Ombi la baba kuhusu watoto wanaokabiliwa na njaa Gaza baada ya mtoto wake kufariki kutokana na utapiamlo

"Nini hatma ya watoto wanaokumbwa na njaa? Je, watapata wa kuwaokoa au watakufa? Mtoto wangu Ali amekwisha kufa."
Baba yake Ali, mtoto mchanga wa Kipalestina ambaye alifariki hivi karibuni kwa utapiamlo na upungufu wa maji mwilini katika hospitali pekee ya watoto iliyo kaskazini mwa Gaza, ameomba msaada kwa watoto wengine wanaotibiwa huko, huku Umoja wa Mataifa ukionya juu ya njaa ikiwa misaada inayotolewa haitaongezeka kwa kiasi kikubwa.
"Ali alizaliwa wakati wa vita na hakukuwa na chakula au chochote kwa mama yake, jambo ambalo lilisababisha figo zake kushindwa kufanya kazi," mwanamume huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema katika mahojiano yaliyorekodiwa na Gaza Lifeline ya BBC Arabic.
"Maisha ya Ali yalizidi kuwa mabaya siku baada ya siku. Tulijaribu kumpeleka kutibiwa hospitalini, lakini hapakuwa na msaada... Ali alikufa mbele ya ulimwengu mzima, ambao uliendelea kumtazama akifariki."
Cha kusikitisha ni kwamba, Ali alikuwa ni mmoja tu wa watoto wasiopungua 10 ambao timu ya Shirika la Afya Ulimwenguni ilisema walifariki kutokana na ukosefu wa chakula katika hospitali ya Kamal Adwan iliyozidiwa katika mji wa Beit Lahia, kufuatia ziara yake mwishoni mwa juma.
Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imeripoti vifo vya watoto 18 kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini katika eneo hilo tangu wiki iliyopita, na angalau 15 vikitokea Kamal Adwan.
Pia imeelezea hofu kwa watoto sita wachanga ambao ilisema walikuwa wakitibiwa utapiamlo katika hospitali hiyo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, limeonya kwamba idadi ya watoto wanaokufa kwa njaa huenda ikaongezeka kwa kasi ikiwa vita kati ya Israel na Hamas havitamalizika na vikwazo vya misaada ya kibinadamu vitatuliwe mara moja.
Wizara ya afya ya Gaza inasema watoto na wanawake ni asilimia 70 ya zaidi ya watu 30,700 waliouawa na wengine 72,000 kujeruhiwa katika eneo hilo tangu kuanza kwa vita.
Jeshi la Israel lilianzisha kampeni ya anga na ardhini huko Gaza baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo karibu watu 1,200 wengi wao wakiwa raia, waliuawa na wengine 253 walichukuliwa mateka.
Takribani watu 300,000 kwa sasa wametengwa kaskazini mwa Gaza, ambapo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linasema njaa imefikia kiwango cha maafa kwa sababu ni misaada michache tu imeweza kupita.
Uchunguzi wa utapiamlo uliofanywa huko na mashirika ya Umoja wa Mataifa mwezi Januari uligundua kuwa mtoto mmoja kati ya sita chini ya umri wa miaka miwili alikuwa na utapiamlo. Kati ya watoto hao, karibu asilimia 3 walikuwa wanakabiliwa na uharibifu mkubwa na kuhitaji matibabu ya haraka.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ukosefu wa chakula chenye lishe bora, maji salama na huduma za matibabu, pamoja na uchovu na kiwewe kinachosababishwa na mzozo huo, pia kunazuia uwezo wa akina mama kunyonyesha watoto wao. Bila maziwa ya mama au fomula, ugavi wake ambao unaripotiwa kuwa karibu haupo kaskazini,watoto wanaweza kukosa maji mwilini kwa haraka na utapiamlo, ambayo huongeza hatari ya hali ya kutishia maisha kama vile kufeli kwa figo.
Dk Samia Abdel Jalil, ambaye anafanya kazi katika kitengo cha wagonjwa mahututi cha Kamal Adwan, alisema katika mahojiano na Gaza Lifeline kwamba mtoto mchanga na dadake mkubwa walikufa hospitalini ndani ya siku chache mmoja baada ya mwingine.
"Tulikuwa na ugumu wa kupata maziwa kwa idara nzima na sio tu kwa msichana huyo mdogo," alikumbuka. "Alikufa bila kupata dozi yake ndogo ya maziwa."
Salah Samara, mvulana wa miezi minne, ni mmoja wa watoto wanaougua sana ambao Dk Abdel Jalil na wenzake wanajaribu kuwatibu kwa rasilimali chache walizonazo.
Mama yake alisema alizaliwa kabla ya wakati wake na aliishiwa na maji mwilini sana, na kwamba sasa anaugua ugonjwa wa figo na kutotoka kwa mkojo, jambo ambalo ni chungu sana na kusababisha tumbo kujaa.
"Moyo wangu unauma sana kutokana na haya yanayotokea kwake. Ni jambo gumu sana kuona mtoto wako analia kila siku kwa kushindwa kukojoa... na madaktari wanashindwa kumpa msaada."
"Ana haki ya kupata matibabu na ana haki ya kila kitu kingine, kwa sababu ya kuwa mtoto mwanzoni mwa maisha yake," aliongeza.
"Hali yake inazidi kuwa mbaya kila siku. Anahitaji matibabu nje ya nchi mara moja na kwa dharura. Ninatumai kwamba yeyote atakayesikiliza sauti yangu atasaidia kumtibu mtoto wangu."

Chanzo cha picha, Getty Images
Dk Ahmed al-Kahlot, mkurugenzi wa Kamal Adwan, wakati huo huo alionya kwamba vifo vya watoto hadi sasa vilivyoripotiwa na wizara ya afya havikutoa picha ya ukubwa wa tatizo.
“Idadi ya vifo vinavyotokana na utapiamlo vilianza kuhesabiwa wiki mbili zilizopita, hivyo idadi halisi ni kubwa zaidi ya hiyo,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliandika kwenye X, zamani Twitter, Jumatatu kwamba shirika hilo liliweza kupeleka mafuta na vifaa muhimu vya matibabu kwa Kamal Adwan na hospitali nyingine waliyotembelea wikendi, Al. -Awda katika Jabalia. Lakini alionya kwamba utoaji uliwakilisha sehemu ndogo ya mahitaji ya dharura ya kuokoa maisha.
"Tunatoa wito kwa Israel kuhakikisha misaada ya kibinadamu inaweza kutolewa kwa usalama, na mara kwa mara. Raia, hasa watoto, na wafanyakazi wa afya wanahitaji msaada wa kuongezwa mara moja. Lakini dawa muhimu ambayo wagonjwa hawa wote wanaihitaji ni amani," alisema.
Serikali za Magharibi pia zinaongeza shinikizo kwa Israel kufanya zaidi kuwezesha usambazaji wa misaada, siku ya Jumanne Joe Biden alisema "Lazima tupate misaada zaidi Gaza... Hakuna kisingizio, hakuna".
Hata hivyo siku ya Jumanne Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema jaribio lake la kwanza katika muda wa wiki mbili la kuleta msaada wa chakula kaskazini mwa Gaza lilizuiwa na wanajeshi wa Israel. Shirika la Umoja wa Mataifa lilisema msafara wa lori 14 "ulirudishwa " kwenye kituo cha ukaguzi na baadaye kuporwa na umati wa "watu waliokata tamaa".
Wizara ya ulinzi ya Israel iliyopewa jukumu la kuratibu upatikanaji wa misaada huko Gaza ilisema: "Tutaendelea kupanua juhudi zetu za kibinadamu kwa wakazi wa Gaza huku tukitimiza malengo yetu ya kuwakomboa mateka wetu kutoka kwa Hamas na kuikomboa Gaza kutoka kwa Hamas."
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa na Lizzy Masinga












