Je, Israel itaweza kuharibu mahandaki ya Hamas huko Gaza? - Magazeti

cv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wanajeshi wawili wa Israel wakiingia katika handaki huko Gaza

Gazeti la Uingereza la "The Times," limechapisha makala ya mhariri wa masuala ya Mashariki ya Kati wa gazeti hilo, Richard Spencer, chini ya kichwa cha habari, "Je, Israel itaweza kuharibu mahandaki ya Hamas huko Gaza?"

Mwandishi anaanza makala yake kwa kuzungumzia kuuawa kwa Sajenti Gal Eisenkot, mtoto wa mjumbe wa Baraza la Vita la Israel, Gadi Eisenkot.

Sajenti Eisenkot kutoka Kikosi cha 551 cha Wanajeshi wa Israel, aliuwawa wakati wa mlipuko katika mlango wa kuingia katika handaki katika eneo la Jabalia, Ukanda wa Gaza.

Spencer anasema mauaji ya Eisenkot yanatoa dalili kuhusu changamoto kubwa inayowakabili wanajeshi wa Israel katika juhudi zao za kuharibu mtandao wa mahandaki ya Hamas.

Uvumi wa hivi karibuni umesambaa kwamba Israel inasukuma maji ya bahari kwa mabomba ili kuyajaza mahandaki hayo. Mwandishi amemnukuu mhandisi wa jeshi la Israel mwenye cheo cha Luteni Kanali Amit akisema:

"Jeshi la Israel linafanya kazi ya kuweka mabomu kwenye mahandaki hayo." Lakini alipomuuliza kuhusu mabomba ya maji, alisema hilo haliko katika mipango yao.

Mpango wa timu ya jeshi la Israel kutoka kitengo cha uhandisi wa njia za chini ya ardhi ni kutafuta mahandaki hayo kupitia vifusi vya majengo yaliyobomolewa na mabomu ya angani kwa kutumia vifaa vya sonar. Lakini mwandishi anasema vifaa hivi vina ufanisi mdogo, haswa kwa mahandaki marefu.

Makala hiyo inaeleza hatari iliyopo ya kazi hii kwa kusema - ikiwa watakosea kuona mlango, wapiganaji wa Hamas wanaweza kutokea nyuma yao na kuwashambulia na kisha kutoweka tena.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uchimbaji wa mahandaki ni njia ya kizamani ya mapambano. Mwandishi anasema hakuna jeshi ambalo limejitayarisha kupigana tu chini ya ardhi kama Hamas walivyofanya.

Waisraeli waliamini madai ya Hamas kwamba wana mahandaki yenye urefu wa maili 300 chini ya Gaza ilikuwa ni kutia chumvi, na sasa wanaamini madai hayo si ya kupuuzwa.

Amit alimwambia Spencer, ''mtandao wa mahandaki huko Gaza, yamejengwa kwa zege na ili kuyaharibu unahitaji kiasi kikubwa cha vilipuzi."

Makala hiyo pia inamnukuu, Profesa wa masomo ya vita kutoka Chuo Kikuu cha Exeter, Anthony King anasema, ''mpango wa jeshi la Israel wa kuharibu mahandaki utachukua muda wa miezi kadhaa, muda huo ni mrefu katika eneo lenye watu milioni 2.3 ambao wanahitaji makazi salama.''

King anasema, "kwa hakika Israel inaweza kuidhoofisha Hamas pakubwa na kuharibu mfumo wa mahandaki kwa kiasi kikubwa, lakini sina imani kwamba kudhibiti mtandao mzima wa mahandaki ni jambo linaloweza kufikiwa kikamilifu.''

'Kuna mauaji ya halaiki yanatokea Gaza na ulimwengu unatazama'

c

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waathirika wengi wa mashambulizi ya Israel ni watoto

Tunaligeukia gazeti la The Guardian la Uingereza, limechapisha makala ya mkuu wa ujumbe wa Palestina nchini Uingereza, Hossam Zomlot, kuhusu kile alichokitaja kuwa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na jumuiya ya kimataifa kutochukua hatua kuhusu kinachoendelea.

Zomlot anasema katika makala hii: "Kuna mauaji ya halaiki yanatokea Gaza na ulimwengu unatazama."

Wakati ulimwengu unatazama mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel - chini ya miezi miwili, na kwa mujibu wa Save the Children, idadi kubwa ya watoto wameuawa kuliko idadi ya watoto wanaouawa katika maeneo ya vita kote duniani kila mwaka tangu 2019.

Kuna idadi kubwa ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wameuawa kuliko kipindi chochote kama hicho katika historia ya Umoja wa Mataifa. Idadi kubwa ya waandishi wa habari wameuwawa kuliko kipindi chochote cha migogoro tangu 1992.

Mwandishi anaendelea kusema, nchi zenye nguvu duniani lazima zianze kutilia maanani wajibu wao kuhusu mfumo wa kimataifa hasa wajibu wa kutekelezwa kwa sheria za kimataifa na maamuzi ya kimataifa kuhusu haki, usawa na uwajibikaji.

Israel haifanyi vita dhidi ya Hamas, bali inaendesha vita dhidi ya watu wa Palestina. Anaamini hilo liko wazi kutokana na ulipuaji wa kiholela katika Ukanda wa Gaza, kutoa lugha ya mauaji ya halaiki kunakofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa Israel.

Mwandishi wa makala hiyo anamalizia kwa kusema: “Hili lazima likomeshwe sasa. Kuna mengi yako hatarini.''

'Maandamano yanadhoofisha juhudi za uokoaji mateka...'

k

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waandamanaji katika jiji la Tel Aviv wakiishinikiza serikali kuachiliwa huru mateka

Katika gazeti la Israel, Yedioth Ahronoth, tunakutana na makala ya Baruch Stein chini ya kichwa cha habari, "Maandamano yanadhoofisha juhudi za uokoaji mateka na kuimarisha upande Hamas."

Makala hii inaangazia maandamano yaliyoandaliwa na familia za mateka wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza kama njia ya shinikizo kwa serikali ya Israel ili mateka waachiliwe.

Mwandishi anasema mwanzoni mwa makala yake anatambua umuhimu wa kufanya kila linalowezekana ili kuachiliwa kwao, ikiwa ni pamoja na maandamano. Hata hivyo, anadokeza, ni muhimu kuhakikisha vitendo hivyo vinaleta matokeo chanya kuliko kuwa kikwazo.

Katika makala yake, mwandishi anabainisha Netanyahu na serikali ya Israel sio waliowachukua mateka hao, na anapendekeza waandamanaji wafanye maandamano mbele ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini humo au mbele ya balozi za nchi zinazotoa wito kwa Israel kusimamisha mapigano.

Mwandishi anaamini mnufaika wa maandamano hayo ni Hamas - kwani maandamano yanaishinikiza serikali ya Israel kufanya makubaliano zaidi na Hamas. Hilo litawafanya Hamas kuwa na misimamo mgumu zaidi, kuimarisha msimamo wao na kutatiza juhudi za kuwaokoa mateka.

"Kadiri Hamas itakavyopata matokeo mazuri katika kubadilishana mateka, itapelekea makundi mengine ya kigaidi yanayoichukia Israel kuanzisha operesheni za kuwateka watu katika siku zijazo."

Mwandishi anamalizia kwa kusema, msukosuko ambao Israel inapitia kwa sasa unapaswa “kuwaleta pamoja jamii ya Waisraeli, sio kuigawanya na mkazo uwe katika kufanya kazi pamoja, si kugawika au kupingana.''

Ni upi wajibu wa jumuiya ya kimataifa?

sd

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken akiwa na Rais wa Israel, Isaac Herzog

Tunahitimisha ziara yetu kwa makala ya mwandishi wa Kipalestina, Tahseen Yaqeen katika gazeti la Palestina "Al-Ayyam" chini ya kichwa cha habari: "Ni upi wajibu wa jumuiya ya kimataifa?" Anazungumzia wajibu wa kimataifa wa kusimamisha vita.

Hakujakuwa na jambo jipya tangu Oktoba 7. Miezi miwili imepita, na habari ni ile ile: vikosi vya uvamizi kutoka sehemu zote za dunia vinaua watu wetu na makundi yenye silaha yanapambana na kupoteza.

Si jambo jipya, kuna hisia mbili; huzuni na hasira juu ya damu iliyomwagwa kwa hila na kiburi.

Mwandishi anaamini ulimwengu hauna hekima wala ubinadamu - ili kukomesha vita dhidi ya watu wa Gaza. Haoni jambo la ajabu katika hili, kwani nchi tatu wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na nchi nyingine za Ulaya, zinaisaidia Israel kwa fedha na vifaa.

Urusi, China na nchi za kikanda hazichukui hatua ya kukomesha vita, wala hazitangazi msimamo wao - wakisubiri matokeo ya vita. Lakini wajibu wa jumuiya ya kimataifa uko wapi?

Si Israel pekee inayopuuza sheria za kibinadamu wakati wa vita, hata wale walio nyamaza na wasiotangaza msimamo wao - nao hawajali sheria za kimataifa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah