Israel Gaza: 'Niliwapitisha watoto wangu katikati ya milipuko na kando ya maiti zilizooza'

Chanzo cha picha, JEHAD EL-MASHHRAW
Baada ya wiki za mashambulizi ya Israel, tarehe 16 Novemba Jehad El-Mashhrawi na familia yake changa walikimbia makazi yao kaskazini mwa Gaza. Mpiga picha wa BBC Idhaa ya Kiarabu anashiriki maelezo ya wazi na ya kushtua ya yale ambayo yeye, mke wake na watoto walipitia walipokuwa wakielekea kusini.
Onyo: Taarifa hii ina maelezo ya picha ambayo huenda yakawaathiri badhi ya wasomaji
Tuliondoka kwa haraka sana. Tulikuwa katikati ya kuoka mikate ndipo tukagundua nyumba zilizokuwa mkabala ya yetu zilikuwa zikipigwa mabomu, moja baada ya nyingine. Nilijua hivi karibuni itakuwa zamu yetu. Tulikuwa tumepakia baadhi ya mabegi endapo hili lingetokea lakini kila kitu kiliharakishwa tukasahau kuyachukua. Hatukufunga hata mlango wa mbele.
Tulikuwa tumengoja kuondoka kwa sababu hatukutaka kuwahamisha wazazi wangu wazee na tulikuwa tumetumia akiba ya miaka kadhaa ili kujenga nyumba yetu huko al-Zeitoun, lakini mwishowe tulilazimika kwenda. Mtoto wangu wa kiume, Omar, alikufa huko mnamo Novemba 2012, aliuawa wakati makombora yalipopiga nyumba yetu katika vita vingine na Israeli na sikuweza kuhatarisha kupoteza watoto wengine zaidi.
Nilijua kuwa huko kusini hakukuwa na umeme, hakuna maji na watu walilazimika kupanga foleni kwa masaa kadhaa ili kutumia choo. Lakini mwishowe, tukichukua chupa tu ya maji na mkate uliobaki, tuliungana na maelfu ya watu wengine waliokuwa katika safari hatari katika barabara ya Salah al-Din kuelekea kusini, ambapo Israel ilisema ilikuwa salama.

Chanzo cha picha, MAJED HAMDAN/ASSOCIATED PRESS
Watu wengi wa familia yangu walitembea pamoja - mke wangu Ahlam, wana wetu wanne, ambao wana umri wa miaka miwili, minane, tisa na 14, wazazi wangu, kaka, dada, binamu na watoto wao.
Barabara ya Salah al-Din
Tulitembea kwa saa nyingi na tulijua kwamba hatimaye tungelazimika kupitia kituo cha ukaguzi cha Israeli ambacho kiliwekwa wakati wa vita. Tulikuwa na wasiwasi na watoto wangu waliendelea kuuliza: "Jeshi litatufanyaje?"
Tulisimama karibu theluthi mbili ya maili (1km) kutoka kituo cha ukaguzi na tukajiunga na foleni kubwa ya watu iliyojaza barabara nzima. Tulitumia zaidi ya saa nne kusubiri pale na baba alizimia mara tatu.
Kulikuwa na askari wa Israel wakitutazama kutoka kwa majengo yaliyolipuliwa kwa mabomu upande mmoja wa barabara na zaidi kwenye eneo tupu la upande mwingine.
Tulipokaribia eneo la ukaguzi tuliona askari zaidi juu yetu wakiwa kwenye hema kwenye kilima. Tunafikiri walisimamia kituo cha ukaguzi wakiwa mbali na hapo, wakitutazama kupitia darubini na kutumia vipaza sauti kutuambia la kufanya.
Kulikuwa na kontena mbili za meli zilizokuwa wazi karibu na hema. Ilibidi wanaume wote wapite kwa moja na wanawake kupitia kwa nyingine, wakiwa na kamera zilizozoezwa kila mahali. Tulipomaliza, wanajeshi wa Israel waliomba kuona vitambulisho vyetu na tukapigwa picha.
Ilikuwa kama siku ya kiama.

Chanzo cha picha, MAXAR
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Niliona watu wapatao 50 wakiwa kizuizini, wote wanaume,wakiwemo majirani zangu wawili. Kijana mmoja alisimamishwa kwa sababu alikuwa amepoteza hati zake na hakuweza kukumbuka nambari yake ya kitambulisho. Mwanaume mwingine aliyekuwa karibu nami kwenye foleni aliitwa gaidi na mwanajeshi wa Israel, na kisha aakachukuliwa .
Waliambiwa wavue nguo zao za ndani na kukaa chini. Baadaye wengine walitakiwa wavae nguo na kuondoka huku wengine wakiwa wamefumbwa macho.
Niliona wafungwa wanne waliokuwa wamefunikwa macho, wakiwemo majirani zangu, wakichukuliwa nyuma ya kilima cha mchanga na jengo lililobomolewa. Walipokuwa hawaonekani, tulisikia milio ya risasi. Sijui kama walipigwa risasi au la.
Baadaye ,watu wengine waliofunga safari kama yangu walipigiwa simu na mfanyakazi mwenzangu huko Cairo. Mmoja wao, Kamal Aljojo, alisema kuwa baada tu ya kupitia kituo cha ukaguzi wiki moja mapema, aliona maiti, lakini hakujua jinsi walivyokufa.
Mwenzangu pia alizungumza na mtu anayeitwa Muhammed ambaye alipitia kizuizi hicho mnamo tarehe 13 Novemba. "Askari aliniomba nivue nguo zangu zote, hata za ndani," Muhammed aliambia BBC. Aliongeza: "Nilikuwa uchi mbele ya kila mtu anayepita. Niliona aibu. Ghafla askari wa kike alininyooshea bunduki na kucheka kabla ya kuiondoa haraka. Nilifedheheka." Muhammed alisema alilazimika kusubiri uchi kwa takriban saa mbili kabla ya kuruhusiwa kwenda.
Ijapokuwa mimi na mke wangu, watoto, wazazi na mimi tulipitia kituo cha ukaguzi salama, ndugu zangu wawili walichelewa.
Tukiwa tunawasubiri, askari mmoja wa Israel alifokea kundi la watu waliokuwa mbele yetu waliokuwa wakijaribu kurudi kwenye makontena ili kuwaangalia ndugu zao waliokuwa wameshikiliwa.
Alitumia kipaza sauti kuwaambia waendelee na wakae umbali wa angalau 300yds (300m), kisha askari akaanza kupiga risasi hewani kuelekea kwao ili kuwatisha. Tulikuwa tumesikia milio mingi ya risasi tukiwa kwenye foleni.
Kila mtu alikuwa akilia na mama yangu alikuwa akilia: "Ni nini kiliwapata wanangu? Je, waliwapiga risasi?"
Baada ya zaidi ya saa moja hatimaye ndugu zangu walikuja .
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) liliambia BBC kwamba "watu wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na mashirika ya kigaidi" walizuiliwa kwa uchunguzi wa awali, na ikiwa wataendelea kuwa washukiwa walihamishiwa Israel kwa mahojiano zaidi. Wengine "waliachiliwa mara moja", ilisema.
Ilisema ilibidi nguo ziondolewe ili kuangalia fulana za vilipuzi au silaha nyingine na wafungwa walivalishwa haraka iwezekanavyo. Ilisema haikulenga "kudhoofisha usalama na utu wa wafungwa" na kwamba IDF "inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa".
IDF pia ilisema "haiwapigi risasi raia wanaotembea kando ya ukanda wa misaada ya kibinadamu kutoka kaskazini kwenda kusini", lakini wakati vijana walipojaribu kuelekea upande mwingine "walikutana na risasi kwa madhumuni ya kutawanywa, baada ya kutawanywa."
Iliongeza kuwa sauti ya risasi ilikuwa ya kawaida na "mlio wa risasi peke yake haujumuishi dalili ya risasi kutoka mahali maalum au ya aina fulani".
Mimi na mke wangu tulihisi afueni tuliposonga mbele na kituo cha ukaguzi kikatoweka mbele yetu, lakini hatukujua kwamba sehemu ngumu zaidi ya safari ilikuwa bado inakuja.

Tulipokuwa tukienda kusini zaidi, niliona miili 10 hivi katika sehemu mbalimbali kando ya barabara.
Sehemu nyingine za mwili zilizotawanyika, zilizooza, zilifunikwa na nzi huku ndege wakinyong'onyea mabaki. Ilitoa moja ya harufu mbaya zaidi ambayo nimewahi kupata.
Sikuweza kustahimili wazo la watoto wangu kuwaona hivyo nilipiga kelele juu kabisa ya mapafu yangu, nikiwaambia watazame angani na waendelee kutembea.
Niliona gari lililoungua na kichwa cha binadamu kilichokatwa kikiwa ndani. Mikono ya maiti iliyooza isiyo na kichwa bado ilikuwa imeshikilia usukani.
Kulikuwa pia na miili ya punda na farasi waliokufa, mingine ikiwa mifupa, na milundo mikubwa ya takataka na vyakula vilivyoharibika.
Kisha kifaru cha Israel kikatokea kando ya barabara, kikisogea kwetu kwa mwendo wa kasi. Tuliogopa na ili tuondoke, ilitubidi kukanyaga maiti. Baadhi ya watu katika umati wa watu walijikwaa kwenye miili. Kifaru kilibadilisha mwendo takriban 20yds (20m) kabla ya kufika kwenye barabara kuu.
Ghafla, kando ya barabara, jengo lililipuliwa kwa bomu. Mlipuko huo ulikuwa wa kutisha na mabomu yaliruka kila mahali.
Nilitaka ulimwengu utumeze.
Tulitetemeka na kuishiwa nguvu lakini tukabebwa kuelekea kambi ya Nuseirat. Tulifika hapo jioni na tukalazimika kulala nje . Kulikuwa na baridi.
Tukaweka koti langu karibu na wana wetu wa kati, tukiingiza mikono yao kwenye mikono ili kujaribu kuwapa joto. Tulimfunika mtoto wetu mdogo kwa shati langu. Sijawahi kuwa na baridi kama hiyo sana katika maisha yangu yote.
Wakati BBC ilipouliza kuhusu kifaru na miili hiyo, IDF ilisema kwamba "wakati wa mchana, vifaru husafiri kwenye njia ambazo zinapita kwenye barabara ya Salah al-Din, lakini hakuna kesi ambayo vifauri viliekelezwa kwa raia kutoka kaskazini kwenda kusini wa Ukanda wa Gaza '
IDF ilisema haifahamu kisa chochote cha milundo ya maiti kwenye barabara ya Salah al-Din lakini kuna nyakati ambapo magari ya Gaza "yalitelekeza miili wakati wa safari, ambayo IDF iliiondoa baadaye".
Msako wa kutafuta eneo salama
Asubuhi iliyofuata tuliondoka mapema kuelekea Khan Younis, mji wa pili kwa ukubwa wa Gaza. Tulimlipa mtu atupeleke sehemu ya njia kwa mkokoteni unaovutwa na punda. Kisha huko Deir al-Balah, tulipanda basi ambalo lilikusudiwa kubeba watu 20 tu, lakini watu 30 walipanda. Wengine walikaa juu ya paa na wengine waling'ang'ania milango na madirisha kutoka nje.
Huko Khan Younis, tulijaribu kutafuta mahali salama pa kukaa katika shule inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa ambayo ilikuwa imegeuzwa kuwa makazi, lakini ilikuwa imejaa. Tuliishia kukodi ghala chini ya jengo la makazi badala yake tukakaa humo kwa juma moja.

Chanzo cha picha, JEHAD EL-MASHHRAW
Wazazi wangu, kaka na dada zangu waliamua kubaki Khan Younis, lakini baada ya soko la ndani kulipuliwa, mimi na mke wangu tuliamua kuwapeleka watoto wetu kusini zaidi hadi Rafah ili kuwa pamoja na familia yake. Walifanikiwa kupata lifti kwenye gari na nilijiunga nao baadaye kwa basi, lakini lilikuwa limejaa sana ikabidi nining'inie nje ya mlango.
Sasa tunakodisha nyumba ndogo ya nje yenye paa iliyojengwa kwa bati na plastiki. Hakuna kitu cha kutulinda kutokana na vitu vinavyotupwa na milipuko.
Kila kitu ni ghali na hatuwezi kupata vitu vingi tunavyohitaji. Ikiwa tunataka maji ya kunywa, tunapaswa kupanga foleni kwa saa tatu na hatuna chakula cha kutosha kwa milo mitatu kwa siku, kwa hiyo hatuli chakula cha mchana tena, bali kifungua kinywa na chakula cha jioni tu.
Mwanangu alikuwa akila yai kila siku. Yai - unaweza kufikiria? Siwezi hata kumpa hilo sasa. Ninachotaka kufanya ni kuondoka Gaza na kuwa salama pamoja na watoto wangu, hata kama hiyo inamaanisha kuishi kwenye hema.
Taarifa za ziada kutoka kwa Abdelrahman Abutaleb wa BBC News Arabic akiwa mjini Cairo.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












