'Biden anacheza na moto Mashariki ya Kati na kuhatarisha Vita vya Tatu vya Dunia' - New York Post

Gazeti la New York Post limechapisha makala ya mwandishi Michael Goodwin, chini ya kichwa, "Biden anacheza na moto Mashariki ya Kati na kuhatarisha vita vya tatu vya dunia."

Godwin anaanza kwa kusema, tangu kuanzishwa kwa Taifa la Israel mwaka 1948 marais wa Marekani wamekuwa wakijaribu kujiepusha na sera zinazoweza kuhatarisha uwepo wa taifa hilo.

Marais hawa walifuata kanuni isiyoandikwa, kwamba "ikiwa Marekani itajitenga na Israel, nchi jirani zinazoizunguka nchi hiyo zitaifuta kwenye uso wa dunia.

Godwin anazungumzia mikataba ya amani iliyosainiwa na Israel, Misri na Jordan, na Mkataba wa Abraham, ambapo nchi nne za eneo hilo ziliitambua Israel na kuanzisha uhusiano wa kiuchumi, kidiplomasia na usalama.

Mafanikio haya hayamaanishi kutokuwepo kwa tishio dhidi ya Israel. Vikundi kama vile Hamas, Hezbollah, Ansar Allah al-Houthis, na mavuguvugu mengine ya kigaidi, bado vina lengo la kuifuta Israel.

Godwin anasema Biden ameanza kuchukua hatua ambazo zitaiacha Israel katika tishio ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia yake.

Miongoni mwa hatua hizi, kulingana na mwandishi; kuisukuma Israel kukubali makubaliano ya amani huko Gaza na kukubali kuanzishwa taifa la Palestina, ili kuwaridhisha wapiga kura Waislamu nchini Marekani pamoja na vijana wenye itikadi kali katika Chama cha Democratic.

Ili kumshawishi Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu kuhusu hatua hizo mbili [ambazo anazikataa vikali], Biden anamwahidi Netanyahu makubaliano ya kurekebisha uhusiano kati ya Israel na Saudi Arabia.

Saudi Arabia itafaidika na mpango huu kwa kupata teknolojia ya nyuklia ya kutoka Marekani kwa matumizi ya kiraia, pamoja na kupata ulinzi wa kijeshi kwa Ufalme.

Kulingana na mwandishi huyo, Biden anataka kufikia malengo haya yote kabla ya kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais: Kusimamisha vita vya Gaza, kurekebisha uhusiano kati ya Saudia na Israel, na kutangaza kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Goodwin, anaamini Biden, kwa ajili ya malengo yake, hajali msimamo wa Israel, wala hajali hatari ya Iran - ambayo haijampa Biden uhakika kuwa imeacha matamanio yake ya kuwa na silaha za nyuklia na lengo lake la kuifuta Israel.

Mwandishi anasema si Iran au mawakala wake wanaopenda mikataba ya amani au kuanzisha uhusiano wa kibiashara na Israel, bali wanashikilia suala lao la msingi kuhusu uwepo wa Israel katika eneo hilo.

Godwin anamaliza kwa kusema: “Kwa hali hiyo, Biden anacheza na moto ambao unaweza kuiteketeza Mashariki ya Kati na kuanzisha vita vya tatu vya dunia.”

'Njia pekee ya kutuliza mvutano Mashariki ya Kati'

Katika gagazeti la Uingereza, kuna tahariri ya The Independent yenye kichwa cha habari "Vita vitaendelea Mashariki ya Kati hadi Wapalestina watakapotangaza kuanzishwa kwa taifa lao."

Gazeti hilo linaeleza kuwa Biden anataka kuonekana kama rais ambaye amekabiliana vikali na vitisho vinavyokabili maslahi ya Marekani duniani kote. Biden anasema:

"Haya yamewahi tokeao huko nyuma. Bill Clinton alishambulia kiwanda cha dawa nchini Sudan kujibu mashambulizi yaliyolenga balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998.”

Gazeti hilo linaandika: Lazima tuelewe ni kwa nini majeshi ya Marekani yamewekwa katika eneo la mbali la jangwa huko Jordan kwenye mpaka wa Syria na Iraq. Kambi ya Tower 22 inatukumbusha kwamba Marekani bado ipo Mashariki ya Kati katika jaribio la kudhibiti ushawishi wa Urusi na Iran katika eneo hilo.

Katika muktadha huu, The Independent inaonya juu ya matokeo ya kujiondoa kabisa kwa Marekani kutoka eneo hilo, ikiwa ina nia ya kukomesha vita vya milele.

Gazeti hilo linaamini wanasiasa wa Marekani na wa Magharibi wanapaswa kujua kwamba "njia pekee ya kutatua mivutano ya kudumu Mashariki ya Kati inayowakabili wananchi wa Palestina na kuanzisha taifa la Palestina."

'Vita vya kisaikolojia vinavyoendeshwa na Hamas'

Katika gazeti la Jerusalem Post tahariri yenye kichwa “Serikali duniani kote zina jukumu la kuishinikiza Hamas kufikia makubaliano ya kuwaachilia mateka.”

Gazeti hilo lilifuatilia ripoti zilizosambaa wiki kadhaa kuhusu kuachiliwa kwa mateka.

Ikiwa ni pamoja na ripoti iliyochapishwa na Wall Street Journal ikisema “kutoelewana kati ya viongozi wa Hamas kulisababisha kuchelewa kuhitimishwa kwa makubaliano yanayoungwa mkono na Marekani.”

Gazeti la Jerusalem Post lilisema, Waisraeli, na hata Wayahudi duniani kote, wanasubiri kwa hamu kukamilishwa kwa mpango huu.

Gazeti hilo linaona, kuchelewa huku ni dhihirisho jingine la vita vya kisaikolojia vinavyofanywa na Hamas, kwa wateka hao ambao wamekuwa wakihangaika kwa takriban siku 120 katika mazingira ya kutisha bila nguo za baridi na chakula cha kutosha.

Linabainisha kuwa mpango uliopendekezwa unagawanya mateka katika makundi matatu; kundi la raia, kundi la askari, na miili ya waliofariki. Mateka hawa watakabidhiwa kwa Israel ndani ya siku 40 baada ya kusitishwa kwa mapigano.

The Jerusalem Post ilibaini mpango huu ulipata uungwaji mkono kamili wa Marekani, na utawala wa Biden umethibitisha zaidi ya mara moja.

Gazeti hilo limemnukuu afisa wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo akisema, Hamas haitatia saini pendekezo hili bila ya hakikisho kwamba Israel itakomesha vita.

Kwa upande mwingine, gazeti hilo liliashiria msisitizo wa serikali ya Israel na Netanyahu kwamba jeshi la Israel halitaondoka katika Ukanda wa Gaza kabla ya kupata ushindi, ambao ni kuliondoa vuguvugu la Hamas.

Gazeti hilo linasema, pande hizo mbili zingefanya maafikiano na kukamilisha makubaliano hayo. Na ni muhimu kutoa shinikizo kubwa kwa Hamas kukubaliana na makubaliano hayo mara moja na kukomesha ucheleweshaji huu.”