Biden azindua pendekezo la Israel la kumaliza vita na Gaza

.

Chanzo cha picha, EPA

Rais wa Marekani Joe Biden amewataka Hamas kukubali pendekezo jipya la Israel la kumaliza mzozo wa Gaza, akisema kuwa "ni wakati wa vita hivi kumalizika".

Pendekezo hilo la sehemu tatu litaanza kwa kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa wiki sita ambapo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litajiondoa katika maeneo yenye wakazi wengi wa Gaza.

Pia misaada ya kibinadamu "itaongezeka", pamoja na kubadilishana baadhi ya mateka kwa wafungwa wa Kipalestina.

Makubaliano hayo hatimaye yatasababisha "kusitishwa kwa uhasama" na mpango mkubwa wa ujenzi mpya wa Gaza.

Hamas ilisema inaliona pendekezo hilo kuwa "chanya".

Akizungumza katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa, Bw Biden alisema kuwa awamu ya kwanza ya mpango huo uliopendekezwa itajumuisha "usitishaji kamili wa vita", kuondolewa kwa vikosi vya IDF kutoka maeneo yenye watu wengi na kubadilishana mateka kwa wafungwa wa Kipalestina.

"Kwa kweli huu ni wakati muhimu," alisema. "Hamas inasema inataka kusitishwa kwa mapigano. Makubaliano haya ni fursa ya kuthibitisha kama kweli wanamaanisha."

Kusitishwa kwa mapigano, aliongeza, kutaruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kufikia eneo lililokabiliwa na vita, "malori 600 yakibeba misaada kuingia Gaza kila siku".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Awamu ya pili ingeshuhudia mateka wote waliosalia wakirudishwa, wakiwemo wanajeshi wa kiume. Usitishaji wa mapigano kisha ungekuwa "kukomesha uhasama, milele."

Miongoni mwa wale ambao wameitaka Hamas kukubaliana na pendekezo hilo ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron, ambaye alisema kwenye mtandao wa X ni kwamba kundi hilo "lazima likubali mpango huu ili tuone kusitishwa kwa mapigano".

"Kwa muda mrefu tumekuwa tukitafuta kusitishwa kwa mapigano na kunaweza kugeuzwa kuwa amani ya kudumu ikiwa sote tuko tayari kuchukua hatua zinazofaa," Bwana Cameron aliongeza. "Wacha tuchukue fursa hii kumaliza mzozo huu."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alikaribisha maendeleo hayo katika mtandao wa X, zamani ukijulikana kama Twitter. Alisema ulimwengu "umeshuhudia mateso mengi [na] uharibifu huko Gaza" na kuongeza ni "wakati wa kusitisha vita".

"Ninakaribisha mpango wa [Rais] Biden [na] kuhimiza pande zote kuchukua fursa hii kwa ajili ya kusitisha mapigano, kuachiliwa kwa mateka wote, kuhakikishiwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu [na] hatimaye amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati," aliongeza.

Katika hotuba yake, Bw Biden alikiri kwamba mazungumzo kati ya awamu ya kwanza na ya pili yatakuwa magumu.

Hivi majuzi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa akisema kwamba alikuwa akipinga kabisa kukubali kusitisha vita kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano - na kufanya rejeleo la Bw. Biden kuhusu mwisho wa vita kuwa muhimu sana.

Ingawa mpango huo unajumuisha maelezo mengi kutoka kwa duru zilizopita za mazungumzo ambayo hayakufanikiwa, Marekani inatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano milele, na hilo linaonekana kuwa ni makubaliano makubwa ambayo yamepangwa kujaribu kuwarejesha Hamas kwenye mazungumzo kwa masharti ambayo tayari wamesema watayakubali.

Usitishaji wa kudumu wa mapigano umekuwa mojawapo ya matakwa muhimu ya kundi hilo.

Awamu ya tatu ya pendekezo hilo ingeshuhudia mabaki ya mateka wote waliofariki wa Israel yakirejeshwa, pamoja na "mpango mkubwa wa ujenzi upya" kwa msaada wa Marekani na kimataifa wa kujenga upya nyumba, shule na hospitali.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika maelezo yake, Bw Biden alikiri kwamba baadhi ya Waisraeli - ikiwa ni pamoja na maafisa ndani ya serikali ya Israel - huenda wakapinga pendekezo hilo.

"Nimeutaka uongozi wa Israel kukubali mpango huu," alisema. "Bila kujali shinikizo lolote [la kisiasa] linalofuata.

Rais wa Marekani pia alihutubia moja kwa moja watu wa Israel, akiwaambia kwamba "hatuwezi kuacha fursa hii ipotee".

Hasa, Bw. Biden alisema kuwa Hamas sasa imedhohofishwa kiasi kwamba haiwezi tena kurudia mashambulizi kama ya tarehe 7 Oktoba - ishara ya uwezekano wa Waisrael kwamba Marekani inaona vita vimemalizika.

Katika taarifa yake, Waziri Mkuu Netanyahu alisisitiza kuwa vita hivyo havitamalizika hadi malengo yake yatimizwe, ikiwa ni pamoja na kuwarejesha mateka wote na kuondolewa uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas. Alisema mpango wa hivi punde zaidi utairuhusu Israel kushikilia kanuni hizi.

Hamas, kwa upande wake, ilisema kwamba inaliona pendekezo hilo kuwa "chanya" kwa sababu ya wito wake wa kusitishwa kwa mapigano ya kudumu, kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka Gaza, ujenzi mpya na kubadilishana wafungwa.

Pendekezo hilo limepitishwa kwa Hamas kupitia wapatanishi walioko Qatar.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliwaita viongozi wenzake wa Jordan, Saudi Arabia na Uturuki kujaribu kujenga uungaji mkono pendekezo hilo.

Bw Blinken "alisisitiza kuwa Hamas inapaswa kukubali mpango huo na kwamba kila nchi yenye uhusiano na Hamas inapaswa kuishinikiza kufanya hivyo bila kuchelewa," msemaji wa serikali Matthew Miller alisema Ijumaa usiku.

Huku akikabiliwa na ongezeko la vifo vya raia huko Gaza, Rais Biden amekabiliwa na ukosoaji unaoongezeka wa ndani juu ya kiwango cha msaada wa Marekani kwa Israel, na anatoa wito wa kufanya zaidi kuhimiza pande zinazozozana kufanya mazungumzo.

Mapema wiki hii, hata hivyo, Ikulu ya White House ilisema kwamba haiamini kuwa operesheni za Israel huko Rafah ni sawa na "operesheni kubwa ya ardhini" ambayo inaweza kuvuka mstari mwekundu na kusababisha mabadiliko yanayowezekana katika sera ya Marekani.

Kauli hiyo imewadia baada ya mashambulizi ya anga ya Israel na kusababisha moto kuwaua Wapalestina 45 siku ya Jumapili.

Zaidi ya 36,000 wameuawa kote Gaza tangu kuanza kwa vita, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

Vita hivyo vilianza mwezi Oktoba wakati watu wenye silaha wa Hamas walipoanzisha mashambulizi dhidi ya Israel ambayo hayajawahi kushuhudiwa, na kuua takriban watu 1,200 na kuwarejesha 252 Gaza kama mateka.