Afrika ni mateka wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine - Zelensky

ggg

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameitaja Afrika kuwa ni "mateka" wa vita vya Urusi wakati akihutubia Umoja wa Afrika (AU) siku ya Jumatatu.

Uvamizi wa Urusi na kuzuia kwake mauzo ya nafaka nje ya Ukraine, kumesababisha uhaba wa nafaka na mbolea na kuweka mamilioni ya watu katika hatari ya njaa.

Mwenyekiti wa tume ya AU alisema kuna "haja ya mazungumzo ya dharura " ili kurejesha utulivu wa kimataifa.

Nchi za Magharibi zimeitaka Urusi kuachilia maduka makubwa ya nafaka ya Ukraine.

Vizuizi hivyo vimepelekea bei za vyakula kupanda.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Kwa hakika Afrika ni mateka... wa wale walioanzisha vita dhidi ya taifa letu", Zelensky alisema katika hotuba yake.

Alisema serikali yake ilikuwa inashiriki katika "mazungumzo magumu" ili kufungua akiba ya nafaka iliyonasa katika bandari za Bahari Nyeusi nchini Ukraine.

"Vita hivi vinaweza kuonekana kuwa mbali sana kwenu na kwa nchi zenu," aliiambia AU. "Lakini bei za vyakula ambazo zinapanda tayari zimeleta [vita] kwenye nyumba za mamilioni ya familia za Kiafrika."

Hotuba ya Zelensky ya AU inakuja karibu wiki 10 tangu alivyoomba kwa mara ya kwanza kuhutubia baraza la bara.

BBC inaelewa kuwa wakuu wa nchi 55 walialikwa kwenye kikao hicho cha mtandaoni, lakini ni wanne pekee waliohudhuria. Nchi zingine zilituma wawakilishi.

Nchi za Afrika zimegawanyika katika kukabiliana na vita vya Urusi nchini Ukraine. Mwezi Machi, nchi 17 za Afrika zilipiga kura za kutofungamana na upande wowote katika kura ya Umoja wa Mataifa ya kulaani uvamizi huo.

Lakini siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa AU Macky Sall alimshukuru Bw Zelensky kwa kuhutubia muungano huo.

Sall alisema kuwa "Afrika itaendelea kuheshimu sheria za kimataifa, utatuzi wa amani wa migogoro na uhuru wa biashara".

Hapo awali, AU haikutaka kuhutubiwa na Zelensky na haikubaliani kabisa na anachosema - wanataka mazungumzo kusuluhisha mzozo huo, kama wanavyofanya kila wakati.

Mapema mwezi huu, Sall alifanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Alimwambia Putin kwamba nchi za Kiafrika ni wahanga wasio na hatia wa vita vya Ukraine na Urusi inapaswa kusaidia kupunguza mateso yao.

DDD

Chanzo cha picha, Getty Images

Mapema Jumatatu, mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema kuhusu vizuizi vya Urusi : "Hii ni uhalifu wa kivita wa kweli, kwa hivyo siwezi kufikiria kuwa hii itadumu kwa muda mrefu zaidi."

Borrell alikutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg siku ya Jumatatu kujadili mzozo huo.

Alielezea hatua za Moscow kama "jaribio la makusudi la kutengeneza njaa duniani".

Alikataa madai ya Urusi kwamba mzozo wa sasa wa chakula ni matokeo ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya, akiongeza kuwa "hazikatazi" nchi zilizo nje ya EU kufanya biashara ya chakula na Urusi au mataifa mengine.

FFF

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna alisema "Urusi lazima iache kucheza na njaa duniani" inapotafuta kujiinua juu ya Magharibi.

"Kuacha vizuizi vya nafaka kuendelea kuwepo ni hatari kwa utulivu duniani," alisema.

Mkuu wa ofisi ya waziri mkuu wa Poland, Michal Dworczyk, alizungumza na waziri wa miundo mbinu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov kuhusu mabadiliko yatakayoharakisha ukaguzi wa malorio kwenye mpaka wa Poland na Ukraine ili kusaidia mauzo ya nafaka zaidi kutoka Ukraine.