Video za wanajeshi wa Israel kutoka Gaza zinaweza kukiuka sheria za kimataifa, wasema wataalamu
Video za wafungwa wa Gaza waliovuliwa nguo, kufungwa na kufunikwa macho ambazo zilinakiliwa na kupakiwa mtandaoni na wanajeshi wa Israel zinaweza kukiuka sheria za kimataifa, wataalamu wa sheria wanasema.
Sheria ya kimataifa inasema wafungwa hawapaswi kufanyiwa fedheha mbele ya Umma.
BBC Verify iliangalia mamia ya video zilizowekwa hadharani na wanajeshi wa Israel huko Gaza tangu Novemba 2023. Tulithibitisha video nane zikiwaonesha wafungwa.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema imemsimamisha kazi mmoja wa askari wa akiba tuliowatambua. Jeshi halikuzungumza zaidi kuhusu hili.
Dk Mark Ellis, mshauri mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mahakama za kimataifa za uhalifu, alisema picha tulizomuonesha za wanajeshi wa Israel zinaweza kukiuka sheria zinazotambulika za kuwahudumia wafungwa wa vita.
Video nyingi tulizochambua zinaonesha matukio ya mapigano na wanajeshi wakitazama nyumba zilizotelekezwa na wakazi.
Video moja inaonesha askari wakiwa na silaha wakiwa wamevalia kama dinosaria, na wengine wanawaonesha wakitengeneza mkahawa wa pizza katika nyumba tupu ya Wapalestina.
Lakini tulipata nane, zilizorekodiwa na kutolewa hadharani, jambo ambalo wataalamu wa sheria wanasema linaonesha unyanyasaji wa wafungwa wa Kipalestina.
Zote zilitumwa na wanaume ambao ni askari, ambao hawakuficha utambulisho wao.
Tuligundua moja kwa kuchambua picha ya mfungwa wa Kipalestina ambayo ilisambazwa sana mtandaoni mapema wiki hii. Zana za kutafuta picha zinaonesha ilitoka kwenye akaunti ya YouTube ya mwanajeshi wa Israel Yossi Gamzoo Letova.
Amepakia video nyingi kutoka Gaza tangu mwanzoni mwa Desemba, zikiwemo picha za wanajeshi wake, ambao analitaja kama Kikosi cha Granite 932, ambacho ni sehemu ya Kikosi cha Nahal cha IDF.
Katika video iliyochapishwa tarehe 24 Desemba 2023, mfungwa huyo wa Kipalestina kutoka kwenye picha hiyo anaoneshwa akiwa amevuliwa nguo na kuvuja damu huku mikono yake ikiwa imefungwa na kuketi kwenye kiti huku akihojiwa.

Chanzo cha picha, Youtube
Tulilitambua eneo hilo kuwa la Chuo cha Gaza, shule iliyo kaskazini mwa ukanda huo, kutokana kna mapambo mahususi pamoja na nembo ya taasisi hiyo ambayo inaweza kuonekana kwenye video na ambayo tulilinganisha na ukurasa wake wa Facebook.
Baadaye katika video hiyo hiyo, mfungwa huyo anaonekana akitembezwa bila viatu katika mitaa ya Gaza.
Katika taarifa, IDF ilisema: "Picha hiyo ilipigwa wakati wa kuhojiwa. Mshukiwa hakujeruhiwa. Askari wa akiba alipiga picha na kuchapisha picha hiyo kinyume na maagizo na maadili ya IDF. Hivi karibuni iliamuliwa kusitisha huduma yake."
Video zaondolewa
Siku hiyo hiyo, Bw Letova alichapisha video nyingine ya YouTube inayoonesha mamia ya wafungwa wa Kipalestina wakiwa wamekusanyika katika uwanja wa michezo, ambao tuliuweka na kuuthibitisha kuwa uwanja wa Yarmouk wa Gaza.
Wengi wa walio kwenye video hiyo wamevuliwa nguo zao za ndani. Wengine wamefunikwa macho na kupiga magoti chini, huku wanajeshi wa Israeli wakitazama.
Wakati mmoja, kundi linalojumuisha wafungwa watatu wa kike wanaonekana wakiwa wamepiga magoti na kufumba macho nyuma ya goli la mpira wa miguu huku bendera ya Israel ikitundikwa juu yake.

Chanzo cha picha, Youtube
Mwanajeshi wa Israel anaonekana kwenye video hiyo mara kadhaa, na anaonekana kufahamu kuwa anarekodiwa.
Kwa kulinganisha sare yake na nembo yake na picha nyingine zinazopatikana hadharani za sare za IDF mtandaoni, tulimtambua kama luteni kanali, au kamanda wa kikosi.
Video zote mbili zilitolewa kwenye ukurasa wa umma wa YouTube wa Bw Letova mara baada ya BBC kuwasiliana na IDF.
Kanuni za maadili
Video mbili zilizopakiwa kwenye mtandao wa Tiktok na mwanajeshi mwingine wa IDF ni pamoja na picha za wafungwa waliofunikwa macho, zikiwa zimeunganishwa na picha za wanajeshi wakiwa wamejipanga na bunduki.
Moja iliyochapishwa tarehe 14 Disemba, iliyowekwa kwenye wimbo wa rap wa Israeli, inajumuisha picha ya wafungwa waliofunikwa macho wakiwa wamepakizwa kwenye gari la kubebea mizigo huku askari akiwa amejiweka karibu nao huku vidole gumba vikiwa juu.
Tulimtambua askari huyo kutoka kwenye akaunti zake nyingine za mitandao ya kijamii kuwa ni Ilya Blank.

Chanzo cha picha, Tik Tok
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alichapisha video ya pili ambayo inajumuisha picha ya mtu aliyefunikwa macho sakafuni, akiwa amezungukwa na wale wanaoonekana kuwa askari watatu wa IDF.
Tumepata idadi ya picha zilizotumiwa kwenye video zake kaskazini mwa Gaza.
Baada ya kuwasiliana na IDF na TikTok, video ziliondolewa.
Kifungu cha 13 cha Mkataba wa Tatu wa Geneva kinasema lazima walindwe wakati wote, haswa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji au vitisho na dhidi ya "matusi".
Dkt. Ellis anasema jambo la msingi ni "kutojenga udadisi wa umma" kwa wafungwa wa vita na sio "kuwadhalilisha".
Aliongeza: "Wazo la kuwatembeza watu wakiwa wamevalia nguo zao za ndani na kurekodi filamu na kuzituma bila shaka litakiuka hilo.
"Sheria ambazo zimewekwa haziwezi kuruhusu aina hii ya vitendo."
Prof Asa Kasher, msomi wa Israeli ambaye alisaidia kuandika kanuni za kwanza za maadili za IDF, alisema kushiriki picha za watu walio nusu uchi ni kinyume na kanuni za maadili za IDF.
Alisema kunaweza kuwa na hitaji la kijeshi kumvua nguo mfungwa kwa muda mfupi ili kuangalia kama wana silaha, lakini haoni sababu ya "kupiga picha kama hiyo na kuisambaza kwa umma".
“Sababu ya kuwaweka nusu uchi ni kuwadhalilisha,” alisema.
Wakili wa haki za binadamu Michael Mansfield alisema picha hizo zinapaswa kutathminiwa na mahakama ya Umoja wa Mataifa.
"Kuna kizuizi kikali sana kuhusu jinsi unavyoshughulika na watu waliowekwa kizuizini ambao ni wafungwa wa vita wakati wa vita au migogoro, ambayo ni wazi, na kifungu hicho ni kweli ambacho umekusudiwa kuwatendea wafungwa. heshima,” alisema.
Tulituma video sita kwa TikTok, ambao walithibitisha kuwa zote zilikiuka miongozo yao ya jukwaa hilo. Walisema miongozo yao ilikuwa wazi kwamba maudhui "yanayotaka kuwadhalilisha waathiriwa wa mikasa ya vurugu" hayakuvumiliwa. Video zote zimetoweka kwenye jukwaa.
Msemaji wa YouTube alisema kuwa imeondoa makumi ya maelfu ya video zenye madhara na kusitisha maelfu ya chaneli wakati wa mzozo kati ya Israel na Gaza, na kwamba ina timu zinazofanya kazi wakati wote kufuatilia maudhui ya video zenye madhara.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga













