Kwa Picha: Mji wa Goma baada ya mapigano kati ya M23 na FDRC

- Author, Robert Kiptoo
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, DR Congo
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Baada ya miezi kadhaa ya mapigano, waasi wa M23 sasa wanaudhibiti mji mkuu wa Goma, mji unaokaliwa na zaidi ya watu milioni mbili, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakati M23 walipowasili mjini Goma, hawakupata upinzani mkali kutoka kwa jeshi la serikali ya DRC. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 700 wameuawa tangu M23 kuingia Goma.
Aidha mamia ya wengine nao walijeruhiwa huku maelfu wakikimbilia maeneo mengine ya nchi jirani.
Mji huu ambao huwa na shughuli nyingi sasa umesalia mahame. Maduka mengi yamefungwa, shule, benki, ofisi za serikali na zile za mashirika yasiyo ya kiserikali zimefungwa.
Mji huu sasa kwa asilimia mia moja uko chini ya waasi wa M23 hasa baada ya wanajeshi wengi kujisalimisha na wengine wakitoroka na kuacha silaha zao na Magari ambayo sasa yanatumiwa na wapiganaji wa M23.
Jeshi la Congo lilistahili kuwalinda raia hao walitoroka mjini humo na hamna hata mmoja aliyesalia.

Katika barabara za mji, mabaki ya athari za vita yanaonekana yametapakaa kila mahali. Magwanda ya wanajeshi waliojisalimisha pia yametapakaa barabarani. Silaha na risasi zilizoachwa nyuma na wanajeshi wa serikali ya DRC zimejaa barabarani.

Ali Richard, mkaazi wa Goma ameiambia BBC kuwa wakati M23 walipoingia mjini humo, wanajeshi wengi walitoa mavazi yao rasmi na kuyatupa ili kuepuka ghadhabu kutoka kwa M23.
'' Wengi walitupa sare zao na bunduki na kukimbia na wengine nao walisikika wakisema kuwa wao hawataki vita. M23 wameokota bunduki zilizotupwa na M23, lakini nyingi zingali mikononi mwa raia'' alisema Ali.
Maafisa wa polisi wa serikali ya DRC nao wamegeuka kuwa raia wa kawaida huku wapiganaji wa kundi hilo wakishika doria katika barabara za mji, uwanja wa ndege na vituo vya mpakani pamoja na kushika doria.
Nje ya uwanja mkuu wa ndege, wakaazi wa eneo hilo wanaendelea kukadiria hasara, baada ya maeneo yao ya kibiashara na mali kuharibiwa.
Kituo kimoja cha mafuta na magari kadhaa yaliteketezwa katikia eneo hilo.

Uwanja mkuu wa ndege nao umesalia kufungwa na sasa wapiganaji wa M23 na wanajeshi wa SADC wanashika doria katika uwanja huo huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuwa huenda wanajeshi hao wa SADC wametimuliwa na M23.
Katika hospitali kuu mjini Goma, mamia ya watu wanaendelea kupokea matibabu, kutokana na majeraha ya risasi.
Afisa mkuu katika hospitali moja ya kibinafsi, ambaye jina lake tumelibana, amesema kuwa wamepokea zaidi ya majeruhiwa mia saba tangu vita hivyo kuanza na 20 kati yao wamefariki.
Wengi wa wanaofika katika hospitali hiyo wana majeraha ya risasi na wengine nao wamevunjika viungo.

Amesema kuwa visa vya ubakaji vimeongezeka na kuwa tayari wamepokea zaidi ya kesi kumi katika kipindi cha wiki moja tangu M23 kuuteka mji huo.
Nathaniel Ciro anasema alijeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limeanguka kwa jirani kulipuka. 'Nilikuwa nyumbani kwangu na mara tu bomu likalipuka kwa jirani wangu ambaye naye alijeruhiwa, na sasa amepoteza jicho lake. Jamaa wake wawili waliuawa kwenye mlipuko huo wa bomu'' alisema

Watu waliojeruhiwa wamefurika katika hospitali mjini humo na chumba cha kuhifadhia maiti kimejaa.
Hata hivyo waakazi wa mji huu wameanza kujitokeza kutoka maficho yao kutafuta chakula na maji na wengine wameanza kurejea baada ya kukimbilia maeneo mengine na nchi jirani

Shughuli za kibiashara nazo zimeathirika pakubwa huku benki zote, shule na ofisi za serikali zikiwa zimefungwa.
Ofisi ya aliyekuwa gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini sasa ni makao makuu ya kundi hilo huku makao makuu ya polisi yakibadilishwa na kuwa makao makuu ya jeshi la M23.
Katika mitaa miingi, maduka yalianza kufunguliwa tena siku ya Jumamosi lakini mengi yamesalia kufungwa.














