'Turudishieni waume zetu' - Wanawake wa Urusi katika maandamano yasiyo ya kawaida

.
Maelezo ya picha, Wake wa wanajeshi wa akiba waliopelekwa vitani wanasema waume zao wametimiza wajibu wao vitani na wanataka warudi nyumbani

Katika chumba kilichopo ukingo wa Moscow, jambo lisilo la kawaida linaendelea.

Kikundi cha wanawake kinakosoa hadharani mamlaka ya Urusi. Waume zao ni miongoni mwa wanajeshi wa akiba 300,000 waliosajiliwa baada ya wito wa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa ajili ya vita vya Ukraine mnamo 2022.

Na wanataka waume zao warudi nyumbani.

"Ni lini waume zetu watazingatiwa kuwa wametimiza wajibu wao wa kijeshi?" anauliza Maria. "Wanaporudishwa wakiwa hawana mikono na miguu? Wakati hawawezi kufanya lolote kwa sababu wamegeuka kuwa mfano tu? Au tusubiri warudishwe kwenye majeneza?"

Wanawake hao walikutana kupitia mitandao ya kijamii na wameanzisha kikundi kiitwacho ‘The Way Home’. Wana maoni tofauti juu ya vita. Wengine wanadai kuunga mkono. Wengine wana shaka kuhusu "operesheni maalum ya kijeshi" ya Urusi.

Kinachoonekana kuwaunganisha ni imani kwamba wanajeshi waliochukuliwa wamefanya sehemu yao katika mapigano na wanapaswa kurejea nyumbani kwa familia zao.

Ni maoni ambayo mamlaka hayayashirikishi hadharani.

Huko Urusi kukosolewa hadharani kwa chochote kinachohusiana na vita huja na hatari yake. Wazungumzaji wengi huchagua maneno yao kwa uangalifu sana. Wanajua kuna msururu wa sheria zilizopo sasa nchini Urusi za kuwaadhibu wapinzani. Mfadhaiko wao hata hivyo, ingawa, ni dhahiri.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Kwa kuanzia tuliiamini serikali yetu," Antonina anasema. "Lakini je tuwaamini sasa hivi? Simwamini mtu yeyote."

Washiriki wa kikundi hicho wako hapa kushirikisha hadithi zao na diwani wa eneo hilo, Boris Nadezhdin. Amekuwa akikosoa "operesheni maalum ya kijeshi" tangu mwanzo.

Cha ajabu Bw Nadezhdin ni mmoja wa wakosoaji wachache wa serikali ambao wameruhusiwa kuonyeshwa kwenye televisheni ya taifa tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine. Yeye ni mgeni wa mara kwa mara kwenye vipindi vya mazungumzo vya TV.

Mwanasiasa huyo anashikilia kuwa vita hivyo vimeharibu umaarufu wa ndani wa Vladimir Putin.

"Putin alikuwa maarufu sana nchini Urusi kwa sababu baada ya miaka ya 1990 alileta utulivu na usalama," Bw Nadezhdin ananiambia. "Utulivu na usalama vilikuwa sababu kuu ya kumuunga mkono Putin. Sasa watu wengi zaidi tayari wameelewa kuwa utulivu na usalama umekamilika."

Wanawake wa Urusi wanaofanya kampeni ya kurudi kwa waume zao waliopelekwa vitani, watoto au kaka zao wamekuja kutoa maoni yao kutoka pande tofauti.

.
Maelezo ya picha, Boris Nadezhdin, ni mmoja wa wakosoaji wachache wa serikali ambao bado wanaruhusiwa kwenye TV ya kitaifa nchini Urusi.

Wafuasi wa Kremlin wanawaonyesha wanawake hao kama vibaraka wa Magharibi.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na tovuti ya habari ya Fontanka, Mbunge wa Urusi Andrei Kartapolov, ambaye anaongoza kamati ya ulinzi ya Duma ya Urusi, alidai kuwa wito huo ulichochewa na "maadui [wa Urusi]". Alionekana kupendekeza kwamba jeshi la Ukraine au CIA ndio walikuwa nyuma ya hilo.

Bw Kartapolov pia alizungumzia Vita vya Pili vya Dunia.

"Je, unaweza kufikiria ujumbe wa wake za wanajeshi kuja Kremlin wakati wa msimu wa vuli 1942 na kumwambia Stalin: 'Waache wale wanaume ambao waliitwa 1941 warudi nyumbani. Wamekuwa wakipigana kwa mwaka tayari.' Hakuna mtu ambaye angewahi kufikiria kufanya hivyo."

Maria Andreeva, ambaye mume wake na binamu yake walisajiliwa na kutumwa Ukraine, anaona maoni ya Bw Kartapolov kuwa matusi.

"Anathubutu kufananisha operesheni maalum ya kijeshi na Vita vya Pili vya Dunia," Maria anasema. "Wakati huo lengo la Urusi lilikuwa kuokoa maisha. Tulikuwa tumeshambuliwa. Kulikuwa na usajili wa wanajeshi kamili na sheria ya kijeshi. Ni kinyume kabisa na kile kinachotokea sasa."

Maria anasema kwamba hafanyi kampeni tu kuwarudisha wanafamilia wake. Anataka kuzuia Warusi zaidi kuitwa na kutumwa vitani.

"Hatutaki wimbi la pili la usajili wa wanajeshi," anasema. "Tunapinga raia kutumiwa katika mzozo wa kijeshi. Na tunataka raia wote wa Urusi kuelewa hili linaweza kuwaathiri wao pia.

"Watu wengine wanafanya mambo kama mbuni. Wanaweka vichwa vyao mchangani na kujaribu kutofikiria juu ya kile kinachotokea. Ninaweza kuwaelewa. Ni vigumu kukubali kwamba, katika nchi yako, serikali haihitaji wewe kuwa na furaha. Lakini ikiwa watu wanataka kuishi, ama wakati huu au baadaye wanahitaji kutambua hili na kusema kwamba hawakubaliani nalo."

.
Maelezo ya picha, Maria Andreeva anafanya kampeni ya kuzuia Warusi zaidi wasisajiliwe na kutumwa vitani

Kuna uwezekano kiasi gani wa "wimbi la pili" la usajili wa wanajeshi nchini Urusi? Desemba iliyopita Rais Putin alionekana kuliondoa hilo, lakini kwa sasa hali ikoje? Moja kwa moja kwenye runinga ya Urusi kiongozi huyo wa Kremlin alidai kuwa mnamo 2023 mamlaka ya Urusi ilifanikiwa kusajili karibu watu nusu milioni wa kujitolea kupigana nchini Ukraine.

"Kwa nini tunahitaji watu kujisajili kuwa wanajeshi? Jinsi mambo yalivyo hakuna haja," kiongozi wa Kremlin alihitimisha.

Bila shaka, "mambo yalivyo" haimaanishi "hayatatokea kamwe". Hali zinaweza kubadilika.

Kwa mfano, mnamo Machi 2022 Rais Putin alitangaza: "Wanajeshi waliosajiliwa hawashiriki na hawatashiriki katika mapigano. Hakutakuwa na mwito wa ziada wa wanajeshi wa akiba. Wanajeshi wenye taaluma pekee ndio wanaoshiriki."

"Usajili wa muda" ulitangazwa miezi sita baadaye.

Ili kuongeza ufahamu Maria na wake wengine wa wanajeshi wa akiba waliosajiliwa na kupelekwa vitani wameanza utamaduni mpya. Kila Jumamosi hujifunga kitambaa cheupe na kusafiri hadi katikati ya Moscow.

Karibu na kuta za Kremlin huweka maua kwenye kaburi la mwanajeshi asiyejulikana. Mikarafuu ya rangi nyekundu huwekwa na moto usiozima kuwashwa. Ni aina yao ya maandamano ya amani.

.

Lakini jamii ya Kirusi inaufahamu kiasi gani? Je, kuna hamu kiasi gani kutoka kwa umma ya kutaka kujua kile wanachosema familia za wanajeshi wa akiba waliopelekwa vitani? Antonina anasema tangu mpenzi wake aliposajiliwa hajapata kuungwa mkono sana na wale walio karibu naye. Alipopokea karatasi zake za wito mnamo Oktoba 2022, aliomba marafiki waendelee kumfuatilia kwa karibu Antonina.

"Walinialika kusherehekea mwaka mpya nao mwaka mmoja uliopita," anasema. "Lakini jioni nzima waliendelea kuniambia kuwa mume wangu hakustahili kwenda huko [Ukraine]."

Antonina anadai kuwa, licha ya kugundulika kuwa na vidonda vya tumbo, mpenzi wake alipelekwa katika kitengo cha mashambulizi nchini Ukraine. Anasema kwamba alimpigia simu tarehe 4 Desemba.

"Alikuwa akilia. Anaogopa. Ilionekana kana kwamba alikuwa ananiaga."

Anasema alipiga simu tena tarehe 13 Desemba. Hiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kusikia kutoka kwake. Antonina anasema tangu wakati huo aliambiwa kwamba mpenzi wake alijeruhiwa akiwa vitani.

"Kuna baadhi ya watu ambao wanataka kupigana. Wanaojitolea kwa ajili ya hilo na kusaini mikataba," Antonina anasema. "Wacha wapigane. Lakini turudishie waume zetu ambao hawataki kuwa huko. Wametimiza wajibu wao kwa nchi yao. Warejeshe nyumbani.

"Nilikuwa na heshima kubwa kwa Vladimir Putin. Sasa siegemei upande wowote. Bado naona vigumu kuamini kwamba anajua mambo ya aina hii yanatokea. Lakini kama kweli anatuona sisi kama wasaliti kwa kuwataka waume zetu, sielewi kwa nini ana mtazamo huu kwa wananchi ambao waliwahi kumpigia kura."

Imefasiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi