Ukraine yasema imeidungua ndege ya kijasusi ya Urusi A-50

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ndege ya Uruysi aina ya A- 50

Jeshi la Ukraine linasema kuwa limeidungua ndege ya kijasusi ya jeshi la Urusi kwenye Bahari ya Azov, katika kile ambacho wachambuzi wanasema kitakuwa pigo kwa uwezo wa kijeshi wa Moscow.

Mkuu wa jeshi Jenerali Valerii Zaluzhnyi amesema jeshi la anga "limeiharibu" ndege ya kutambua rada ya masafa marefu ya A-50, na kituo cha udhibiti wa anga cha Il-22.

Ndege hiyo aina ya A-50 hutambua ulinzi wa angani na kuratibu mashambulizi yanayofanywa na ndege za kijeshi za Urusi.

Ukraine imeshindwa kufanya mashambulizi makubwa hivi karibuni dhidi ya vikosi vya Urusi kusini-mashariki.

Maafisa wa Urusi walisema "hawana habari" kuhusu mashambulizi hayo, lakini wachambuzi mashuhuri wa Urusi wanaounga mkono vita wamesema kupotea kwa ndege hiyo aina ya A-50 ni pigo kubwa .

Idhaa moja maarufu ya kijeshi, Rybar, ilisema kwamba - ikiwa habari hiyo ya Ukraine kuhusu hasara ya Urusi itathibitishwa - itakuwa "siku nyingine nyeusi kwa jeshi la anga la Urusi".

Kituo kingine kilisemakwamba kituo hicho cha amri cha Il-22 kilishambuliwa kimakosa na Urusi .

Jenerali Zaluzhnyi alisema kwenye Telegram kwamba jeshi la anga la Ukraine "lilipanga na kuendesha vyema" operesheni katika eneo la Azov, kusini-mashariki mwa Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Ukraine Mykola Oleshchuk alitoa maoni yake kuhusu kutunguliwa kwa ndege hiyo kwenye chapisho la Telegram, lakini hakutoa maelezo.

Justin Bronk, mtaalamu wa vita vya anga kutoka taasisi ya ulinzi ya Rusi, aliambia BBC kwamba ikiwa itathibitishwa kupoteza ndege aina ya A-50 itakuwa "hasara kubwa sana na ya aibu" kwa jeshi la anga la Urusi.

Alielezea ndege aina ya A-50 kama "jukwaa kuu la amri, udhibiti na ufuatiliaji" ambalo hutoa kwa ndege za Urusi na mifumo ya makombora ya kutoka ardhini hadi angani "tahadhari ya mapema na habari kuhusu ndege za Ukraine zinazoruka chini chini".

Aliongeza kuwa kuna "idadi ndogo " ya ndege hizi ndani ya jeshi la anga la Urusi, na "wahudumu wachache waliofunzwa, kumaanisha kwamba kupoteza moja itakuwa pigo kubwa".

Frank Gardner, mwandishi wa habari wa usalama wa BBC, alisema hatua hiyo ni "habari ndogo na nzuri kwa upande wa Ukraine ambayo nimekuwa na habari mbaya chungu nzima."

Alisema hali kwa ujumla "si nzuri kwa Ukraine", kwani inashughulikia uhaba wa risasi, ari ya chini kati ya wanajeshi wake na kuendelea kwa mashambulio ya Urusi kwenye miundombinu yake.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla