Uhaba wa pesa wakwamisha teksi zinazopaa

Chanzo cha picha, Volocopter
- Author, Theo Leggett & Ben Morris
- Nafasi, BBC News World
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Mojawapo ya ubunifu katika Michezo ya Olimpiki ya Paris ya mwaka huu, ilipaswa kuwa ni huduma ya teksi za umeme zinazopaa.
Kampuni ya Volocopter ya Ujerumani, iliahidi teksi zake za umeme, zenye viti viwili, VoloCity, zitakuwa zikisafirisha abiria kuzunguka jiji hilo.
Lakini lengo lake la kuunda teksi hizo zisizo kelele wala uzalishaji wa hewa chafu halikutimia.
Na sasa matumaini yamewekwa kwa kampuni ya Geely ya China, ambayo iko kwenye mazungumzo ya kuchukua hisa 85% kutoka kwa Volocopter kwa malipo ya ufadhili dola za kimarekani milioni 95, kulingana na ripoti ya Bloomberg.
Kutokana na kukabiliwa na gharama kubwa ya kupata kibali kwa teksi hizo na kujenga uwezo wa utengenezaji, wawekezaji wengi wamejiondoa.
Kampuni zinazosuasua
Kampuni ya Uingereza ya Vertical Aerospace, ilianzishwa mwaka 2016 na mfanyabiashara Stephen Fitzpatrick, ambaye pia alianzisha OVO Energy.
Bwana Fitzpatrick ametoa madai makubwa teksi yake ya kupaa itakuwa "mara 100" salama na tulivu kuliko helikopta, kwa 20% ya gharama.
Kampuni hiyo imepata maendeleo. Baada ya kukamilisha mpango wa majaribio kwa njia ya rimoti, sasa imeanza kufanya majaribio ya rubani mapema mwaka huu.
Lakini kumekuwa na vikwazo vikubwa. Mwezi Agosti mwaka jana, majaribio ya kuruka bila rubani yalitatizika pale ilipoanguka wakati wa majaribio kwenye Uwanja wa Ndege wa Cotswold.

Chanzo cha picha, Vertical Aerospace
Mwezi Mei mmoja wa washirika wake wakuu, kampuni kubwa ya uhandisi Rolls Royce ilijiondoa katika makubaliano ya kusambaza injini za umeme za ndege hiyo.
Matamanio yanabaki kuwa makubwa. Vertical Aerospace inasema itawasilisha ndege 150 kwa wateja wake kufikia mwisho wa muongo huu.
Kufikia wakati huo, inatarajia pia kuwa na uwezo wa kuzalisha ndege nyingi kwa mwaka, na kuwa na uwezo na uwezo wa kufanya biashara.
Hata hivyo matatizo ya kifedha yamekuwa yakiongezeka. Fitzpatrick aliwekeza dola milioni 25 ya ziada katika kampuni yake mwezi Machi. Lakini dola milioni 25 zaidi, iliyotakiwa mwezi Agosti kama uwekezaji haikupatikana.
Maendeleo na Changamoto

Chanzo cha picha, Airbus
Katikati ya msukosuko huo, mradi mmoja wa Ulaya unaendelea kimya kimya, anasema Bjorn Fehrm, mhandisi wa angani na mhandisi wa ndege za kivita za majaribio za Jeshi la Wanahewa la Sweden.
Anasema mradi wa EVTOL unaoendelea wa Airbus huenda ukaendelea kuwepo. Unaitwa CityAirbus NextGen, ndege zao ni za viti vinne zina propela nane na inaweza kupaa umbali wa kilomita 80.
Pindi ndege zinazotengenezwa zitakuwa tayari, changamoto inayofuata itakuwa ni kuona ikiwa kuna soko litakalo wapa faida.
Safari za kwanza zinaweza kuwa kati ya viwanja vya ndege na katikati mwa miji. Lakini watapata pesa?
"Tatizo kubwa linapokuja suala la gharama ya kuendesha teksi hizi, ni rubani na betri. Unahitaji kubadilisha betri mara kadhaa kwa mwaka," anasema Fehrm.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












