Vita vya Gaza: 'Wanangu hawaniachilii wakiogopa mbwa wanaovamia makaburi ya Rafah yaliyopo karibu na makazi yetu'

Na Fergal Keane,

Mwandishi maalum, Jerusalem

g
Maelezo ya picha, "Sikubali mimi au watoto wangu tuishi karibu na makaburi," anasema Rehab Abu Daqqa.

Watoto wanasikia mbwa wakibweka nje karibu na hema lao dhaifu la plastiki.

Watoto saba wa Rehab Abu Daqqa wakiwa wamemzunguka mama yao. Ni eneo la mwisho salama katika maisha yao. Watoto hawa wameshuhudia mambo mengi na mama yao ambayo hayawezi kusimuliwa kwa wale ambao hawajaona vitu walivyoona. Je, kuna neno la kueleza kile mtoto anahisi akijua kwamba umbali wa yadi chache tu, wanyama wanavuta miili kutoka kaburini?

Maisha ya utotoni hayapo kwa watoto hawa kutokana na hali ya kutisha ya makaburi haya ya dharura huko Rafah.

Hofu ni neno analotumia Rehab Abu Daqqa.

ONYO: Ripoti hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kupata kuwa ya kutatiza

Hili ni sahihi. Lakini kuna zaidi ya hayo. Watoto wameona mbwa wakila miili. Mguu wa binadamu umelazwa karibu na uzio. Kwa hivyo ndio wanaogopa. Lakini pia, hawaelewi. Watoto ambao hapo awali walikuwa na nyumba, walienda shule, wakiishi kulingana na utaratibu ulioanzishwa ya familia zao na jamii, sasa ni wakimbizi katika sehemu ambayo wanakaribia kifo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Leo asubuhi mbwa walitoa mwili kutoka kwenye moja ya kaburi na walikuwa wanaula," Rehab Abu Daqqa anasema. "Kuanzia usiku hadi alfajiri mbwa hawaturuhusu kulala ... watoto wangu wanaendelea kunishikilia kwa sababu ya jinsi wanavyoogopa."

Mbwa huja katika makundi ya makumi kadhaa. Wanyama ambao kawaida hufuhgwa nyumbani ambao wamiliki wao wamekufa au wamehamishwa makazi yao, waliochanganyika na idadi ya watu waliopotea wa Rafah, wote kwa sasa ni wanyama pori na wanatafuta chochote wanachoweza kula.

Eneo hilo la Makaburi lina makaburi mengi ya kina kifupi ambapo watu huweka wafu wao hadi wakati utakapofika ambapo wanaweza kupelekwa nyumbani kwao. Katika baadhi ya makaburi jamaa wameweka matofali ili kujaribu kuwazuia mbwa kuwafikia wafu.

Rehab Abu Daqqa amedhoofika na amechoka. Mdomo na pua yake vimefunikwa na kitambaa ili kujikinga na uvundo wa makaburi. Anawasifu vijana waliokuja mapema kurudisha mwili uliokokotwa asubuhi hiyo.

“Sikubali mimi au watoto wangu tukae karibu na makaburi, mtoto wangu yuko darasa la 3 na leo badala ya kucheza mchezo anachora kaburi na katikati yake alichora maiti. Wtoto wa Palestina… Naweza kukuambia nini ni dhiki , neno huzuni halielezei hata kidogo hali halisi''.

Makaburi hayo ni mojawapo ya maeneo kadhaa ya Gaza ambayo yamekuwa kimbilio la watu ambao nyumba zao zimeharibiwa katika mapigano hayo.

Kuna zaidi ya watu milioni 1.4 waliosongamana mjini Rafah - mara tano ya idadi yake ya kabla ya vita.

Kulingana na Baraza la Wakimbizi la Norway ambalo linawashughulikia watu 22,000 kwa kila kilomita ya mraba. Tayari maonjwa yanaenea huku kukiwa na milipuko ya kuhara, hepatitis A, na homa ya uti wa mgongo - pamoja na njaa inayoendelea.

Rafah ni mahali ambapo wakimbizi wa Gaza wanaufikia ukuta wa mwisho, mpaka na Misri ambao umefungwa kwa idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao.

Wanawasili baada ya kusukumwa kutoka sehemu moja hadi nyingine na kusonga mbele kwa majeshi ya Israel.

Huena Rehab akalazimika kukimbia na familia yake tena ikiwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litaendelea na mashambulizi dhidi ya Rafah.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema operesheni ya kijeshi huko Rafah itaendelea iwe "kwa au bila" kusitisha mapigano ili kuharibu kile anachosema kuwa ni vikosi vinne vya Hamas katika mji huo.

Hamas inasisitiza kuwa hakuwezi kuwa na mpango wowote bila kujitolea kumaliza vita hivyo. Wanachama wa mrengo kulia kabisa wa baraza la mawaziri la muungano wa Israel wanamuonya Bw Netanyahu dhidi ya kufikia maelewano na Hamas.

Waziri wa Fedha, Bezalel Smotrich, ambaye ndiye anayesimamia viwango vya vuguvugu la walowezi, ametoa wito wa "uharibifu kabisa" huko Rafah, akisema hakuwezi kuwa na "kazi nusu".

"Je, [wakimbizi] wanahamia wapi?" anauliza Dk Rik Peeperkorn, mkurugenzi wa kikanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ambaye alirejea hivi karibuni kutoka Rafah.

f
Maelezo ya picha, Dk Rik Peeperkorn kutoka WHO anaonya kwamba mashambulizi huko Rafah yatasababisha maafa mengine ya kibinadamu juu ya yaliyopo.

"Tayari tuna tatizo katika afya. Tuna shitatizo la maji na usafi wa mazingira, tatizo la chakula. Kuna janga la kibinadamu. Kwa hivyo, kutakuwa na maafa mengine ya kibinadamu juu ya haya ... Tunachotarajia itakuwa vifo vya ziada na magonjwa wakati uvamizi wa kijeshi unatokea, kwa hivyo, watu wengi zaidi wanakufa… vifo vingi zaidi na magonjwa mengi zaidi.

Dk Peeperkorn alifanya kazi kwa miaka saba nchini Afghanistan na Umoja wa Mataifa na si mtu ambaye ni rahisi kuogopa. Lakini tulipokutana Jerusalemu alionekana amechoka. Uchovu wa mtu anayeamka kila asubuhi kwa uhakika wa matatizo ambayo yanaonekana kutishia kuleta matokeo mabaya zaidi.

WHO tayari inatayarisha hospitali za ziada kusaidia ikiwa watu watalazimika kuhama. Lakini ni nini kinatokea kwa wagonjwa mahututi na wazee, wagonjwa 700 wa kusafishwa kwa figo ambao kwa sasa wanatibiwa katika kituo ambacho hapo awali kilihudumia 50?

"Ukiangalia sekta yetu ya afya, tayari imeharibika na uvamizi utamaanisha kwamba tunapoteza hospitali nyingine tatu ... kama haziwezi kufikiwa, zinaweza kuharibika, zinaweza kuharibiwa kwa kiasi."

g
Maelezo ya picha, Mvulana akipokea matibabu katika Hospitali ya Ulaya huko Rafah

Wenzangu wa BBC wametoa ushahidi wa wazi wa hali ndani ya hospitali, wakipiga picha siku baada ya siku katika muda wote wa vita.

Katika Hospitali ya Ulaya huko Rafah familia zimepiga kambi katika nafasi yoyote wanayoweza kupata, katika uwanja na ndani. Wanatayarisha chakula katika wodi.

Watoto wao wanazurura kando ya korido zenye giza, wakiwaona majeruhi wakiendeshwa kwenye troli, mwanamke mzee ameketi peke yake akitazama kwa mbali.

Katika wodi ya huduma ya dharura, Yassin al Ghalban mwenye umri wa miaka 11 analia kitandani mwake. Hana miguu, imekatwa chini ya goti baada ya mashambulio ya anga. Jamaa aliyesimama karibu na kitanda anasema, "anaishi kwa dawa za kutuliza maumivu".

g
Maelezo ya picha, Yassin al Ghalban mwenye umri wa miaka 11 amelazwa katika kitanda cha hospitali katika Hospitali ya Ulaya iliyopo Rafah

Kwenye makaburi, Rehab Abu Daqqa anawatazama watoto wake wakicheza yadi chache kutoka makaburini.

Mbwa wamekwenda lakini watoto wanakaa karibu na mama yao. Hivi karibuni atakuwa kwenye safari tena kwasababu hawezi kuvumilia watoto wake kukaa mahali hapa.

Hakuna mazungumzo ya matumaini hapa. Tumaini huko Gaza huondoka kwa kasi tofauti kulingana na hali yako. Matumiani yanaweza kutoweka kwa sekunde moja na kutokana na mauaji ya mpendwa. Au yanaweza kuondoka mara kwa mara, saa baada ya saa, unapofurushwa kutoka kambi moja chafu hadi nyingine, na unakosa la kusema kutokana na maswali yasiyoisha kutoka kwa watoto.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi