'Kwa manufaa ya nchi yetu, lazima tubadili uongozi' - Magazeti ya Israel

Chanzo cha picha, REUTERS
Katika magazeti ya Israel na Uingereza, tunatazama makala zinazojadili vita vya Gaza, ikiwa ni pamoja na makala katika gazeti la Yedioth Ahronoth.
Katika uvamizi wa kusini mwa Gaza, lazima tutegemee maafa, makala hii imeandikwa na mwandishi Nahumu Barnea.
'Uvamizi wa Kusini mwa Gaza utaleta maafa'

Chanzo cha picha, Reuters
Mwandishi anaanza makala yake kwa kusema Hamas ilitarajia kuendelea kubadilishana mateka na wafungwa, lakini hakuna nafasi ya kulinganisha kati ya wafungwa wa Kipalestina na mateka.
Anaamini mateka wa Israel ni wakaazi wa kibbutzim, wakati wafungwa ambao Hamas inataka waachiliwe huru wengine ni wauaji waliohukumiwa vifungo vya maisha.
Mwandishi anaamini tatizo kubwa kwa Israel ni mateka ambao wengi wao bado wako hai, lakini wengine wameaga dunia na miili yao lazima ipelekwe Israel kwa mazishi.
Mateka na miili ya wale waliouawa iko Khan Yunis pamoja na viongozi waliobaki wa Hamas. Anaamini Hamas itawatumia kama ngao za kibinadamu. Pia anaamini hakutakuwa na kurudi nyuma mara tu vita vya ardhini na angani vitakapoanza tena.
Mwandishi anasema jeshi la Israel halina dira ya hatua inayofuata, kwani eneo hilo limejaa raia ambao hawana uhusiano wowote na Hamas, hawana makazi na hawana matumaini ya kupata nafuu kutokana na mashambulio.
Umoja wa Mataifa unahofia kuenea kwa magonjwa ya mlipuko. Mwandishi anaeleza - kwa sababu hiyo, Israel inaweza kuwa na wiki mbili tu kukamilisha kazi yake, lakini hizo hazitotosha.
Mwandishi anashauri kupunguza matarajio kwa kampeni hiyo ya kijeshi, kwani kufikia ushindi kamili katika mazingira haya ni jambo gumu.
'Kwa manufaa ya nchi, lazima tubadili uongozi'

Chanzo cha picha, REUTERS
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika gazeti la "Jerusalem Post" kuna makala ya mwandishi Mark Simon yenye anuani: "Kwa manufaa ya nchi, lazima tubadili uongozi wetu."
Mwandishi anaanza makala yake kwa kusema miezi miwili imepita tangu tukio la kigaidi, watu anaowajua bado wanajaribu kupambana na kile kilichotokea.
Lakini hatupaswi kuacha matukio hayo yatuendeshe, uzoefu unaonyesha kufanya maamuzi chini ya shinikizo husababisha kutofanya maamuzi bora.
Mwandishi anasema kuna haja ya kuwa na mpango wa mpito wa kitaifa - kwani kura za maoni zinaonyesha watu wa Israel wanataka kuishinda Hamas na kuanza kuponya majeraha ya nchi hiyo.
Kutakuwa na wakati wa kuchambua makosa, lakini hii ni kazi iliyoahirishwa. Kazi ya sasa, ni kuwaokoa mateka, kuwaondoa Hamas, na kupanga mchakato wa kuliponya taifa.
Anasema ameishi Israel tangu 1988 na kushiriki katika chaguzi zaidi ya mara moja, na alipiga kura kwa Chama cha Likud katika chaguzi nyingi, lakini sasa hataweza kufanya hivyo kwa dhamiri safi.
Anaeleza ingawa Benjamin Netanyahu si mkamilifu, amefanya mambo mengi makubwa kwa Israel, lakini yeye, kama wengine wengi, anataka Netanyahu aondoke madarakani.
Mwandishi anaendelea kusema, “ikiwa Netanyahu angenisikiliza, ningemnong’oneza hivi: ‘Bibi (jina la utani la Netanyahu), umefanya mengi kwa ajili ya nchi yetu, na umekaa madarakani kwa muda mrefu kuliko mtu yeyote lakini sasa ni wakati wa mabadiliko kwa ajili ya taifa.'
Mwandishi anaamini pamoja na kuthamini alichokifanya Netanyahu lakini si yeye pekee mwenye uwezo wa kuongoza nchi hiyo na kuondoka kwake kutakuwa na manufaa kwa taifa na chama chake.
Mwandishi wa makala hiyo anatarajia Netanyahu kutangaza uchaguzi mpya ambao hatakuwa mmoja wa wagombea na atastaafu maisha ya kisiasa - baada ya kumalizika kwa vita na kuondolewa kwa Hamas,
Anaamini iwapo Netanyahu atafanya hivyo, itamsaidia kukabiliana vyema na matatizo yake ya mahakamani. Anahitimisha makala kwa kusema, "mpira uko kwa Netanyahu, kuamua iwapo Israel itasonga mbele au kurudi nyuma kwenye mtego wa machafuko."
'Lazima tupaze sauti kwa ajili ya Palestina'

Chanzo cha picha, REUTERS
Katika gazeti la Uingereza The Guardian, mwandishi mashuhuri wa Misri, Ahdaf Soueif - makala yake yenye anuani, “Hapa Misri, ukiandamana waweza kufungwa lakini lazima tupaze sauti kwa ajili ya majirani zetu wa Palestina.”
Anaanza makala yake kwa kusema: “Mbele ya makao makuu ya Umoja wa Waandishi wa Habari huko Cairo, mwanamke mmoja aliinua bendera siku ya Alhamisi yenye picha ya watoto wanane.
Watoto wote walikuwa wameaga dunia. Mwanamke aliyekuwa karibu naye alikuwa amemshika mtoto wake mchanga, akipiga kelele, 'Fungua Kivuko cha Rafah.'
Idadi ya waandamanaji ilikuwa takriban 100. Soueif anasema idadi ya washiriki ni ndogo sana ikilinganishwa na maelfu ya waandamanaji wanaojitokeza katika majiji makubwa kote ulimwenguni.
Mwandishi anahusisha sababu ya idadi ndogo ya washiriki na marufuku ya maandamano iliyowekwa nchini Misri - tangu Novemba 2013.
Walikuwa wakiandamana kwa ajili ya Gaza na wakati huo huo wakidai haki ya kuandamana, na nyimbo zao ziliangazia kinachozungumzwa majumbani na mitaani.
Anasema mitandao ya kijamii inaakisi hisia za kweli za Wamisri. Picha zinazotoka Gaza zinasambaa kote TikTok na Instagram kama moto wa nyika.
Maandamano mengine ambayo yanaakisi kinachotokea ni pamoja na madereva wa teksi za Uber - huzima mita zao wanapowachukua abiria wa Kipalestina.
Misaada hutiririka kwenye vituo maalumu vilivyoanzishwa kwa ajili yao, licha ya hali ngumu ya kiuchumi. Ombi la kutoa makazi kwa familia tatu zilizoweza kuondoka Gaza lilipokelewa ndani ya dakika chache.
Ahdad anasema: “Kwa miaka 16, tumeelemewa na hisia ya hatia kwa sababu ya ushiriki wa Misri. Kwa miaka 16, Misri ilisimamia kivuko cha Rafah kwa kutii sera ya Israeli.”
Mwandishi anasema, katika kila nchi ya Kiarabu ambapo watu wanaandamana kudai haki zao, pia wanadai haki za Wapalestina. Wanajua haki za Wapalestina haziwezi kutenganishwa na haki za raia wengine wa ulimwengu wa Kiarabu.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












