Kufumbwa macho na kupigwa vibaya: Wanaume sita Wapalestina wanasimulia jinsi walivyowekwa kizuizini kwa mwezi mmoja Israeli

- Author, Adnan El-Bursh
- Nafasi, BBC Arabic
- Akiripoti kutoka, Rafah, Gaza
Wanaume sita wa Kipalestina kutoka Gaza wanasema walipigwa vibaya na jeshi la Israel kwa takriban mwezi mmoja wakiwa kizuizini.
Mmoja wa watu hao anasema wanajeshi wa Israel walimpiga risasi kwenye mguu wake wa kulia, ambao ulikatwa wakati yeye na wengine wakishikiliwa.
Chini ya sheria za vita, wafungwa wote wanatakiwa kutendewa utu.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) aliambia BBC kwamba haikuwa na taarifa za kutosha kuchunguza madai ya mtu huyo ambaye mguu wake ulikatwa.
Msemaji huyo pia alisema Israel inaheshimu sheria za kimataifa.

Israel iliwaachilia wanaume hao siku ya Alhamisi, 14 Desemba katika mpaka wa Kerem Shalom unaovuka kutoka Israel hadi Gaza.
Wanaume hao kisha walitafuta matibabu katika hospitali ya Martyr Mohammed Yusuf al-Najjar huko Rafah kusini mwa Gaza.
Makumi ya wafungwa wa zamani walikuwepo. Jumla ya wanaume saba walikubali kuzungumza nami.
Wanaume wanne walikaa kwenye mstari kwenye kitanda cha hospitali, mtu wa tano alisimama kando yao.
Wote walikuwa wamevalia nguo za rangi ya kijivu na kunyoosha viganja vyao vilivyo na michubuko, huku wengine wakiwa wamefura midomo iliyokuwa na vidonda.
Wengine walikuwa bado wamevalia pingu nyeupe za plastiki zilizotumiwa na Israel kuwaweka kizuizini.

Mohammed Dawood alisema alizuiliwa alipokuwa akifuata amri ya Israel ya kuhamia kusini.
"Tulitoka Beit Lahia kaskazini na tulikuwa tunahamia kusini kupiti njia salama iliyotolewa," aliniambia.
"Walitukamata (IDF) kutoka huko. Walituhoji. Je! nyinyi ni Hamas? Je, ninyi ni wanamgambo wa kundi la Islamic Jihad?"
Alisema alizuiliwa kwa siku 26 na hatimaye kuachiliwa kwa sababu "hawakuweza kupata chochote kutoka kwetu".

Tarehe 14 Novemba IDF ilitangaza kufunguliwa kwa muda kwa njia za kuwahamisha Wapalestina kuelekea kusini kutoka kaskazini mwa Gaza.
Israel ilielezea kama "njia salama" kwa maslahi ya kibinadamu kwenye barabara kuu ya Salah al-Din.
Kulikuwa na ripoti za wanaume kuchunguzwa na IDF na kuwekwa kizuizini.
"Nilifungwa kamba na macho yangu yalikuwa yamezibwa kama wanaume wengine wote," alisema Mohammed Dawood.
“Walitunyanyasa, walitutemea mate na kutudharau, sote tulipigwa.
"Iwapo mtu yeyote atawaambia kuwa ni mgonjwa au mguu wao umekatwa, wao (askari wa Israeli) wangejibu, 'Kufia hapa'.
"Na wangewafunga kwa pingu zao."

Msemaji wa IDF alikana madai haya.
"Kuhusu michubuko kutokana na kufungwa pingu wafungwa, tunafafanua kwamba wafungwa wanafungwa pingu kulingana na kiwango cha tishio walichonacho na afya zao," IDF ilisema katika taarifa.
"Hawaning'inizwi kutoka kwa mikono yao kwenye kituo wakati wowote."
Mohammed alisema walikuwa na blanketi moja tu kati yao na waliwekwa nje kwenye mvua, huku wakipewa chakula kidogo au maji.
Kwa mara nyingine, IDF ilikataa hili na kusema wafungwa wanapewa milo mitatu kwa siku, maji na huduma za matibabu.
Hakuna anayejua ni wanaume wangapi wamezuiliwa na jeshi la Israel huko Gaza au wanazuiliwa wapi.
Suala hili limekuwa gumzo tangu video kutoka Beit Lahia ilipoibuka mapema mwezi huu.
Ilionyesha makumi ya wanaume wa Kipalestina wakiwa wamevuliwa nguo zao za ndani na kuketi pamoja huku wanajeshi wa Israel wakiwalinda.

Mtu wa sita, Mahmoud Abu Husein, alikaa kwenye kiti kwenye korido ya hospitali.
Alikuwa na mvi na mguu wake wa kulia haukuwepo, na dalili za damu kwenye sehemu ya chini ya nguo yake .
"Nilikuwa nyumbani kwangu, niliwaambia kuwa ninaumwa, mimi ni mzee, mwenye umri wa miaka 62," aliambia BBC, akiongeza kuwa anatoka kambi ya al-Shati kaskazini mwa Gaza.
"Waliniambia hapana, unahitaji kutujulisha Hamas iko wapi na mateka wako wapi.
“Nilipowaambia sijui walinipiga risasi mguuni, baadaye wakanikata mguu.
"Walinifanya nisaini karatasi iliyosema kuwa mguu wangu ulikuwa na tatizo."
IDF ilisema haikuwa na taarifa za kutosha kuchunguza tukio hili.

Madaktari katika hospitali hiyo ambao hawakutaka kutajwa majina walisema watu hao walifika hospitalini wakiwa katika hali mbaya. Walisema wawili kati ya wanaume hao wangali wanapokea matibabu, akiwemo Bw Husein.
Mzee mwingine, Mohammed Yusuf Ali Abu Shamla, naye alikuwa akisubiri kuhudumiwa kwenye hospitali hiyo. Anatokea kitongoji cha Zeitoun, mashariki mwa mji wa Gaza.
Bw Shamla, mwanamume wa saba ambaye BBC ilizungumza naye, alikuwa amevalia suti ya rangi ya kijivu sawa na wengine, lakini alionekana kuzuiliwa na Israel baadaye.

"Tinga lilianza kuharibu nyumba yangu nikiwa ndani. Watu wengine karibu watu 40 pia waliharibiwa nyumba zao ," aliiambia BBC. "Wanawake walikuwa wakipiga kelele. Tuliondoka nyumbani tukiwa tumeinua mikono juu."
Alisema aliwekwa kizuizini pamoja na watu wengine sita: wanawe watatu, wapwa wawili na kaka mmoja.
"Walitutaka tuvue nguo, unamaanisha nini tuvue nguo zetu, tuliona aibu lakini tukafuata mashati," alisema.
"Waliendelea kutuamuru tuvue zaidi zaidi. Tulivua hadi nguo zetu za ndani."
IDF ilisema inahitaji kuwavua nguo wafungwa ili kuangalia ikiwa wamevaa mkanda wa vilipuzi au wamebeba silaha.

Bw Shamla alisema walizuiliwa huko Gaza kwa siku tatu na kisha kupelekwa Israel.
Alisema alikuwa akijaribu kuitafuta familia yake kwani aliachiliwa peke yake.
"Sijui wengine wako wapi. Ninajijua tu."
Imetafasiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












