Jinsi tikitimaji lilivyogeuka kuwa nembo ya Palestina

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Selin Girit
- Nafasi, BBC
"Palestina ambako ni uhalifu kupeperusha bendera ya Palestina, vipande vya matikiti maji hutumiwa kuonesha uasi dhidi ya vikosi vya Israel kwa rangi yake nyekundu, nyeusi, nyeupe na kijani za bendera ya Palestina."
Ni maneno katika mashairi ya "Ode to the Watermelon," ya mshairi wa Marekani, Aracelis Girmay, yakielezea matumizi ya tundo hilo katika harakati za Palestina.
Rangi nyekundu, nyeusi, nyeupe na kijani sio tu rangi za tikiti maji lakini pia za bendera ya Palestina, na nembo hiyo inaweza kuonekana kote ulimwenguni katika maandamano ya kuwaunga mkono na katika machapisho ya mitandao ya kijamii huku Israel ikiendelea kuivamia Gaza.
Lakini kuna historia nyuma ya sitiari ya tikitimaji.
Baada ya vita vya Waarabu na Israel vya 1967, Israel ilipochukua udhibiti wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ilipiga marufuku kubeba alama za kitaifa za Palestina kama bendera na rangi zake katika maeneo yaliyotekwa.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Ikawa ni kosa la jinai kubeba bendera, badala yake Wapalestina walianza kutumia vipande vya matikiti maji kama aina ya upinzani.
Baada ya Israel na Wapalestina kutia saini mfululizo wa mikataba ya amani - ujuulikanao kama Mkataba wa Oslo mwaka 1993, bendera hiyo ilitambuliwa kuwa ya Mamlaka ya Palestina, mamlaka iliyoundwa kusimamia Gaza na sehemu za Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
"Katika Ukanda wa Gaza, ambako wakati fulani vijana walikamatwa kwa kubeba matikiti maji yaliyokatwakatwa - kwa kuonyesha rangi nyekundu, nyeusi na kijani za Palestina - leo askari wamesimama pembeni, wakati maandamano yanasonga mbele yakipeperusha bendera iliyowahi kupigwa marufuku huko nyuma," aliripoti mwandishi wa gazeti la The New York, John Kifner baada ya kutiwa saini Mkataba wa Oslo.
Miezi kadhaa baadaye, Disemba 1993, gazeti hilo lilibainisha kuwa madai ya kukamatwa vijana kwa kubeba matikiti maji hayakuweza kuthibitishwa, ingawa taarifa iliongeza "msemaji wa Serikali ya Israel, alipoulizwa, alisema hawezi kukataa kwamba matukio kama hayo huenda yalitokea."

Chanzo cha picha, INSTAGRAM/KHALED HOURANI
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu wakati huo, wanaharakati wameendelea kuunda sanaa za kutumia tikiti maji kuonyesha mshikamano na Wapalestina.
Moja ya kazi za sanaa ambayo ni maarufu ni ya Khaled Hourani. 2007 alichora kipande cha tikiti maji kwa ajili ya kitabu kiitwacho Subjective Atlas of Palestine.
Mchoro huo unaoitwa Hadithi ya Tikitimaji, ulisafiri kote ulimwenguni, na ukapata umaarufu mkubwa wakati wa mzozo wa Israel na Hamas wa Mei 2021.
Mfano mwingine ni mwezi Januari, pale Waziri wa Usalama wa Israel, Itamar Ben Gvir, alipowaagiza polisi kuziondoa bendera za Palestina kwenye maeneo ya umma na kusema kuzipeperusha ni "kuunga mkono ugaidi," picha za matikiti maji zilionekana wakati wa maandamano dhidi ya Israel.
Sheria za Israel haziharamishi bendera za Palestina lakini polisi na wanajeshi wana haki ya kuziondoa ikiwa wanaona kuna tishio kwa utulivu wa umma.
Katika maandamano mjini Jerusalem mwezi Julai, waandamanaji wa Israel walishikilia mabango yenye rangi za bendera ya Palestina pamoja na tikiti maji au neno "uhuru."
Mwezi Agosti, kundi la waandamanaji walivaa fulana zenye michoro ya tikitimaji walipokusanyika Tel Aviv kupinga mipango ya mageuzi ya mahakama ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Hivi karibuni matikiti maji yameonekana kwenye mitandao ya kijamii kupinga vita vya Gaza. Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanachapisha tikiti maji badala ya bendera za Palestina kwa kuhofia akaunti au video zao zinaweza kuzuiwa na mitandao ya kijamii.
Watumiaji wanaounga mkono Palestina siku za nyuma waliwahi kuituhumu Instagram kuzuia baadhi ya machapisho. Lakini Mwandishi wa Habari wa BBC Joe Tidy anasema hakuna ushahidi kwamba hayo yanafanyika siku hizi.
"Haionekani kuwa kuna njama yoyote ya kuwapiga marufuku watumiaji kuchapisha machapisho yanayounga mkono Palestina," anasema.
"Watu wanatumia picha za tikitimaji kwenye mitandao ya kijamii, lakini pia wanatumia kwa uhuru bendera ya Palestina na kuandika kwa uwazi kuhusu mzozo huo."
Tikiti maji limechukuliwa kuwa alama ya kisiasa kwa miongo kadhaa huko Palestina, haswa wakati wa uasi wa kwanza wa Palestina dhidi ya Israel na maasi yaliyofuatia.
Leo hii tikitimaji sio tu chakula maarufu katika eneo hilo, pia ni sitiari yenye nguvu kwa vizazi vya Wapalestina na wale wanaounga mkono mapambano yao.















