Je, kuna vikundi vingapi vyenye silaha huko Gaza na ni nani?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Na Feras Kilani
- Nafasi, BBC Arabic
Kiongozi mkuu wa Hamas Moussa Abu Marzouk aliambia BBC katika mahojiano ya hivi majuzi kwamba haikuwashikilia mateka wote huko Gaza.
Alisema baadhi yao wanazuiliwa na "makundi tofauti" ambayo yalishiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7 nchini Israel.
BBC Verify imebaini kuwa makundi matano yalishiriki katika shambulio hilo pamoja na Hamas.
Ingawa wameungana katika nia yao ya kutumia ghasia dhidi ya Israel, wanatofautiana kuhusu jinsi taifa la Palestina la baadaye linapaswa kuendeshwa na jukumu la dini ndani yake.
Ni vigumu kutaja idadi kamili ya vikundi vingapi vyenye silaha vipo Gaza.
Kwa hivyo tunajua nini juu ya vikundi hivyo?

Chanzo cha picha, Reuters
Wapiganaji wa Hamas/Al-Qassam
Wapiganaji wa Izz al-Din al-Qassam ni tawi la kijeshi la vuguvugu la Hamas, linalosimamia Gaza tangu 2007.
Imepewa jina la mhubiri ambaye alionekana kama ishara ya upinzani wa Wapalestina.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kundi hilo limepigana katika vita kadhaa na Israel, pamoja na kuwashambulia Waisraeli kwa washambuliaji wa kujitoa mhanga na maelfu ya maroketi.
Hamas ni ilichipuka kutoka vuguvugu la Muslim Brotherhood nchini Misri, ambalo lilianza miaka ya 1920 kwa lengo la kueneza maadili ya Kiislamu na matendo mema, lakini baadaye likaja kuwa la kisiasa .
Moja ya malengo ya Muslim Brotherhood ni kuunda serikali inayotawaliwa na sheria za Kiislamu au Sharia.
Mnamo mwaka wa 2017, Hamas ilitangaza kukata uhusiano na Muslim Brotherhood, lakini mwandishi wa BBC Arabic Feras Kilani anasema wengi katika eneo hilo wanaamini kuwa hicho kilikuwa kifumba macho tu, na uhusiano huo umekaa hivyo muda wote huo.
Likiorodheshwa kama shirika la kigaidi na Israel, Marekani, Uingereza, EU na wengine, tawi la kijeshi la Hamas ndilo kundi lililoongoza mashambulizi dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.
Inakadiriwa kuwa na wapiganaji kati ya 20,000 na 30,000 katika Ukanda wa Gaza.
Hakuna kikundi kingine chenye nguvu na kilichojikita katika uendeshaji wa eneo hilo
Iran inaunga mkono Hamas kwa kutoa ufadhili, silaha na mafunzo, na viongozi wake wameishukuru Iran mara kadhaa hadharani kwa uungaji mkono wake.

Chanzo cha picha, Reuters
Wapiganaji wa Palestinian Islamic Jihad/Al-Quds
Vikosi vya Al-Quds vinachukuliwa kuwa jeshi la pili kwa ukubwa huko Gaza.
Kundi hilo lilianzishwa katika miaka ya 1980 kama tawi la kijeshi la vuguvugu la Islamic Jihad - ambalo tena, kama mengi ya makundi haya, linaitwa shirika la kigaidi na serikali za Magharibi.
Jina hilo linalorejelea Jerusalem kwa Kiarabu, lilipata umaarufu baada ya kundi hilo kuhusika katika mapigano makali na wanajeshi wa Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi mwaka 2002.
Kundi hilo linasemekana kuwa na wapiganaji 2,000, na uhusiano wake na Iran ni mkubwa kuliko ule wa Hamas, mwandishi wetu anaongeza.
Wakati makundi yote mawili yanataka Palestina huru ambayo Uislamu unachukua nafasi muhimu katika serikali, toleo la Islamic Jihad litakuwa taifa lenye misimamo mikali zaidi ya kidini.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na Al Jazeera Arabic, mmoja wa viongozi wake alikiri kuwa walichukua mateka 30 kutoka Israel tarehe 7 Oktoba, lakini alidai kuwa sasa wamewarudisha wale ambao ni wanawake na watoto.
Kiongozi wa PIJ alikataa kuthibitisha ni mateka wangapi bado wanawashikilia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wapiganaji wa Popular Front for the Liberation of Palestine / Abu Ali Mustafa
Wakati mmoja ikijulikana kama Popular Resistance Forces, Abu Ali Mustafa Brigades ni mrengo wa kijeshi wa PFLP, kikundi cha maegemeo ya kikomunisti.
Ilijulikana sana kwa utekaji nyara wa ndege na mashambulizi mengine ya juu ya kimataifa, hasa katika miaka ya 1960 na 1970.
Kabla ya kuibuka kwa Hamas, lilikuwa kundi la pili kwa ukubwa la Wapalestina.
Baadhi ya ripoti zinasema wanashikilia mateka lakini BBC haijaweza kuthibitisha hili kwa njia huru .
Waoiganaji wa Al-Nasir Salah al-Deen
Mwanzoni ilianzishwa mwaka 2000, inaripotiwa kuwa hapo awali ilishiriki katika mashambulizi ya pamoja na Hamas, ikiwa ni pamoja na kuteka nyara mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit mwaka 2006.
Ni mrengo wa tatu kwa ukubwa wa Gaza, mshirika wa Hamas na PIJ, na unachangia jeshi la polisi la Gaza.
Imekuwa na nguvu za kutosha kurusha makombora yake ndani ya Israeli na kudai kuwa ilikamata wanajeshi kadhaa wa Israeli mnamo 7 Oktoba, bila kutoa ushahidi wowote.
Al-Aqsa Martyrs' Brigade
Kundi la wanamgambo linalohusishwa na vuguvugu la Fatah, ingawa halijaidhinishwa moja kwa moja nao.
Fatah ni kundi la kisiasa la kisekula ambalo linaendesha Mamlaka ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Lakini baada ya kupoteza udhibiti wa Gaza kwa Hamas katika uchaguzi wa 2006, ililazimishwa kuondoka katika eneo hilo na Hamas mwaka uliofuata.
Kuna vikundi tofauti vya Brigedi ya Mashahidi wa Al-Aqsa yenye uhusiano na viongozi tofauti wa Fatah, lakini huko Gaza sasa wana nguvu kidogo.
Hii haikuzuia baadhi ya wanachama kuonekana kushiriki tarehe 7 Oktoba, kulingana na uchunguzi wa BBC Verify.
Ilipata picha zinazoonyesha kuhusika, siku ya mashambulizi na katika mazoezi ya mafunzo na makundi mengine kabla.
Mwandishi wa BBC Feras Kilani anasema ni vigumu kujua ikiwa ulikuwa uamuzi wa kundi kuhusika au ni chaguo la watu binafsi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wapiganaji wa Mujahideen
Pia ikiwa na mizizi katika kundi la Fatah, ina uhusiano na Islamic Jihad na itikadi kali ya kidini.
Ni kundi jingine ambalo linadai kuwa linashikilia mateka waliochukuliwa tarehe 7 Oktoba.
Taarifa ya ziada ya Abdirahim Saeed
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












