Vita vya Gaza: 'Alikwenda kuwatafutia watoto wake chakula akarudi ndani ya jeneza'

.
Maelezo ya picha, Zouahra anasema mumewe aliuawa aliposhambuliwa kichwani na Israeli

Katika nyakati ambazo hayuko kwenye hema akitunza watoto, Zouahra anatazama nje kwenye bahari inayounda mpaka wa ulimwengu wake. Katika siku hii, jua linamuonekano wa bluu na wakati linapotua, vivuli vya dhahabu na nyekundu vitatanda kwenye upeo wa macho.

Ni bahari hiyo hiyo inayosomba fukwe za Tel Aviv upande wa kaskazini, na kusababisha mafuriko kwenye pwani zote za Mediterania. Na ni bahari ambayo, Zouahra anasema, kombora kutoka upande wa Israeli lilisababisha kifo kwa mumewe.

"Alikuwa akielekea ufukweni mwa bahari ambako kulikuwa na magari na msafara wa misaada… Kulikuwa kumejaa watu hadi pomoni, na boti za kijeshi zikaanza kuwafyatulia watu risasi. Mume wangu alishambiliwa kichwani," anasema.

Hiyo ilikuwa tarehe 9 Februari - lakini Zouahra, ambaye sasa anaishi katika sehemu ya kambi inayohifadhi wajane na mayatima, hakujua mara moja.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 26 alikuwa amejifungua mtoto wake wa nne.

Mwanzoni, wale vijana waliokuwa kwenye eneo la tukio na walikuwa wanajua ukweli walitaka kumficha Zouahra habari hizo. "Mahmoud amechelewa tu," walisema.

Lakini alijua kuna kitu ambacho hakiko sawa. Shemeji yake alifika huku akilia na kupiga kelele kuwa Mahmoud amefariki. Akiwa na tamaa ya kutaka kujua ukweli, alienda hospitalini, kama asemavyo, "hadi mwisho wa ulimwengu" - kumtafuta.

Zouahra anainama mbele, anainamisha kichwa chake na kulia. Akiona mamake mwenye mfadhaiko, Lana mwenye umri wa miaka mitatu anagusa mkono wake kwa upole. Kisha anaupapasa taratibu mwili wa kaka yake mdogo, Mohammed aliyelala kwenye mapaja ya mama yake.

Zouahra anaanza kuongea tena. "Mwili wake wote ulikuwa umeunganishwa na mashine, na alihisi baridi kali. Sikuweza kuzungumza naye. Nilijaribu, lakini hakujibu".

"Alikuwa amelala... 'Akaenda kuwatafutia watoto wake chakula lakini akarudi ndani ya jeneza'"

Familia ilisambaratika kutokana na vita. Waliishi katika jiji la Gaza kabla ya mapigano na baada ya vita kuanza walikimbilia kambi ya wakimbizi ya Al-Nusseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Huo ulikuwa mwisho wa Mahmoud kufanya kazi kama kibarua katika Kampuni ya Pioneer Food huko Gaza.

Kutoka Al-Nusseirat, waliondolewa tena, wakikimbilia kusini hadi Rafah baada ya Jeshi la Ulinzi la Israeli kuwaambia kuwa ni eneo salama.

,
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zouahra anaishi na wajane wengine katika sehemu ya kambi ya wakimbizi ya Al-Mawasi iliyotengwa kwa ajili ya wanawake na watoto wasio na pa kwenda. Jirani yake Amina alipoteza mume wake na watoto watatu katika shambulio la anga la Israeli kwenye nyumba yao karibu na Khan Younis.

Amina na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitano, Ibrahim - ambaye pia ni mlemavu - walitolewa wakiwa hai kutoka kwenye kifusi kilichozika familia nzima.

Mjane mwingine, Amani Jasser Al-Khawr, 32, alipoteza mume wake, polisi, na watoto wake watano katika shambulio la anga huko Gaza ya Kati mwezi Oktoba - na sasa anaishi katika makazi yaliyotengenezwa kwa paneli za zinki.

Upepo husikika kwenye paneli, kama vile unavyopeperusha karatasi ya plastiki na kitambaa kinamchofunika Zouahra na watoto wake.

Wanaweza kuona jinsi anavyopambana. Lakini ingawa makazi yake ni hafifu na nzi mara kwa mara huwa wako juu ya watoto, ardhi imefagiliwa na nguo za familia zimebanwa kwenye kamba ya kuanikia nguo zinapofuliwa nje.

Zouahra anaonyesha picha za marehemu mumewe - mwanamume mzuri, anayeilinda familia yake.

"Sijui nifanye nini bila yeye. Yeye ndiye alikuwa akikimu mahitaji yangu na watoto wangu. Hakuwahi kunifanya mimi nimuhitaji mtu yeyote… Hakuna anayetujali sasa," Zouahra anasema.

Maisha haya yanafanya kuwe na wajane wengi. Zouahra anahitaji nepi kwa ajili ya mtoto na mvulana wake mlemavu, Mustafa. Anazungumza juu ya wasiwasi wake wa kila wakati.

"Anaona kitu nashindwa kumpatia, analia na kujigonga chini akiomba, lakini siwezi kumnunulia.

"Mustafa ana mahitaji mengi ambayo siwezi kumudu. Anaendelea kujikojolea na kuniomba vitu ambavyo siwezi kumpa. Anaomba chakula, juisi, tufaha na matunda, na mimi siwezi kumnunulia."

Siku chache zilizopita, familia nyingine iliyo karibu iliweza, kwa namna fulani, kupata kuku. Watoto wa Zouahra walitazama. Walikuwa na hamu kubwa sana ya kula.

Kisha, Lana mwenye umri wa miaka mitatu akaanza kulia. Lakini hakukuwa na chochote cha kufanya. Watu wengine walikuwa na bahati, au labda walikuwa na pesa, na watoto wao wangeweza kula.

Wajane wa Al-Mawasi wanasubiri kwenda kwenye kambi mpya ya wanawake wasio na waume zao na watoto wao baada ya kukamilika kutengenezwa.

Huko wanatumaini la kupata chakula, mahali pa kujikinga na upepo - vivyo hivyo wanatumai kwamba mauaji yanaweza kukoma ili kusiwe na kinachochukuliwa tena kutoka kwao.

Imefasiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi