Je, Marekani inafanya nini kuipa Iran inachotaka bila vita vya moja kwa moja na Israel?

Mnamo Januari 2024, Mashariki ya Kati ilikumbwa na mzozo. Vita vilizuka kati ya Israel na Hamas huko Gaza. Kundi la waasi wa Houthi liliteka nyara meli katika Bahari ya Shamu.

Iran ilifanya shambulizi la kombora ndani ya nchi jirani ya Pakistan.

Shambulio hilo liliwashtua wengi. Pakistan ilishtushwa sana na hili kwa sababu wote wawili ni washirika. Katika kujibu, Pakistan pia ilishambulia Iran. Nchi zote mbili zimetaja mashambulizi hayo kuwa ni ya kujilinda na kulenga maficho ya magaidi katika mpaka.

China iliingilia kati na kuzitaka pande zote mbili kuacha mashambulizi huku kukiwa na mvutano unaoongezeka.

Hili halikuwa shambulio pekee lililofanywa na Iran mwezi Januari ili kuimarisha vikosi vyake.

Iran pia imefanya mashambulizi ndani ya nchi washirika wake Syria na Iraq.

Pia inaonekana nia ya kushambulia Israeli. Imeishutumu Iran kwa kuwaua maafisa wakuu wa usalama katika shambulio la anga la Israel nchini Syria.

Mvutano umeongezeka katika siasa za Mashariki ya Kati ambazo tayari zimechafuka. Katika makala haya tutajaribu kuelewa Iran inataka nini.

Mhimili wa Upinzani katika Mashariki ya Kati

Nigar Mortzawi, mwandishi wa habari wa Iran na mtafiti mkuu katika Kituo cha Sera ya Kimataifa, anaamini kwamba 'Mhimili wa Upinzani' ni muungano usio rasmi wa makundi yasiyo ya Dola ya Kiislamu katika Mashariki ya Kati ambayo ni washirika wa Iran.

Hizi ni pamoja na Hezbollah ya Lebanon, vikundi vya wanamgambo wa Shia wa Iraq, Hamas na vikundi vya Houthi.

Iran inayaona makundi hayo kuwa washirika dhidi ya maadui zake, Marekani na Israel.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2002, Rais George Bush wa Marekani alizitaja Iran, Iraq na Korea Kaskazini kuwa mhimili wa uovu na tishio kwa amani ya dunia.

"Mhimili wa upinzani ni ule ulioundwa dhidi ya utawala huo wa Marekani. Sisi sio waovu. Lakini Marekani imeeneza machafuko katika eneo letu. Wanasema watapinga na kupigana hadi nchi hiyo itasimamisha shughuli zake," Nigar Mortzawi alibainisha.

Hivi karibuni, mashambulizi ya roketi na makombora yalifanywa kwenye kambi ya jeshi la anga la magharibi mwa Iraq ambapo wanajeshi wa Marekani walikuwa wamekaa. Wanajeshi wengi walijeruhiwa katika shambulio hilo.

Kundi lenye uhusiano na Iran, Islamic Resistance, limedai kuhusika na shambulio hilo.

Nigar Mortzawi anasema kuwa mapigano kwenye mpaka wa Iran na Pakistan hayana uhusiano wowote na mhimili wa upinzani. Lengo lake ni kundi la ndani la Baluchi, ambalo Iran inalichukulia kuwa shirika la kigaidi.

Nchi nyingi za Magharibi zimetangaza makundi mengi ya mhimili wa upinzani kuwa ni mashirika ya kigaidi.

Niqar Mortzawi alisema kundi la Houthi nchini Yemen lilianza kuandamana kudai haki za wenyeji miongo miwili iliyopita.

Kundi la Houthi la Yemen linaiona Israel kama adui na limezidisha mashambulizi dhidi ya meli za wafanyabiashara katika Bahari ya Shamu ili kuonesha uungaji mkono kwa mwanachama wa Hamas tangu kuanza kwa vita vya Israel huko Gaza.

Kujibu, Marekani na Uingereza zilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Houthi.

Kwa mujibu wa Nigar Mortzawi, kundi hilo linapata uungwaji mkono wa kiuchumi na kisiasa kutoka Iran. Kundi hilo linafanya kama Iran inavyosema. Hii inaruhusu Iran kutoa changamoto ya kijeshi isiyo ya kawaida kwa wapinzani wake.

Iran haina jeshi kubwa au rasilimali za kutosha kupambana na maadui wenye nguvu.

Hivyo imejenga uhusiano na makundi ya upinzani yenye nia moja.Lakini haijulikani Iran imejitolea vipi kusaidia makundi haya.

"Iran inasema haya ni makundi yanayojitawala na inayaunga mkono tu kwa sababu yana lengo moja. Ninakubaliana na ripoti za kijasusi za Marekani kwamba Iran haikuwa na jukumu la kupanga mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel kutoka Gaza," alibainisha Nigar Mortzawi.

"Maafisa wa Iran walitoa taarifa mbili tofauti. Kwa upande mmoja, waliunga mkono hatua hiyo kimsingi, na kwa upande mwingine, walisema ni hatua ya Wapalestina."

Kuna tofauti za maoni kati ya mhimili wa upinzani na Iran katika masuala mengi. Lakini ili kuelewa jukumu la Iran, ni muhimu kuangalia historia yake, anasema Nigar Mortzawi.

Mabadiliko ya utawala nchini Iran

Iran ya leo ni Jamhuri ya Kiislamu. Lakini kabla ya hapo kulikuwa na ufalme.

Shah wa Iran alitaka kuifanya nchi kuwa ya kisasa kwa msaada wa nchi za Magharibi. Shah Mohammad Reza Pahlavi wa Iran alikuwa na uhusiano wa karibu na Marekani, anasema Maryam Alemzadeh, profesa wa historia na siasa za Iran katika Chuo Kikuu cha Oxford.

"Mohammed Reza Pahlavi alitaka ukuu na alijiona kuwa mshirika wa kutegemewa wa Marekani. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, siasa za nje za Iran zilizingatia ushirikiano wake na Marekani. Hili liliathiri uhusiano wake na nchi nyingine za Mashariki ya Kati."

Wakati huo, mvutano kati ya Marekani, Muungano wa Sovieti, na washirika wao ulikuwa ukiongezeka. Marekani ilitaka mshirika kuongeza ushawishi wake katika Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Shah alizidisha juhudi zake za kuifanya Iran ifanane zaidi na nchi za Magharibi.

Mashambulizi na ghasia zilizuka kote nchini dhidi ya utawala wake. Shah aliikimbia nchi mwaka 1979 baada ya takribani miaka arobaini madarakani.

Ayatollah Khomeini, kiongozi wa kidini aliyehamishwa alirejea Iran na kuwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo.

Mariam Alemzadeh anaamini kuwa mabadiliko makubwa zaidi katika maisha ya watu nchini Iran yametokea tangu Mapinduzi ya Kiislamu. Wanawake waliumbwa kuvaa hijabu na wanaume kuvaa nguo za kawaida.

Mabadiliko ya pili yalikuja katika sera ya kigeni ya Iran. Iran ilianza kuona wengi kama maadui. Mkazo uliwekwa juu ya kukaa mbali na mvutano wa serikali kuu za ulimwengu.

Sambamba na hili, mipango ya kuleta mapinduzi ya Kiislamu katika nchi nyingine pia ilianzishwa. Mariam Alemzadeh anasema kwamba hakuna hatua madhubuti zimechukuliwa kwa sababu ni sehemu ndogo sana ya jumuiya zenye ushawishi mkubwa nchini humo zilizotaka.

Baadhi ya viongozi wa kidini na viongozi wa wapiganaji wa msituni ambao walidumisha uhusiano na Syria, Lebanon na makundi ya Wapalestina walipendelea hili. Lakini viongozi hawa waliwekwa kando ndani ya miaka michache ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Maryam Alemzadeh ameongeza kuwa kwa sababu siasa kuu za Iran zimejikita katika kujenga nchi na kujenga ushirikiano na nchi nyingine za eneo.

Kiongozi mkuu wa Iran alifariki mwaka 1989. Mrithi wake, Ayatollah Ali Khamenei, amekuwa madarakani kwa miaka 35. Lakini ni sura gani ya muundo wa nguvu nchini Iran?

kuhusu ngazi ya madaraka ya nchi ni Kiongozi Mkuu. Kisha kuna serikali iliyochaguliwa, baraza la mawaziri na bunge. Lakini washirika wengi wana sauti katika maamuzi ya sera, anasema Mariam Alemzadeh.

Hii ni pamoja na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Shirika hili la kijeshi liliundwa kwa ajili ya ulinzi wa nchi na kwa ajili ya mapinduzi ya Kiislamu. Sio tu shirika la kijeshi, pia huwa na sauti katika masuala ya fedha na sera za kigeni.

Kuna tofauti za maoni ndani ya IRGC. Baadhi ya viongozi wake hawakuunga mkono siasa kali za kigeni za Kiongozi Muadhamu. Lakini maadamu Kiongozi Mkuu wa sasa Ayatollah Ali Khamenei bado yuko, uamuzi wa mwisho uko kwake, Maryam Alemzadeh alibainisha.

Upinzani dhidi ya itikadi za kisiasa na kitamaduni za Magharibi unaendelea nchini Iran. Huku uhusiano wa Iran na nchi za Magharibi ukizidi kuwa mbaya, itapata wapi washirika wa kiuchumi?

Ushirikiano wa kiuchumi na Urusi na China

"Iran hivi sasa inajenga ushirikiano wa kiuchumi na Urusi, China na mataifa makubwa ya kiuchumi barani Asia," anasema Susan Maloney, makamu wa rais na mkurugenzi wa mpango wa sera za kigeni katika Taasisi ya Brookings yenye makao yake makuu mjini Washington.

"Uongozi wa nchi unataka kuifanya Iran kuwa sawa na Urusi na China.

Kupitia muungano huu, Urusi inapata makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran kwa ajili ya vita vya Ukraine, huku Iran ikipata manufaa ya kiuchumi kutokana nayo."

Urusi na Iran ndizo zenye vikwazo vingi zaidi duniani. Vikwazo vimewekewa Iran kwa sababu inakataa ufuatiliaji wa kimataifa wa vinu vyake vya nyuklia na imekuwa ikishutumiwa kufanya baadhi ya shughuli nje ya nchi.

Susan Maloney anasema nchi hizo mbili zinasaidiana kuepuka vikwazo na kuendeleza biashara. Iran inataka kupata ndege za kivita na zana nyingine za kijeshi kutoka Urusi ili kuimarisha uwezo wake wa kijeshi. Ushirikiano huo kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi.

Uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na China pia umekuwa ukiimarika kwa miaka mingi.

China ni muhimu kwa uchumi wa Iran. Kwa sababu China inanunua mafuta mengi ya Iran licha ya vikwazo vya Marekani. China na Urusi zimeendeleza uhusiano wa karibu na Iran. Kwa sababu Iran ni adui mkubwa wa Marekani, Susan Maloney alibainisha.

Anaongeza kuwa Iran inajenga ushirikiano mpya barani Asia pia. Ushawishi wa Iran nchini Iraq umeongezeka tangu kuondolewa madarakani kwa Saddam Hussein mwaka 2003. Ina jukumu muhimu katika kusambaza umeme na bidhaa nyingine muhimu kwa Iraq.

Kwa upatanishi wa China, Iran imeboresha uhusiano wake na Saudi Arabia na mataifa mengine ya Ghuba. Lakini vikwazo vimegharimu uchumi wa Iran mabilioni ya dola. Ilibidi kulipa gharama kubwa kwa sera zake.

Uwezekano wa mazungumzo na nchi za Magharibi

Viongozi wa Iran wanaona majirani zao wa kikanda na sehemu kubwa ya dunia kama tishio, anasema Christine Fontaineros, mtafiti katika Mpango wa Mashariki ya Kati wa Baraza la Atlantiki la Scowcroft.

"Badala ya kufikiria maendeleo ya elimu nchini, teknolojia mpya, uhakika wa chakula na nafasi katika soko la dunia, wanataka kuokoa serikali yao. Hivyo ni vigumu kufanya mazungumzo nao."

Lakini mazungumzo kati ya Iran na nchi za Magharibi hayajakoma kabisa. Kwa mfano, Septemba mwaka jana, kwa upatanishi wa Qatar, makubaliano yalifikiwa kati ya Iran na Marekani kuwaachia huru wafungwa.

Marekani ilikuwa tayari kurudisha nchini Iran dola bilioni 6 zilizonyakuliwa kutoka Iran kutokana na vikwazo. Lakini baada ya Hamas kuishambulia Israel tarehe 7 Oktoba, Marekani na Qatar ziliamua kutoipatia Iran fedha hizo kwa sasa kwa sababu huenda pesa hizo zikatumika vibaya.

Christine Fontaineros anasema hatua zinachukuliwa ili kupunguza hatari kwao wanapokabidhi madaraka kwa kiongozi ajaye, na kwamba shambulio la kombora la kuvuka mpaka litasaidia katika kazi hii.

Viongozi wa Iran wanataka kutuma ujumbe kwa watu wao kwamba taifa hilo liko imara na linaweza kuwalinda dhidi ya makundi ya upinzani. Watu wawaamini viongozi wa nchi na waunge mkono sera zao.

Wengine pia wanaamini kuwa mzozo kati ya Israel na Gaza umepunguza umakini wa ulimwengu kwa shughuli za Iran.

Christine Fontaineros anasema serikali ya Iran inachukua fursa hii kukandamiza maandamano ndani na nje ya nchi. Mwezi Januari, Iran iliiteka tena meli ya mafuta katika Ghuba ya Oman ambayo Marekani iliiteka mwaka jana kwa kukiuka vikwazo.

Iran pia ilianzisha mashambulizi ya makombora katika nchi tatu jirani. Lakini vipi Iran ina nia ya kumaliza vita hivi?

"Iran inataka Israel iangamizwe katika mzozo wa Gaza kwa sababu lengo lake lililotajwa ni kuifuta Israel kwenye ramani ya dunia. Inajua kuwa jambo hili haliwezi kufikiwa. Katika hali kama hiyo, inataka kufanya iwe vigumu kwa nchi jirani za Kiarabu na nyinginezo za dunia kuunda muungano na Israel, na hivyo kupunguza ushawishi wa Israel na Marekani katika eneo hili''.

''Iwapo Iran inaweza kufikia lengo hili, inaweza kusema kwamba uwekezaji wake katika Hamas katika miaka kadhaa iliyopita umezaa matunda," alibainisha. Christine Fontaineros.

Sasa tuje kwenye swali letu kuu. Iran inataka nini? Viongozi wa Iran wanataka kudumisha mamlaka yao.

Pili, Iran inataka kuwa nchi yenye ushawishi mkubwa katika Mashariki ya Kati.

Wataalamu wetu wanasema kuwa badala ya kupambana moja kwa moja na Israel na Marekani, inataka kuongeza nguvu kwa kushirikiana na China na Urusi.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga