Waziri wa mrengo mkali wa Israel atembelea eneo la msikiti wa Al Aqsa, Wapalestina walaani

Waziri mpya wa usalama wa taifa wa mrengo mkali wa kulia wa Israel Itamar Ben-Gvir alizuru kwa muda mfupi eneo la msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem siku ya Jumanne

Moja kwa moja

  1. Tarehe ya kuzikwa kwa mkongwe wa mwisho wa vita vya pili vya Dunia (WW2) wa DR Congo yapangwa

    w

    Chanzo cha picha, AFP

    Mkongwe wa mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Koplo Albert Kunyuku, atazikwa Ijumaa ijayo, kwa mujibu wa mtayarishaji wa filamu kuhusu maisha yake José Adolphe Voto.

    Koplo Kunyuku alifariki tarehe 25 Novemba mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 100. Alikuwa miongoni mwa wanajeshi 25,000 wa Jeshi la Ubelgiji la Congo, La Force Publique, waliotumwa kupigana pamoja na wanajeshi wa Ubelgiji wakati wa vita.

    Alitunukiwa Juni mwaka jana na Mfalme Philippe wa Ubelgiji katika hafla ya kina wakati wa ziara ya kwanza ya mfalme huyo katika nchi hiyo ya Kiafrika.

  2. Ghana na Morocco yaweka vikwazo vya Covid kwa wasafiri kutoka China,

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ghana na Morocco zimekuwa nchi za kwanza barani Afrika kuweka vikwazo vya usafiri kwa abiria kutoka China kutokana na wasiwasi wa virusi vya corona.

    Kuanzia Jumanne, Morocco imepiga marufuku wasafiri kutoka China bila kujali utaifa wao hadi ilani nyingine.

    Wizara ya mambo ya nje inasema hatua hiyo inalenga kuzuia ongezeko la maambukizi nchini.

    Vizuizi vya Ghana vitaanza kutumika Ijumaa.

    Hatua hizo zinakuja baada ya Uchina kuacha ghafla udhibiti wake wa Covid-19 mnamo Desemba mwaka jana.

    Nchi nyingine nje ya Afrika pia zimeweka vikwazo. Kwa mfano, abiria wanaowasili Uingereza kutoka China sasa wanapaswa kutoa kipimo hasi cha Covid kabla ya kupanda ndege.

    Marekani inawapima watu wanapowasili. Nchi zinazopanga kuwapima wasafiri zinasema sera hiyo itasaidia kutambua data mpya zinazotia wasiwasi mapema na kuzuia kuongezeka kwa visa vya virusi.

    Ghana inasema abiria kutoka China watapimwa katika uwanja wa ndege bila malipo na lazima pia wawasilishe matokeo ya vipimo hasi saa 48 kabla ya kuwasili.

    Wataalam wa afya wa kimataifa wamesema kuwa kuondolewa kwa vizuizi nchini China kumesababisha Covid-19 kuenea kwa kasi zaidi.

    Lakini wizara ya mambo ya nje ya Beijing imesema sheria za corona zinapaswa kuletwa tu kwa msingi wa "kisayansi" na kuzishutumu nchi za Magharibi na vyombo vya habari kwa "kudanganya" hali hiyo.

  3. Mwanajeshi wa Uganda awaua wenzake watatu nchini Somalia

    w

    Chanzo cha picha, AFP

    Uchunguzi umeanza katika mazingira ambapo askari wa Uganda chini ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Atmis) aliwapiga risasi wenzake watatu na kuwaua huko Mogadishu Jumatatu asubuhi.

    Ufyatuaji risasi huo ulifanyika katika makao makuu ya kikosi cha jeshi la Uganda. Msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulaigye, alithibitisha tukio hilo kwa BBC na kukamatwa kwa mwanajeshi huyo.

    Inasemekana kuwa alivamia na kumpiga risasi muathiriwa wake wa kwanza kifuani. Wanajeshi wengine hapo awali walidhani kuwa kambi yao ilikuwa imeshambuliwa. Mwathiriwa wa pili alipigwa risasi tatu kichwani alipokuwa akijaribu kujua kinachoendelea.

    Askari wa tatu alipigwa risasi ya mgongoni alipokuwa akijaribu kukimbia. Milio ya risasi ilikoma tu wakati afisa aliponyanyua na kumpokonya mpiga risasi silaha.

    Hili ni tukio la kwanza katika miaka kadhaa nchini Somalia linalohusisha wanajeshi wa Uganda.

    Tukio kama hilo lilitokea mnamo 2019 wakati nahodha wa Uganda alijiua baada ya kumpiga risasi mwenzake na kumuua.

  4. Waziri wa mrengo mkali Israel atembelea eneo la msikiti wa Al Aqsa, Wapalestina walaani

    w

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri mpya wa usalama wa taifa wa mrengo mkali wa kulia wa Israel Itamar Ben-Gvir alizuru kwa muda mfupi eneo la msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem siku ya Jumanne, eneo ambalo pia linaheshimiwa na Wayahudi, na kusababisha kulaaniwa kutoka kwa Wapalestina na nchi jirani ya Jordan.

    "Hekalu la Mlima liko wazi kwa wote," Ben-Gvir alisema kwenye Twitter, akitumia jina la Kiyahudi kwa eneo hilo.

    Picha za video zilimuonyesha akitembea pembezoni mwa boma, akiwa amezungukwa ulinzi mzito.

    Afisa mmoja wa Israel alisema ziara ya Ben Gvir ya dakika 15 katika eneo la Al Aqsa ilizingatia kile kinachoitwa mpangilio wa hali ilivyo, wa miongo kadhaa iliyopita, ambao unawaruhusu wasio Waislamu kuzuru kwa sharti la kutoswali.

    Kujiunga kwa Ben-Gvir, kiongozi wa chama cha Jewish Power, kujiunga na muungano wa kidini-kitaifa chini ya Waziri Mkuu aliyechaguliwa tena Benjamin Netanyahu kumezidisha hasira ya Wapalestina kuhusu juhudi zao za muda mrefu za kupata taifa.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ilisema "inalaani vikali kuvamiwa kwa msikiti wa Al-Aqsa na waziri mwenye itikadi kali Ben-Gvir na inaona kuwa ni uchochezi usio na kifani na ongezeko la hatari la mzozo".

    Msemaji wa Hamas, kundi la Kiislamu la Palestina ambalo linakataa kuishi pamoja na Israel, alisema kuhusu ziara ya Ben-Gvir: "Kuendelea kwa tabia hii kutazileta pande zote karibu na mzozo mkubwa."

    Mvutano kati yake na Israel ambao ulizidi kuwa ghasia katika eneo hilo mnamo Mei 2021 ulishuhudia Hamas wakirusha makombora kuelekea Jerusalem, na kusababisha mzozo wa siku 11 na Israel.

    Ziara ya mwaka 2000 ya kiongozi wa mrengo wa kulia wa Israel Ariel Sharon, kiongozi wa upinzani wakati huo, iliwakasirisha Wapalestina. Ghasia zilizofuata ziliongezeka na kuwa maasi ya pili ya Wapalestina, au maarufu intifada.

    Jumba la Al Aqsa, linalojulikana kwa Waislamu kama Patakatifu, ni eneo la tatu kwa Uislamu kwa utakatifu. Pia ni eneo takatifu zaidi la Uyahudi, mabaki ya mahekalu mawili ya kale ya imani.

  5. Miili 28 ya watu waliopigwa risasi na kuuawa yapatikana Burkina Faso

    m

    Mamlaka ya nchini Burkina Faso imeanzisha uchunguzi kuhusu mazingira ya vifo vya watu 28 ambao miili yao ilipatikana katika mji wa kaskazini-magharibi wa Nouna.

    Katika taarifa ya serikali ilisema mauaji hayo yaligunduliwa usiku wa tarehe 30 Disemba na kulaani "vurugu zisizokubalika".

    Shirika la habari la Reuters limewanukuu waendesha mashitaka wakisema kuwa waathiriwa waliuawa kwa kupigwa risasi, lakini hakukuwa na viashiria vya wahusika wa mauaji au kitu kilichowachochea kufanya shambulizi hilo.

    Mamlaka imewataka watu kuwa watulivu kusubiri matokeo ya uchunguzi.

    "Tukio hili linatokea wakati ambapo Burkina Faso imeanzisha operesheni ya uhamasishaji wa watu wote kwa umoja kuchukua hatua katika mapambano dhidi ya ugaidi," taarifa ya serikali ilisema.

    Nchi hiyo ya Afrika Magharibi inapambana na waasi wa Kiislamu ambapo tayari karibu watu milioni mbili wamekimbia makazi yao, na kusababisha mapinduzi mawili ya kijeshi ndani ya mwaka.

  6. Marekani yaiondoa Burkina Faso katika mpango wa biashara huru

    mm

    Chanzo cha picha, Reuters

    Burkina Faso imerudia ahadi yake ya kurejesha utawala wa kikatiba ndani ya miezi 18 kufuatia uamuzi wa Marekani kuiondoa katika mpango wake maalum wa kibiashara.

    Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani ilisema nchi hiyo imeshindwa kukidhi vigezo vya mpango wa AGOA(African Growth and Opportunity Act) kwa sababu ilifanya kazi kinyume na katiba.

    Kulikuwa na mapinduzi mawili ya kijeshi nchini Burkina Faso mwaka jana, yaliyosababishwa na kushindwa kwa mamlaka kudhibiti uasi unaozidi kuongezeka wa Kiislamu.

    Agoa inazipa fursa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kupeleka bidhaa nchini Marekani bila ushuru ili mradi zinatimiza masharti fulani yanayohitajika, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kidemokrasia.

    Unaweza kusoma zaidi:

    • Je Afrika imefaidika na mpango wa AGOA ?
    • Obama aing'oa Burundi kutoka kwenye AGOA
  7. Tembo wavamia nyumba na maghala, Msumbiji

    tembo

    Chanzo cha picha, AFP

    Kundi la tembo limevamia katikati ya mji, nchini Msumbiji na kuharibu nyumba, maghala na mazao.

    Maafisa katika jimbo la Safala walisema wanyama hao walikuwa wanatafuta maji kwani vyanzo vyao vya kawaida vimekauka kabisa.

    Walisema tembo hao wamekuwa wakiharibu kila kitu katika njia walizopita, na familia zingine zililazimika kuhama makazi yao na kuhamia kwingine.

    Uvamizi wa tembo ni tatizo linaloongezeka nchini Msumbiji na wanaondoka katika maeneo ya hifadhi kutafuta chakula na maji.

    Shirika la kitaifa la mazingira linasema karibu watu 100 wameuawa na wanyama pori katika miaka miwili iliyopita

  8. Burna Boy awaomba radhi mashabiki kwa kuchelewa kuingia jukwaani

    TH

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Nyota wa Afrobeat wa Nigeria Burna Boy ameomba msamaha kwa mashabiki baada ya kukosolewa kwa kuchelewa kuwatumbuiza kwenye tamasha ambalo alipanda jukwaani saa chache siku ya Jumatatu.

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, mwanamuziki huyo aliwalaumu waandaji kwa kuchelewa kwake katika Tamasha la Love Damini lililofanyika Lagos.

    "Muundo wa shirika na miundombinu haipo kwa ugumu wa mahitaji yangu ya sauti na utayarishaji," mwanamuziki huyo alisema.

    Aliongeza: "Ninaomba radhi kwa mashabiki wangu kwa jinsi ilivyokuwa, asante kwa kukaa na kustahimili dhoruba pamoja nami."

    Alisema atafanya kazi na wawekezaji kujenga miundombinu ya kiwango cha kimataifa katika tasnia ra ya burudani ya Nigeria.

    Mwimbaji huyo ni mmoja wa wanamuziki wa Kiafrika waliofanikiwa zaidi ulimwenguni.

    Soma pia

  9. Obasanjo azua hasira Nigeria kwa kuidhinisha mgombeaji wa urais

    th

    Chanzo cha picha, PETER OBI / FACEBOOK

    Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo yuko katikati ya dhoruba ya kisiasa baada ya kumuidhinisha mgombea urais wa upinzani Peter Obi kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao.

    Katika ujumbe wa kumuidhinisha, Bw Obasanjo alimtaja Bw Obi wa chama cha Labour kama "mwanafunzi" ambaye alikuwa na "makali juu ya wagombea wengine".

    Pia alielezea hali ya sasa ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kama "kuhama kutoka kwenye kikaangio hadi kwenye moto na kutoka kilele cha mlima hadi kwenye bonde".

    Bw Obasanjo aliiongoza Nigeria kati ya 1999 na 2007 kama mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha PDP.

    Lakini katika jibu la hasira, ofisi ya Rais Muhammadu Buhari ilisema kiongozi huyo wa zamani "alikuwa na wivu" na aliwakilisha "siku za giza za demokrasia ya Nigeria".

    Rais huyo wa zamani anadhani "yeye ndiye bora zaidi kuwahi kuiongoza Nigeria na hakutakuwa na mwingine bora zaidi yake", taarifa kutoka kwa msaidizi wa rais ilisema.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Peter Obi anaonekana kama mmoja wa wagombea watatu wakuu. Wengine ni Bola Ahmed Tinubu wa chama tawala cha APC na Abubakar Atiku wa chama cha upinzani cha PDP.

    Vyombo vya habaro vya ndani vinanukuu kampeni ya Bw Tinubu ikisema kuwa mgombea wao "hatakosa usingizi" kuhusu hatua hiyo ya Bw Obasanjo, huku kambi ya Bw Atiku ikisema "kuidhinishwa kwa mtu binafsi bila kujali kiwango cha juu hakusababishi ushindi katika uchaguzi".

    Kampeni zimeongezeka kabla ya uchaguzi mkuu.

  10. Tuzo za filamu za César zapiga marufuku wateule wanaochunguzwa kwa unyanyasaji wa kingono

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Toleo la Ufaransa la tuzo za Oscar limetangaza kuwa litapiga marufuku mtu yeyote anayekabiliwa na kifungo cha jela kwa unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa sherehe yake ya 2023.

    Tuzo za César - zinazotarajiwa kufanyika mwezi ujao - ilisema kuwa inafanya hivyo kwa heshima kwa wahasiriwa

    Ina maana sherehe hiyo itamtenga mwigizaji wa Ufaransa Sofiane Bennacer, ambaye anachunguzwa kwa tuhuma za ubakaji ambazo anakanusha.

    Kumekuwa na hofu ya maandamano iwapo Bw Bennacer angehudhuria.

    Inafuatia msukosuko wa mwaka wa 2020 wakati Roman Polanski, aliyetafutwa nchini Marekani kwa ubakaji, aliposhinda tuzo ya mkurugenzi bora.

    César Academy, ambayo hutunuku tuzo hizo, ilimwondoa Bw Bennacer kwenye orodha ya walioteuliwa mnamo Novemba, na kusema inazingatia mabadiliko ya sheria kuhusu kustahiki.

    Sasa imetangaza kwamba mtu yeyote anayechunguzwa kwa uhalifu wa kutumia nguvu unaoadhibiwa kwa kifungo - hasa ule wa asili ya ngono - atazuiwa kuhudhuria sherehe za mwaka huu tarehe 25 Februari.

    Sheria hiyo pia inatumika kwa mtu yeyote ambaye ametiwa hatiani kwa kosa hilo.

    Chuo kitapiga kura iwapo kitafanya mabadiliko ya kudumu kwa vigezo vya kustahiki.

    "Kwa heshima kwa wahasiriwa... imeamuliwa kutoangazia watu ambao wanaweza kuhusishwa na mahakama katika vitendo vya unyanyasaji," ilisema katika taarifa, ikibainisha kuwa hii ni pamoja na "wahasiriwa" katika kesi zinazochunguzwa.

  11. Damar Hamlin: Mchezo wa NFL wasimamishwa baada ya mchezaji kuanguka uwanjani

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mchezo wa Ligi ya Taifa ya Soka ya Marekani umesimamishwa baada ya mchezaji wa Buffalo Bills Damar Hamlin kuzimia wakati wa mchezo dhidi ya Cincinnati Bengals.

    Hamlin, 24, ambaye anacheza nafasi ya usalama, alianguka chini katika robo ya kwanza ya mchezo baada ya kugongana na Tee Higgins wa Bengal.

    Amepelekwa katika hospitali ya eneo hilo na yuko katika hali mbaya, NFL ilisema.

    Wachezaji walionekana wakitokwa na machozi na kukumbatiana katika maombi ya pamoja kwa ajili ya Hamlin.

    Ripota wa michezo nchini Joe Danneman aliandika kwenye Twitter kwamba aliambiwa Hamlin "ana mapigo ya moyo, lakini hapumui peke yake".

    Maafisa wa matibabu walikuwa wamempa CPR mchezaji huyo uwanjani mara moja kabla ya kumpeleka kwenye gari la wagonjwa, ESPN iliripoti.

    Waandaaji waliafikia uamuzi wa kusimamisha rasmi mchezo huo kwa usiku huo takriban saa moja baada ya tukio hilo. Michezo ya NFL mara chache husimamishwa kwa sababu ya jeraha.

    Chama cha wachezaji wa ligi hiyo kiliandika katika taarifa: "Tumekuwa tukiwasiliana na wachezaji wa Bills na Bengals, na NFL. Kitu pekee ambacho ni muhimu kwa wakati huu ni afya na ustawi wa Damar."

  12. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo tarehe 3 Januari 2023