Je, Biden hatimaye ataweza kuizuia Iran?" - Jarida la Wall Street

Magazeti ya kimataifa yalitoa maoni yake kuhusu mashambulizi ya Marekani ambayo yalilenga maeneo saba ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Syria na Iraq siku ya Ijumaa, kulingana na taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani.

Jarida la Wall Street, katika tahariri yenye kichwa "Je, Biden hatimaye ataweza kuizuia Iran," lilieleza mashambulizi haya kama "mojawapo ya mashambulizi ya kijeshi yaliyotangazwa sana dhidi ya adui katika historia."

Gazeti hilo lilionyesha kuwa maafisa wa Marekani wamekuwa wakitangaza mashambulizi yajayo kwa siku kadhaa kujibu mashambulizi ambayo yalilenga kambi ya kijeshi ya Marekani huko Jordan na kupoteza maisha ya wanajeshi watatu wa Marekani.

Gazeti hilo pia lilifuatilia dalili kutoka kwa maafisa wa utawala wa Rais Biden kwamba mashambulizi haya yatakuwa dhidi ya wanamgambo na sio dhidi ya Iran, na kubainisha kuwa kulikuwa na uvujaji wa vyombo vya habari kuonyesha kwamba Marekani inasubiri kuelewa hali ya Mashariki ya Kati zaidi.

Gazeti The Wall Street Journal lilisema kwamba viongozi wa wanamgambo hawawezi kudai kwamba hawakupokea onyo, “na ikiwa kuna wale ambao kati yao hawakuenda mbali na maeneo yaliyolengwa, basi bila shaka hao ndio magaidi walioazimia zaidi ulimwenguni.”

Gazeti hilo lilimfuatilia Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin siku ya Alhamisi likidokeza “uwezo wa kufanya zaidi,” likisema kwamba swali hapa ni: Je, Marekani itafanikiwa kutumia uwezo huo wa kutosha kutuma ujumbe wa kuzuia vita?

Jarida la Wall Street lilichukulia kwamba mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Marekani hadi sasa ni dhaifu na hayajafanya kazi iliyokusudiwa, likisema kwamba maonyo mengi ya Marekani yaliyotangulia mashambulizi haya yanatuma ujumbe kwamba Marekani haitaki kuleta madhara makubwa kwa wanamgambo, na hii kwa upande mwingine inaweza kutafsiri kama hofu.

Gazeti hilo lilisema, "Mashambulizi dhidi ya Wamarekani yanawezekana hayataisha isipokuwa hofu ya adui ya kuongezeka kwa mashambulizi inazidi hofu ya Rais Biden ya kitu kile kile."

"Hatutaki vita"

Katika gazeti la London Rai Al-Youm, kuna makala ya mwandishi wa Kipalestina Kamal Khalaf, yenye kichwa, "Uchokozi wa Marekani hautabadilisha chochote."

Khalaf aliamini kwamba siku tano za vitisho vya mara kwa mara vya Marekani vya kuanzisha mashambulizi nchini Syria na Iraq "zilitosha kuhamisha makao makuu ya kijeshi na kujiandaa kwa shambulio lililotarajiwa, ambalo ndilo lililotokea kabla ya mashambulizi ya Marekani ... pamoja na Washington kuitaarifu serikali ya Iraq mapema kuhusu tarehe ya mashambulizi hayo."

Mwandishi alishangaa juu ya manufaa ya mashambulizi haya ikiwa utawala wa Marekani ungejua kwamba "uchokozi huu hautazuia mashambulizi dhidi ya vikosi vyake nchini Syria na Iraq?"

Khalaf aliendelea, akisema kwamba ikiwa utawala wa Marekani haukujua kwamba mashambulizi hayo hayana umuhimu wowote, "iligundua saa chache baada ya uvamizi, wakati kituo chake cha Al-Tanf kwenye mpaka wa pembetatu wa Syria-Jordan-Iraqi kushambuliwa na droni kutoka Iraq, na kambi ya Ain al-Assad pia ilishambuliwa kwa kombora, pamoja na uwanja wa Koniko nchini Syria - katika ujumbe wa wazi kutoka kwa upinzani kwamba mashambulizi hayajaathiri, na tunaendelea."

Mwandishi aliona kwamba utawala huu wa Marekani “unahatarisha uwepo wake, wanajeshi, maslahi na nafasi yake katika Mashariki ya Kati, kwa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen, Iraq, na Syria, na kuishinikiza na kutishia Lebanon,” wakati utawala huo unapaswa kumlazimisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusitisha vita huko Gaza kwa sababu "hiki ndicho ... Kitu pekee kinachookoa kuokoa Marekani kutokana na ongezeko hili la mashambilizi na matukio haya ya kijeshi yenye matokeo yasiyoweza kutathminiwa.

Khalaf alisisitiza kwamba mashambulizi "yaliyoanzishwa na Marekani katika jiografia ya upinzani kwenye eneo letu hayatabadilisha ukweli wa mabadiliko ya asili ya kimkakati Mashariki ya Kati."

'Msimamo usiona na maana'

The Jerusalem Post ilichapisha makala ya Jonathan Spyer yenye kichwa “Ni nani aliyewaua wanajeshi watatu wa Marekani katika kambi ya Tower 22?”

Spyer aliamini kwamba yeyote aliyetekeleza shambulio hilo "aliweza, kwa mpigo mmoja, kumaliza kampeni iliyoongozwa na Marekani nchini Iraq na Syria katika picha ya sasa ya Mashariki ya Kati," na akazifanya zote mbili wafuasi wa Marekani na wapinzani katika eneo hilo kutarajia jinsi mwitikio wa Marekani ungekuwa.

Spyer aliashiria kundi linalojiita "Islamic Resistance nchini Iraq," akibainisha kuwa ni chama ambacho kimekuwa kikidai kuwajibika tangu Oktoba 2023 kwa mashambulizi dhidi ya kambi za Marekani nchini Iraq na Syria.

Mwandishi huyo alisema kuwa jina la " Islamic Resistance nchini Iraq" ni jina la pamoja linalorejelea idadi ya wanamgambo wa Kishia ambao ni waaminifu kwa Iran, badala ya kundi maalum.

Spyer aliamini kwamba wanamgambo wa Iraq hutumia aina hii ya jina kulingana na mkakati wa zamani wa kuepusha hatua za kisasi za Marekani dhidi ya kundi maalum, pamoja na ukweli kwamba wanamgambo hawa ni silaha za kijeshi za vyama vya kisiasa ambavyo ni sehemu ya serikali ya Iraqi, na wanataka kuhakikisha kuendelea kupata mfumo wa kifedha wa Marekani, kulingana na madai yake.

Mwandishi huyo alidokeza kwamba "Upinzani wa Kiislamu nchini Iraq" ni mwavuli wa wanamgambo kadhaa, wakiwemo: Kataib Hezbollah na Harakat al-Nujaba, akisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba moja ya makundi haya mawili (hasa Kataib Hezbollah, kutokana na rekodi ya kushambulia maeneo ya Marekani kabla na baada ya Oktoba 7) ndiye aliyefanya shambulio katika kambi ya Burj 22

Spyer amesema makundi hayo mawili yana mfungamano na Kikosi cha Quds ambacho ni kikosi maalum cha Jeshi la Walinzi wa Iran na kubainisha kuwa hakuna kundi lolote linalojaribu kuficha mfungamano huo.

Tehran, kwa upande mwingine, inasisitiza kukataa uhusiano wowote kati yake na wanamgambo wanaoshambulia vikosi vya Marekani huko Iraqi na Syria - "msimamo usiona na maana," maoni ya mwandishi.

Imetafsiriwa na Asha Juma