The Lion's Den: Kundi jipya la wa Kipalestina linaokabiliana na uvamizi wa Israel

ggg

Chanzo cha picha, AFP

Mvutano na ghasia kati ya majeshi ya Israel na Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Jerusalem Mashariki umeongezeka tangu mwanzini mwa mwaka huu, huku kukiwa na kundi moja la Wapalestina lililojipatia umaarufu: the Lion's Den (Arin al Usud, kwa Kiarabu).

Wanamgambo hao wapya, ambao walizuka katika Mji Mkongwe wa Nablus kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, wanajulikana kuwa wanahusika na mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Israel na walowezi.

Wanachama na wafuasi wake ni Wapalestina vijana, ambao wanadai kuwa juu ya mirengo ya jadi ambayo imeunda siasa za Palestina katika miongo ya hivi karibuni.

Lakini je kundi hili ni wakina nani na uwepo wao una maana kiasi gani?

"Vijana wa Kipalestina waliochukizwa"

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwezi Februari, wanajeshi wa Israel waliwaua Wapalestina 11, sita kati yao wakiwa wanachama wa The Lion's Den.

"The Lion's Den ni kundi la vijana, Wapalestina waliochukizwa na wenye hasira, wengi wao wakiwa katika umri wa miaka 20, ambao si sehemu ya mirengo yoyote ya kisiasa iliyopo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan au Gaza na ambao kimsingi wamejikita katika kupambana na uvamizi wa Israel," Anasema Ibrahim Jibril Dalalsha, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Horizon cha Mafunzo ya Sera, chenye makao yake makuu katika mji wa Ramallah wa Ukingo wa Magharibi.

Kundi hilo lenye silaha linafanya kazi zaidi ya yote katika mji wa Nablus, hasa katika kitongoji cha al Yasmina, ambapo wameweza kuajiri makumi ya vijana katika miezi ya hivi karibuni.

Ingawa wanamgambo hawana uhusiano rasmi na kundi lolote la kisiasa lililopo, baadhi ya wanachama wana misimamo ya hapo awali ya kisiasa, kulingana na wataalamu.

"Hao ni kundi lisiloegemea upande wowote, wanafanya kazi kama kundi moja la wanamgambo, ingawa baadhi yao wamejihusisha na vikundi vingine kabla ya "The Lion's Den, kama vile Islamic Jihad au Al-Aqsa Martyrs Brigades, Hamas au Fatah," anafafanua Dana el. Kurd, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Richmond, kilichopo Virginia (Marekani).

Lilianzaje?

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mama wa mmoja wa Wapalestina waliouawa na wanajeshi wa Israel.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika kuanzishwa kwake, mnamo Februari 2022, kikundi hicho kiliitwa Kikosi cha Nablus. Wakati huo kulikuwa na wanamgambo 10, wakiongozwa na Kikosi cha Jenin, wanamgambo wanaofanya kazi katika kambi ya wakimbizi yenye jina kama hilo.

Mnamo Agosti 2022, wanajeshi wa Israeli walivamia nyumba huko Nablus na kuwaua wapiganaji wao watatu, akiwemo Ibrahim al-Nablusi, mwenye umri wa miaka 18 anayejulikana kama Simba wa Nablus. Mauaji yake yalichangia katika uhamasishaji kwa kiasi kikubwa.

Inaaminika The Lion's Den's walionekana kwa mara ya kwanza msimu wa joto uliopita, wakati wa kutoa heshima mjini Nablus kuwaenzi wapiganaji wake waliouawa na vikosi vya Israel.

Mwanzoni mwa 2023, baadhi ya wanachama wake wakuu walikamatwa au kuuawa na jeshi la Israeli, wote wakishutumiwa kufanya mashambulizi dhidi ya malengo ya Israeli.

Picha na video za wanamgambo hao zilionekana kwenye mitandao yote ya kijamii, haswa kwenye TikTok. Miezi kadhaa baadaye, makumi ya watu wenye silaha waliojifunika nyuso zao waliandamana kwenye vichochoro vya Mji Mkongwe wa Nablus, jambo ambalo lilihusu hasa Mamlaka ya Palestina na idara za usalama za Israel.

"Kuongezeka kwa kutokujali kwa Israeli, ukandamizaji, shughuli za makazi na kudhoofisha mwitikio wa kimataifa na kikanda, pamoja na mkwamo wa kisiasa unaoendelea, [mambo haya yote] yamehimiza kuundwa kwa kundi hili," anasema. Dana wa Kurd.

ggg

Je! linapata uungwaji mkono mkubwa?

Kundi hilo limeweza kuteka mawazo ya vijana wa Kipalestina "wanaokataa hali iliyopo na siasa za kizamani ambazo Fatah na Hamas wanawakilisha," kulingana na Wakurdi, na kuna ushahidi kwamba kundi hilo linaungwa mkono mkubwa miongoni mwa Wapalestina.

Kulingana na utafiti wa Desemba uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Sera na Kura za Wapalestina miongoni mwa wakazi wa Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, zaidi ya 70% wanaunga mkono uundaji wa makundi huru yenye silaha kama vile the Lion's Den.

Kukakaa kwa uongozi wa Wapalestina kwa muda mrefu madarakani ni sababu mojawapo ya vijana wa Palestina kuvutiwa na kundi hili jipya la upinzani wenye silaha, kulingana na wachambuzi.

Wengi wa wanachama wake wamejitenga na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina.

"Wanaamini kuwa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina imefilisika kisiasa na haiwezi kupata uhuru wa kisiasa kwa njia za amani. Kwa hiyo, wanahisi kuwa mapigano kutoka kwa upinzani ndiyo yatakayoleta suluhu la mzozo," anasema Ibrahim Dalalsha.

Kundi hilo pia ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii. Mamia ya Wapalestina waliitikia ombi walilotuma kupitia chaneli ya telegram ya Lion's Den, ambapo wana wafuasi zaidi ya 130,000, walipowataka waliojisajili kupanda juu ya paa na kupiga takbir (tangazo la ukuu wa Mungu) kusimama kwa mshikamano na wanamgambo wanaoshambulia maeneo ya Israel.

Katika majimbo yote ya Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu, Wapalestina vijana waliimba kauli mbiu: "Lair haijashindwa."

ggg

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mwanamgambo akifyatua bunduki kwenye mazishi ya mmoja wa wanakikundi.

Je, uhusiano na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina uko vipi?

Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina (PNA) ni chombo kinachosimamia maeneo huru ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi, kama ilivyoanzishwa na Makubaliano ya Amani ya Oslo kati ya Israeli na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PLO).

Majiji na miji ya Palestina inatawaliwa zaidi na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina, ambayo inatawaliwa na kundi lisilo la kidini la Fatah. Kikundi tofauti, Hamas, kinadhibiti Ukanda wa Gaza na hakina umaarufu katika Ukingo wa Magharibi.

Vijana wengi wa Kipalestina wanaopigana pamoja na makundi haya mapya yenye silaha hawakuwa wamezaliwa hata wakati Mkataba wa Oslo ulipotiwa saini mwaka 1993.

"Viongozi wakuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina na chama tawala cha Fatah hawafurahishwi na kundi hilo kwa sababu nyingi," anasema Dalalsha, ambaye anaamini kuwa "uamuzi wa kimkakati umefanywa kujaribu kushirikiana na kundi hilo badala ya kulisambaratisha nguvu".

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uvamizi karibu na moja ya makazi ya Lion's Den ulizua mapigano katika soko hili la Nablus Old City.

Duru zingine zinasema kuwa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina imejaribu kushawishi kundi hilo kuachana na wanamgambo wenye silaha na kujiunga na huduma za usalama za Palestina.

Walifanikiwa kuwashinda baadhi ya wanachama, lakini viongozi wa kikundi hicho walikataa kukabidhi silaha zao, wakisisitiza kuwa wataendelea kupambana hadi mwisho.

"Baadhi ya wanachama wa the Lion's Den wameikosoa, lakini wanajiepusha kuingia kwenye mzozo na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina," anasema Ibrahim Dalalsha.

"Kwenda kinyume na PNA kunawaweka kwenye mzozo wa moja kwa moja, kama sio na umma mzima wa Palestina, basi kwa sehemu kubwa. Nadhani wanajaribu kuepusha hilo," anaongeza mkurugenzi wa Kituo cha Horizon.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maficho ambayo washiriki wa the Lion's Den walikimbilia Nablus.

Je, Israeli wanalionaje?

Israel inaliona kundi la the Lion's Den kama "shirika la kigaidi" .

Mwezi Februari mwaka huu, vikosi vya usalama vya Israel viliingia mjini Nablus na kuwaua Wapalestina 11, sita kati yao wakiwa wanachama wa kundi hilo, kwa mujibu wa chapisho kwenye chaneli yake ya Telegram.

Baada ya uvamizi huo uliochukua muda wa saa nne, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilidai kuwa limezidisha operesheni hiyo baada ya watu wenye silaha wa Kipalestina kuwafyatulia risasi wanajeshi wao.

"Tuliona tishio hilo na tukalazimika kuingia ili kumaliza kazi," msemaji wa IDF Luteni Kanali Richard Hecht aliwaambia waandishi wa habari.

Israel hivi karibuni iliziba maeneo kadhaa karibu na Nablus na Jerusalem mashariki kwa vizuizi vya mchanga na saruji.

"Jibu la Israeli limekuwa kali sana," anakubali Dana el Kurd, "lakini [the Lion's Den] litaendelea kuwa na ushawishi, na linaweza kuzalisha makundi mengine au nia ya kujiunga nao."

Kulingana na Ibrahim Dalalsha, wanaweza pia kushawishi siasa za maeneo ya Palestina.

"Si rahisi kwao kufikia lengo lao kubwa, ambalo ni ukombozi na mwisho wa uvamizi. Lakini ninaamini kuwa kuwepo kwao na shughuli zao kunasababisha mvurugano mkubwa na ni changamoto kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina na Waisraeli," alisema mtaalam.