Huenda ukaanza kutumia teksi inayopaa miaka mitatu inayokuja

Chanzo cha picha, Ethan Pines/The Forbers Collection
Kwa watu wengi wa umri fulani, wazo la teksi zinazoruka ama kupaa, kuwasafirisha watu kati ya miji, inawakumbusha filamu ya televisheni kwa jina The Jetsons.
Fulamu hii ya miaka ya 1960 inaonyesha familia moja iliyokuwa inaishi mjini ambapo wasafiri walikuwa wakienda kazini wa magari yanayoruka.
Miongo miwili ndani ya karne ya 21, ndoto za watengeneza kipindi cha cha The Jetsons zinakaribia kutimia.
Huku kampuni kama Uber na Boeing wakiwa wanajikita katika kutengeneza magari yanayoruka maarufu kama eVTOL (electric vertical take-off and landing), ripoti moja inatabiri kuwa ifikapo mwaka 2040, kutakuwa na magari 430,000 ya aina hiyo yatakayokuwa yakihudumu kote duniani.
Hii inajiri wakati ndege zisizo na rubani zinazotumika kusafirisha bidhaa zinaendelea kuundwa huku soko la dunia la ndege hizo lilikadiriwa kufikia thamani ya dola bilioni 5.6 ifikapo mwaka 2028.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kampuni ya Joby Aviation yenye makao yake huko California, iko mstari wa mbele kuunda teksi zinazoruka ikiwa hadi sasa imefanya zaidi ya majaribio 1,000 kwa teksi zake za eVTOL.
Ina matumaini kupata kibali kutoka kwa serikali ili kuanza huduma za biashara mwaka 2024.
Ndege hizo za Joby zinaweza kubeba abiria wanne na kuruka kwa kasi ya kilomita 322 kwa saa na kusafiri umbali wa kilomita 241.
"Tuna mpango wa kutoa huduma zetu karibu na maeneo watu wanaishi, wanafanya kazi, na wanataka kwenda," anasema Oliver Walkwer Jones, msemaji wa Joby.
"Tunashirikiana na mifumo mingine ya usafiri kuhakiksha kuwa huduma zetu zina uwiano kwa mfano na vituo vya treni, viwanja vya ndege na zinginezo."

Chanzo cha picha, Bradley Wentzel
Joby tayari imeshirikiana na kampuni ya huduma za kuegesha magari nchini Marekani Reef Technology, kwa lengo la kubadili paa za baadhi ya maeneo yao ya kuegesha kuwa vituo vya vya kutua.
Licha ya mtandao wa sehemu za kutua kwa ndege hizo kuoneka kuwa changamoto, mpango huo tayari unapata uungwaji mkono hasa kutoka miji kadhaa nchini Marekani.
Houston, Los Angeles, na Orlando tayari imetangaza mipango ya kubuni miundo msingi ya teksi zinazoruka na huduma zingine kama hizo.
Meya wa los Angeles Eric Garcetti anasema mapendekezo kwenye mji wake yatatoa mfano kuhusu vile serikali zingine za miji zinaweza hata kuboresha zaidi teknolojia hii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchini Uingereza mipango ya kujengwa kituo cha teksi zinazoruka huko Coventry karibu na uwanja wa raga na soka umeungwa mkono na serikali ya Uingereza.
Kikitarajiwa kuwa kituo cha kwanza duniani cha kutoa huduma za teksi zinazoruka na ndege za mizigo zisizo na rubani, kituo hicho kinajengwa na kampuni mshirika wa Hyundai kwa jina Urban Air Port.
Kampuni hiyo ina matumani kuwa kituo hicho kisichokuwa na gesi ya carbon kitanakiliwa kote duniani ili kupunguza misongamano ya magari barabarani na kupunguza hewa chafu kutoka kwa magari.
"Viwanja vya ndege kote duniani ni vikubwa, vinazalisha gesi chafu, vikiwa na barabara ya hadi umbali ya wa kilomita 1.2," anasema muasisi ya Urban Air Port, Ricky Sandhu. "Hii ni kwa sababu ya teknoljia ya jinsi ndege inavyo paa na inavyo tua.

Chanzo cha picha, Urban Air Port
Magari yanaweza kupaa kwa kuinuka na kutua kwa kushuka, na hivyo uwanja unaohitajika utakuwa wa aina mpya.
Wataalamu hata hivyo wanaona chamgoto kadhaa ambazo zinaweza kuwa kizingiti kwa teksi zinazoruka na viwanja vya kuhudumu.
Hii ni pamoja na umma kukubali, magari hayo kuundwa kwa wingi, miundo msingi na kubuniwa mfumo wa teknolojia ya juu wa kuendesha huduma hizo ni baadhi ya vizingiti kwa mujibu wa Jennifer Richter, wakili anayehusika na masuala ya sheria zinazohusu ndege zisizokuwa na rubani na teski zinazoruka mjini Washington DC.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini Ricky Sadhu anasema wasi wasi mkubwa ni kwamba uwekezaji kwenye vituo au viwanja vya kutua na miundomsingi mingine inaweza kuchelewewa ikilinganishwa na uwekezaji kwa magari yenyewe.
Anaongeza kuwa licha ya kuwepo changamoto, tayari kuna mahitaji ya vituo vya kutoa huduma kutoka miji kote duniani nchini Marekani , Ulaya na Asia.
"Tunatarajia kuona vituo 200 vya magari hayo katika kipindi cha miaka mitano inayokuja, lakini pia miji mikubwa huenda ikahitaji zaidi," aliongeza Bw Sadhu.














