa lilikuwa na uwezekano zaidi, kwa 38%, kupendelea mkuu wa nchi aliyechaguliwa, ingawa 30% iliyobaki walisema hawajui.

Kutojali kunaweza kuwa suala kama kupinga, na 78% ya vijana wanasema "hawapendezwi" na Familia ya Kifalme.

Familia ya Kifalme inaishi wapi?

Mfalme Charles na Camilla, Malkia mfariji, wanaishi katika kasri la Buckingham. Huko nyuma waliwahi kuishi Clarence House huko London na Highgrove huko Gloucestershire.

Makao mengine ya Kifalme ni pamoja na Windsor Castle, Sandringham, huko Norfolk, Ikulu ya Holyroodhouse, huko Edinburgh, na Ngome ya Balmoral, huko Aberdeenshire.

Mnamo Agosti 2022, Prince na Princess wa Wales walihama kutoka kasri la Kensington magharibi mwa London na kuishi Adelaide Cottage, Windsor Estate.

Prince George, the Princess of Wales, Prince Louis, the Prince of Wales and Princess Charlotte walking hand-in-hand on the children's first day at Lambrook School

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Prince na Princess wa Wales, wakiwa na watoto wao katika siku yao ya kwanza katika Shule ya Lambrook huko Berkshire