Jinsi mwanamke alivyowapata wazazi wake halisi Facebook baada ya miaka 40

Muda wa kusoma: Dakika 5

Tamona Mosridze alifikiri kwamba wazazi wake halisi wanaweza kuwa watu wengine. Akiwa na mawazo hayo, akashusha pumzi ndefu na kupiga namba ya simu.

Alitaka kumpata mwanamke ambaye anaweza kuwa mama yake halisi. Kwake, mawazo haya yalionekana kama ndoto mbaya.

Lakini kilichomshangaza Tamuna ni ile hali ya ubaridi na hasira ya yule mwanamke wa upande wa pili wa simu.

"Alianza kupiga kelele na kulia, akisema hakuwahi kupata mtoto na hataki kuzungumza nami," Tamona anasema.

"Majibu yake yalinishangaza zaidi kuliko yalivyonikasirisha."

"Nilikuwa tayari kwa lolote, lakini majibu yake yalikuwa zaidi ya vile ambavyo ningeweza kufikiria."

Tamona, mwenye umri wa miaka 40, alijua alipompigia simu mamake mnamo Agosti kwamba huenda hataki arudishwe maishani mwake.

Lakini Tamona hakukata tamaa kirahisi hivyo. Alitaka kujua jinsi alivyolelewa, na alichotaka kujua baba yake ni nani, siri ambayo mama yake pekee ndiye angeweza kumwambia.

Tamuna alianza kumtafuta mwaka wa 2016. Akiwa anasafisha nyumba ya mamake, alishangaa kupata cheti cha kuzaliwa. Jina la Tamuna liliandikwa kwenye nyaraka hiyo, lakini tarehe yake ya kuzaliwa haikuwa sahihi.

Hii ilimfanya ashuku kuwa anaweza kuwa mtoto wa kulea. Baada ya kufanya utafiti, alianzisha kikundi cha Facebook, "I'm Looking," kwa matumaini ya kupata wazazi wake wa kumzaa.

Pia alifichua ulanguzi wa watoto huko Georgia, na kubadilisha maisha ya makumi ya maelfu ya watu. Kwa miongo kadhaa, wazazi walidanganywa, wakidai watoto wao wamekufa, huku watoto wachanga wakiuzwa.

Tamuna, mwandishi wa habari ambaye ameunganisha mamia ya familia kupitia kazi yake, bado hajafichua siri ya maisha yake ya zamani.

Anadhani yeye pia huenda alitekwa nyara akiwa mtoto.

"Nilikuwa nashughulikia kesi hii kama mwandishi, lakini pia ilikuwa kusudio langu binafsi," anasema.

Alianza Msako huo kuelekea katika majira ya joto. Wakati huo, alipokea ujumbe kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Mtumaji huyo, anayeishi vijijini vya Georgia, alidai kuwa anamjua mwanamke ambaye alikuwa ameficha ujauzito wake na alijifungua huko Tbilisi mnamo Septemba 1984.

Tarehe ya kuzaliwa ambayo mtu huyu alichapisha ililingana na tarehe ya kuzaliwa ya Tamuna ambayo aliichapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Mwanaume huyu aliamini kuwa mwanamke huyu ndiye mama yake Tamuna. Jambo lingine muhimu ni kwamba pia alimpa Tamuna jina lake.

Tamuna alianza mara moja kumtafuta mtandaoni, lakini hakuweza kupata chochote, aliamua kutuma ombi kwenye mtandao wa Facebook kuwauliza watu kama kuna anayemfahamu.

Mwanamke mmoja alijibu haraka, akisema kwamba mwanamke aliyeficha ujauzito wake ni shangazi yake. Lakini alimwomba Tamuna aondoe chapisho hilo na akakubali kupimwa DNA.

Wakiwa wanasubiri majibu ya DNA, Tamuna aliwasiliana na mama yake.

Wiki moja baadaye, matokeo ya DNA yalitoka, yakithibitisha kwamba Tamuna na mwanamke huyo kwenye Facebook walikuwa binamu.

Kwa ushahidi huu, Tamuna aliweza kumshawishi mama yake kukiri ukweli na kufichua jina la baba yake. Jina la baba yake lilikuwa Gorkan Khoruwa.

"Miezi miwili ya kwanza ilikuwa ya kushangaza," anasema. "Sikuamini haya yote yaliyokuwa yakitokea. Sikuamini kuwa nilikuwa nimewapata."

Baada ya kupokea jina la Gorgon, Tamona alimpata haraka kwenye Facebook. Alibaini kuwa ni mfuasi wake Tamona kwenye mtandao huo wa kijamii.

Kazi ya Tamona katika kuunganisha familia inajulikana sana kote nchini Georgia.

Tamona alishangaa kwamba Gorgon alikuwa "kwenye orodha ya marafiki zake kwa miaka mitatu." Gorgon hakujua kuwa alikuwa sehemu ya hadithi ya Tamona.

Walipanga kukutana haraka huko Zugdidi, magharibi mwa Georgia, alikozaliwa, kilomita 260 kutoka nyumbani kwa Tamuna huko Tbilisi.

Tamuna, ambaye anakumbuka siku za nyuma, anasema alikuwa katika "mshtuko" wakati huo. Lakini anasema kwamba alipokaribia lango la bustani ya Gorgon, kinyume na matarajio yake, alihisi utulivu wa ajabu.

Mzee huyo aliyekuwa na umri wa miaka 72 alipofika, walikumbatiana, kisha wakasimama kwa muda na kutazamana kwa tabasamu.

Tamuna anasema, "Ilikuwa ajabu, aliponitazama, alijua mimi ni binti yake. Tulikuwa na hisia mseto sana"

Tamona alikuwa na maswali mengi na hakujua aanzie wapi. "Tuliketi tu, tukatazamana, na kujaribu kutafuta pa kuanzia," anasema.

Walipokuwa wakizungumza, waligundua kwamba walikuwa na mambo mengi ya kufanana.

Gorgan wakati mmoja alikuwa mcheza densi maarufu huko Georgia, na pia alifurahi kwamba binti za Tamuna (wajukuu zake) pia walipenda kucheza hivyo.

"Binti zangu wote wawili wanapenda kucheza dansi, na pia mke wangu," anasema huku akicheka.

Gorgon alialika familia yake yote nyumbani kwake kuonana na Tamuna, akimtambulisha kwa kundi kubwa la jamaa. Alikutana na kaka na dada zake, wajomba zake, wanawe na wakwe zake.

Kila mtu katika familia alikubali kwamba Tamuna anafanana sana na baba yake, "Kati ya watoto wake wote, nilifanana zaidi na baba yangu."

Walitumia jioni hiyo kukumbuka mambo yaliyopita, wakila chakula cha Kigeorgia, wakiimba nyimbo za Kigeorgia, na kucheza wakipiga kinanda aina ya accordion.

Baada ya kukutana na Tamuna na baba yake, swali moja bado lilibaki akilini mwake: Je, yeye, kama maelfu ya Wageorgia wengine, alitekwa nyara kutoka kwa mama yake wakati wa kuzaliwa na kuuzwa?

Kwa kuwa baba na mama yake walezi wamekufa, ameshindwa kupata majibu yoyote.

Hatimaye, mnamo Oktoba, Tamona alipata fursa ya kumuuliza mama yake halisi. Kituo cha televisheni cha Poland kilikuwa kikitengeneza filamu kuhusu Tamona na kumpeleka kukutana na mama yake. Mama yake alikubali kuongea naye faragha.

Tofauti na watu wengi ambao Tamuna aliwasaidia kuungana na familia zao, aligundua kwamba hakuwa ametekwa nyara akiwa mtoto.

Ni kwamba, mama yake alikuwa amemwacha na kuficha siri hiyo kwa miaka 40.

Wazazi wake hawakuwa na uhusiano na walikuwa pamoja kwa muda mfupi tu. Mama yake aliona aibu sana wakati huo na kuamua kuficha ujauzito wake.

Mnamo Septemba 1984, alisafiri kwenda Tbilisi kwa kisingizio cha upasuaji, lakini kwa kweli alimzaa binti yake huko na alibaki huko hadi mchakato wa kuasili wa Tamuna ukakamilika.

"Nilipogundua kuwa nimechukuliwa na mtu mwingine na nilikuwa nimekaa kwa siku kumi tu na mama yangu, nilihisi uchungu sana," Tamuna anasema kwa huzuni. "Ninajaribu kujizuia kufikiria hilo."

Tamuna anaamini kuwa haitakuwa haki kwa akina mama na baba wote ambao watoto wao wametekwa.

"Nikidanganya, hakuna atakayeamini wanachosema akina mama hawa," anaongeza.

Baadaye, mama yake alimwomba aondoke nyumbani na hawakuzungumza tena baada ya hapo.

"Je, niko tayari kupitia hatua hizi zote tena?" Kwa kweli, ndivyo nilivyofanya, nilijifunza mengi kuhusu familia yangu mpya."

Imetafsiriwa na Martha Saranga